Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack amefanya ziara ya kukagua kilimo cha zao la Pamba na Mtama wilayani Kishapu kwa ajili ya kuendelea kuhamasisha wakulima kulima mazao hayo kwa wingi kwa njia za kitaalamu ambayo yatawafanya wakue kiuchumi na mkoa kwa ujumla. 
Telack amefanya ziara hiyo leo Jumatatu Januari 8,2018 wilayani Kishapu kwa kukagua baadhi ya mashamba ya pamba na mtama ambayo yamelimwa na wakulima kwa njia ya kitaalamu na kuwataka wakulima kuendelea kutii magizo ya serikali kwa kulima mazao hayo ya biashara na chakula ambayo yatabadili mfumo wa maisha yao pamoja na kuacha kuishi kwenye nyumba za tembe.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara baada ya kutembelea mashamba ya wakulima katika kijiji na kata ya Shangihilu Telack amewataka wakulima kijijini kuendelea kujikita kulima mazao hayo ya pamba na mtama kwa njia ya kitaalamu ambayo itawafanya kupata mavuno mengi na kuinuka kiuchumi. 
“Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli imejipanga kumuinua mkulima kiuchumi kupitia kilimo na ndiyo maana changamoto zote zilizokuwa zikimkabili mkulima zinatatuliwa ili muweze kunufaika na kilimo chenu , hivyo nawasihi mlime mazao ya pamba na mtama kwa wingi kwani soko lake lipo”,alisema Telack. 
Aidha aliwataka wakulima hao pindi watakapouza mazao yao baadhi ya fedha wazielekeze kwenye ujenzi wa nyumba za kisasa na kuondoa matembe yaliyopo ili kuishi katika nyumba zenye usalama na zisizo na mashaka hasa pale mvua zinapoanza kunyesha kwa hofu ya nyumba kuanguka. 
Pia alitoa agizo kwa wakulima ambao wanalima mazao kwa kuchanganya kwenye shamba moja wakamatwe na kushughulikiwa kisheria kwa sababu wanaonekana kukaidi maagizo ya serikali ya kuhamasisha wakulima kulima kilimo cha kisasa ambacho kitakuwa na tija kwa wananchi katika kuwainua kiuchumi. 
Naye mkuu wa wilaya ya Kishapu Nyabaganga Taraba akisoma taarifa ya utekelezaji wa kilimo wilayani humo katika msimu wa kilimo (2017-18) alisema asilimia 80 ya wakazi wilayani humo ambao wapo 298,554 wanategemea kilimo na katika msimu huu zaidi ya wakulima 24,216 wamejisajili kulima zao la pamba. 
Alisema katika msimu huu (2017-18) wamelenga kulima zao la pamba hekali 177,026 sawa na hekta 70,811 ambapo eneo hilo linahitaji tani 1,770 za mbegu za manyoya au Tani 1,062 za mbegu zisizo na manyoya, na mpaka sasa wakulima wamelima hekta 52,095 na matarajio ya mavuno ni tani 169,454, au kilo milioni 100 za zao hilo. 
Aliongeza kuwa bado wanaendelea kuandikisha wakulima watakao lima zao hilo kwa vile kilimo bado kinaendelea pamoja na kuunda vyama vya ushirika kwa kila kijiji ambavyo vitasaidia wakulima kuwa wamoja pamoja na kuuza mazao yao kwa uhakika bia ya kupunjwa na kupata faida. 
Nao baadhi ya wakulima wilayani humo ambao walibahatika kutembelewa mashamba yao na mkuu wa mkoa,akiwemo Kazimiri Masunga walipaza kilio chao kikuu ambacho kilikuwa ni wadudu waharibufu ambao wameonekana kuishambulia pamba huku dawa ambayo wanaipulizia ya maji ya kuulia wadudu kutokuwa na nguvu tofauti na ya zamani ya mafuta ambayo ilikuwa bora zaidi. 
Naye ofisa kilimo wa kata hiyo ya Shaghihilu Yona William alikiri wadudu hao kushambulia pamba za wakulima na kutolea ufafanuzi kuwa dawa ambayo wanaipulizia (Dudu all) ya kuulia wadudu hao baadhi yao wanaikosea kwa kuzidisha vipimo na kujikuta inakosa nguvu na kutoua wadudu hao. 
Alisema baadhi ya wakulima wamekuwa wakikaidi kutohudhuria kwenye mikutano ya hadhara ambayo hutoa elimu ya dawa hizo za kuulia wadudu pamoja na kuifanya kwa vitendo kwenda kwenye moja ya shamba na matokeo yake wanapoamua kutumia dawa hizo hujikuta wakiikosea na kutoua wadudu. 
Kwa upande wake mkaguzi wa pamba kutoka wilaya ya Kishapu na Shinyanga Thomas Tiluhongelwa alisema dawa zote za kuuliwa wadudu za maji na mafuta zote ni bora isipokuwa dawa ya mafuta ina gharama na ndiyo maana ilisitishwa kuingizwa nchini na kuruhusiwa hiyo ya maji ambayo ina gaharama nafuu ambayo kila mkulima atakuwa na uwezo wa kuinunua, isipokuwa wanatakiwa kufuata masharti yake ambayo hupewa na wataalamu. 
Habari imeandikwa na Marco Maduhu -Malunde1 blog 
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack mwenye ushungi akiwa na mkuu wa wilaya ya Kishapu Nyabaganga Taraba (katikati mwenye nguo ya njano) na aliyepo mkono wa kushoto ni Diwani wa Kata ya Shangihilu Mohamed Hamadi pamoja na wataalamu wa kilimo na mkurugenzi wa halmashauri hiyo Steven Magoiga wakikagua shamba la pamba hekali 22 la mkulima Kazimiri Masunga -Picha na Marco Maduhu- Malunde1 blog

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack akiwa katika shamba la pamba na viongozi mbalimbali

Mkulima wa zao la Pamba Kazimiri Masunga akimuonyesha mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack ukubwa wa eneo alilolima shamba hilo hekali 22, na kutarajia kwenye mavuno kumuinua kiuchumi huku akiomba serikali kuwapatia dawa ya kuua wadudu waharibifu ili wasipate hasara.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack akiangalia wadudu wanavyolishambulia zao hilo la pamba na kutoa maagizo kuhusu ufumbuzi upatikane wa kuwateketeza kwa kupulizia dawa yenye nguvu ya kuua wadudu ili kutowapatia hasara wakulima.
Viongozi wakiwemo wataalamu wa kilimo wakiangalia jinsi pamba ilivyoshambuliwa na wadudu
Mkaguzi wa pamba wilaya ya Kishapu na Shinyanga kutoka bodi ya Pamba Thomas Tiluhongelwa akiangalia wadudu wanavyo shambulia zao hilo la pamba na kumuahidi mkuu wa mkoa kulifanyia kazi ndani ya Siku mbili ilikufahamu ni wadudu wa aina gani wanaoshambulia zao hilo na kuwateketeza kabisa
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack akimpongeza mkulima wa zao la pamba hekali 22 Kazimiri Masunga kwa kutii maagizo ya serikali kulima zao hilo tena kwa kilimo cha kisasa.
Mke wa Kazimiri Felista Kija akipunguza mashina kwenye zao la pamba ili lipate kustawi vizuri
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack akiwataka wataalamu wa Kilimo kuwa karibu na wakulima muda wote mashambani na kutoa elimu kwa wakulima namna ya kupulizia dawa na kuwaua wadudu waharibifu pamoja na kuendelea kulima kilimo cha kisasa
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack akisikiliza maelezo kutoka kwa mkulima wa zao la Mtama Nkalango Ngiti Bundala mkazi wa kijiji cha Mwataga ambaye amelima hekali 270 za Mtama baada ya kuhamasishwa na serikali kupitia mkuu wa wilaya hiyo Nyabaganga Taraba
Mkulima wa zao la Mtama Nkalango Ngiti Bundala mkazi wa kijiji cha Mwataga akimwelezea mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Taraba namna alivyohamasika kulima zao hilo
Eneo lililolimwa hekali 270 za zao la mtama na bwana Nkalango Ngiti Bundala
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack akiwataka wataalamu wa kilimo kuwa karibu na wakulima muda wote mashambani na kutoa elimu kwa wakulima namna ya kulima kwa njia za kitaalamu 
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack akiwa kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha Shangihilu na kuwataka walime kwa wingi mazao ya pamba na mtama angalau kwa kila kaya kekali tatu ,tatu tena kilimo cha kitaalamu ambacho kitawapatia mavuno mengi na kuinuka kiuchumi na kubadirisha mfumo wa maisha yao pamoja na kuondokana na nyumba za tembe. 
Wananchi wa kijiji cha Shangihilu wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wakisikiliza maagizo ya serikali ya kulima mazao ya pamba na mtama ,pamoja na kusomesha watoto wao 
Wananchi wakiwa katika mkutano 
Wananchi wakimsikiliza mkuu wa mkoa wa Shinyanga 
Viongozi wa CCM wakiwa kwenye mkutano huo wa hadhara wakisikiliza maagizo ya serikali ya kulima mazao ya biashara na chakula 

 

Wananchi wakiwa katika mkutano. 
Please follow and like us:
Pin Share