Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewataka wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari bila shuruti pamoja na kutoa risiti za EFD.

Vilevile, Chalamila amewaonya wafanyabiashara wanaotishia kugoma pale ambapo wanatakiwa kulipa kodi, ambapo amesema migomo ni tamko la vita.

Ameyasema hayo leo Mei 22, mwaka huu wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema Taifa linajengwa kwa kodi, hivyo ni muhimu kulipa ili serikali iweze kupeleka huduma kwa Watanzania.

“Natumia rai hii kuwasisitiza wafanyabiashara na watu wote ambao wanapaswa kulipa kodi kwa sheria kuweza kufanya hivyo ili taifa letu liweze kusimamia vizuri misingi ya kupeleka huduma kwa jamii.

“Mara kadhaa tumekuwa tukisikia harufu ya migomo kwa baadhi ya wafanyabiashara na migomo hii huja mara baada ya TRA inapotaka kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria katika magodown au maduka ama katika operesheni za kuangalia matumizi sahihi ya EFD.

“Wafanyabiashara wote watakaoinuka na kutangaza migomo, hii kwetu sisi kama serikali migomo ni tamko la vita. Nitoe rai kwamba Tanzania sio nchi ya kivita ni nchi inayosimamia misingi ya maridhiano ya kujenga upya taifa letu, lakini zaidi la kuvumiliana na kustahimiliana,” amesema.

Aidha Chalamila ametoa wito kwa wafanyabiashara wote wa vinywaji baridi na moto, kuhakikisha wanapouza bidhaa hizo zinakuwa na stemps halisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Pia kumekuwa na trend ya uingizaji wa vinywaji ambavyo havijathibitiwa na mamlaka maalum kama vile TBS na mamlaka zingine, na hata kwa zile ambazo zimezalishwa hapa nchini vipo baadhi ya vinywaji vinauzwa bila stika au stemps huu ni uhujumu wa taifa letu na uhujumu wa afya kwa watanzania. Nitoe rai kwa wafanyabiashara wote wa vinywaji baridi na moto, kuhakikisha wanapouza bidhaa hizo zinakuwa na stemp za TRA ambazo ziko halisi hazijafojiwa,” amesema.

Hata hivyo amesema kumekuwa na malalamiko kwa TRA ambayo yanatokana kwa baadhi ya wafanyabiashara kufanya biashara bila kutoa risiti za EFD na hata pale wanapotoa hua zinakinzana na fedha iliyolipwa na mteja.

“Yaani fedha ya mteja inakuwa kubwa lakini inayoandikwa ni ndogo. Nitumie fursa hii kuwaasa wafanyabiashara wote mko wa Dar es Salaam kwamba ni muhimu kutoa risiti kwasababu mfanyabiashara ni wakala tu wa kukusanya fedha kutoka kwa mwananchi kwenda kwa serikali.

Amezisisitiza kuwa, wanaendeleza operesheni kubwa ili kuwabaini wote wanaofanya kazi hizo kuwa lengo la kuhujumu uchumi wa taifa.

“Mtakumbuka sasa tupo mwishoni mwa mwaka wa fedha wa 2023/24 na kila tarehe 7 ya kila mwezi wafanyabiashara wote wakuu wa taasisi na mashirika hua tunapaswa kupeleka retuin ya paye…naomba wafanye hivyo mara moja ili taifa letu liendelee kupata kodi zitakazokwenda kupeleka huduma kwa watanzania,” amesema Chalamila.

Amewataka wanafanyabiashara kuzingatia sheria kwani serikali iko tayari kupokea maoni, kusikiliza na pengine kufanya mabadiliko ya kisheria pale itakapolazimika kufanya hivyo

“Tukumbukeni wema wa Rais Dkt Samia wa kulijenga taifa na usitafsiriwe vinginevyo bali tuungane pamoja na mkuu TRA nchini Tanzania kulipa kodi kwa hiari, kwani kukwepa kodi sio dili,” amesisisitiza