Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Dkt .Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala pamoja na miradi mingine mikubwa ya kimkakati.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 22,2025 katika ukumbi mdogo wa mikutano uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge alieleza ,hafla hiyo itafanyika 31,Julai 2025 .
Alieleza, Rais Samia pia atazindua safari ya treni ya mizigo kwa njia Reli ya kisasa( SGR), mapokezi ya mabehewa ya MGR na uzinduzi wa Kongani ya Viwanda ya kwala (Kwala Industrial Park)eneo la Kwala Mkoani Pwani.

Alisema , safari ya treni ya mizigo kupitia SGR itazinduliwa rasmi katika Kituo Kikuu cha kuunganishia mabehewa ya mizigo na karakana maalum ya treni hizo maarufu kama Marchalling Yard ambayo ipo katika eneo hilo hilo la Kwala
Kuhusu Bandari Kavu ya Kwala Mhe Kunenge alisema mradi huo utaongeza ufanisi mkubwa kwa kuhudumia wastani wa makasha 823 kwa siku sawa na zaidi ya makasha 300,000 kwa mwaka hatua itakayopunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam kwa zaidi ya asilimia 30.
Aidha alifafanua, Rais Samia anatarajiwa kupokea jumla ya mabehewa 160 ambapo mabehewa 100 ni mapya yaliyonunuliwa na Serikali kwa ajili ya reli ya MGR ,mabehewa 20 yamefanyiwa ukarabati na mabehewa 40 yametolewa na Shirika la Chakula Duniani WFP.
Katika Kongani ya Viwanda ya Kwala ambayo inatajwa kuwa moja ya maeneo makubwa ya viwanda Afrika Mashariki Rais atazindua viwanda 7 ambavyo tayari vimekamilika na kuanza kazi sanjali na viwanda 5 vilivyopo kwenye hatua mbalimbali za ujenzi.
Kunenge aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo muhimu la kihistoria akisisitiza kuwa linadhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha miundombinu ya uchumi wa viwanda na usafirishaji.
Hafla hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa kitaifa na kimataifa ambapo Rais atafanya mkutano mkubwa wa hadhara na wananchi .

Kunenge alisema uzinduzi wa miradi hiyo unaonyesha utekelezaji mahiri wa Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta ya usafirishaji viwanda na biashara ambapo Kwala inabadilika kuwa kitovu cha biashara usafirishaji na uchukuzi kimataifa (International Logistic Hub) .
Faida zinazotarajiwa kutokana na miradi hiyo ni pamoja na kuongeza mapato ya serikali kukuza matumizi ya reli kupunguza uharibifu wa miundombinu ya barabara kulinda mazingira na kuongeza ushindani wa kikanda na ushirikiano wa kiuchumi na nchi jirani zikiwemo DRC Zambia Rwanda Burundi Malawi Zimbabwe Uganda na Sudani ya Kusini.