Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kigoma

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, amezindua rasmi zoezi la ugawaji wa vyandarua vyenye dawa katika ngazi ya kata, mitaa, vijiji na kaya, mkoani humo, ambapo vyandarua zaidi ya milioni 1.7 vitagawiwa bure kwa wananchi katika halmashauri nane za mkoa huo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo leo Mei 27,2025 katika eneo la Ujiji, Manispaa ya Kigoma Ujiji, Andengenye amesema walengwa wa zoezi hili ni wananchi 2,872,007 kutoka kaya 503,303 ambapo hadi sasa wananchi walioandikishwa ni 3,299,402 kutoka kaya 506,762.

Andengenye ameipongeza serikali na wadau wa zoezi hilo ambao ni Global Fund kwa kutekeleza kampeni hiyo, na kusema jumla ya vyandarua vitakavyosambazwa ni 1,775,359 vyenye thamani ya sh. 35,506, 680,000/=.

Hata hivyo, Mhe. Andengenye ametoa rai kwa wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya vyandarua vitakavyogawiwa ili viweze kuleta tija kwenye kupunguza maambukizi ya Malaria Mkoani Kigoma, badala ya kuviuza, kuzungushia bustani, kufugia vifaranga au kuvulia samaki.

Aidha, amesisitiza kwamba ni vyema jamii ielewe vyandarua hivyo havina mahusisano na suala la kupunguza nguvu za kiume ama kushindwa kupata ujauzito kwa wanawake.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ugavi wa MSD Bw. Victor Sungusia ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuendelea kuiamini MSD na kuipatia jukumu hilo adhimu la usambazaji wa vyandarua.

“Tunaishukuru Wizara ya Afya na tupo tayari kuanza zoezi hili la usambazaji kama tuvyoelekezwa, MSD haisambazi vyandarua peke yake lakini inasambaza bidhaa zote za afya ambazo zinapatikana kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini. alisema Sungusia.