TABORA

Na Benny Kingson

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ali Hapi, amemwagiza Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Itaga, Manispaa ya Tabora, Mashaka Ramadhani, kurejesha Sh 150,000 alizomdhulumu mkazi wa kijijini hapo.

Agizo hilo limetolewa kwenye mkutano wa hadhara baada ya mkazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Magreth Kashindye, kudai kudhulumiwa na Ramadhani.

“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inawajali wananchi ndiyo maana nimekuja kusikiliza kero zenu. Sipo tayari kuona kiongozi yeyote akitumia cheo chake kuwanyanyasa wananchi,” anasema Hapi.

Amewataka viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza kutenda haki wakati wote na si kutumia ubabe au cheo kudhulumu haki; akikiita kitendo hicho kuwa ni sawa na wizi.

“Nimesikiliza maelezo ya huyu mama na mashahidi wengine wakiwamo viongozi wenzako, ninakupa siku 14 kurudisha fedha zake zote ulizomdhulumu Sh 150,000. Unawajua mliogawana nao. Nataka arejeshewe fedha zake zote,” anasema.

Mbali na hayo, Hapi amempa miezi mitatu kiongozi huyo kubadilika, vinginevyo sheria itachukua mkondo wake, ikiwamo kuondolewa katika nafasi yake.

Baadaye Ramadhani aliwaomba radhi wakazi wa kijiji hicho mbele ya RC, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tabora, Mohamed Katete na Katibu wa CCM Wilaya, Nicholus Malema.

Ramadhani ameahidi kujirekebisha na kwamba hatarudia tabia hiyo.

Kwa upande mwingine, Hapi ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Ofisa Ardhi wa Manispaa na Kamisha wa Ardhi Msaidizi wa Mkoa kuchunguza madai yote ya wananchi kudhulumiwa haki zao ili sheria ichukue mkondo.

Malema amempongeza RC kwa kutanguliza masilahi ya wananchi na kuchukua hatua stahiki kwa wote wanaodhulumu haki za raia.

By Jamhuri