nmb-4Ligi mabingwa Ulaya hatua ya mtoano inaendelea leo na kesho kwa mechi za marudiano ambazo zitapigwa saa 3:45 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Katika mechi za kwanza zilizopigwa wiki iliyopita, matokeo yalikuwa kama ifuatavyo: katika mechi zilizopigwa Jumanne, Astana 1-0 APOEL Nicosiano, BATE Borisov 1-0 Partizan Belgradeo, Lazio 1-0 Bayer Leverkusen, Sporting CP 2-1 CSKA Moscow, Manchester United 3-1 Club Brugge.

Mechi zilizofuata zikapigwa Jumatano na matokeo yalikuwa: Skernderbeu 1-2 Dinamo Zagreb, Celtic 3-2 Malmo, FC Basel 2-2 Meccabi Telaviv, Rapid Vienna 0-1 Shakhtar Donetsk na Valencia 3-1 AS Monaco.

Mechi hizo za UEFA hatua ya mtoano zinarudia tena wiki hii ambako mechi za Jumatano wiki iliyopita zitachezwa leo Jumanne huku zile za Jumanne wiki iliyopita zikichezwa kesho Jumatano

Katika mechi za kesho ndipo Wayne Rooney wa Manchester United atakapovaa jezi zake na kuingia uwanjani kwenda kucheza kama mshambuliaji yaani namba 9. 

Suala la Rooney kucheza kama mshambuliaji katika timu ya Man U limeliliwa sana na Waingereza na ilifika wakati Jose Mourinho alitaka kumvuta darajani kapteni huyo wa United na timu ya Taifa ya England.

Mourinho alipata nguvu ya kumhitaji Rooney baada ya kelele za Waingereza kwamba Rooney hatendewi haki kwa kuchezeshwa kama mshambuliaji wa pili, kiungo mshambuliaji na wakati mwingine kama kiungo mkabaji.

Waingereza walikwenda mbali zaidi na kumtuhumu Kocha Luis Van Gaal kwamba anampendelea Mholanzi mwenzake, Robin Van Persie, kwa kumpanga kama straika namba moja.

Waingereza wanajua kupamba vya kwao mpaka wanapoteza uhalisia ndiyo maana imeonekana kama ni sahihi Luis Suarez na Raheem Sterling kuwa na thamani moja sokoni.

Ni kweli Wayne Rooney ni mtu muhimu sana uwanjani, na yeye ni kama roho ya timu, amekuwa akikaba, akipandisha timu, kusambaza mipira na kutoa pasi za mabao. 

Waingereza wamesahau kwamba umuhimu wa kitu unategemea na kitu kilipo ndiyo maana umuhimu wa sweta au koti ni mkubwa sana Makete, lakini sweta linapoteza thamani Dar es Salaam.

Heshima na umuhimu wa Rooney unaonekana sana anapokuwa huru uwanjani kupambana kila kona kwa kadri awezavyo.

Rooney ana shauku ya ushindi na kama timu inashambuliwa huwa anarudi nyuma kabisa kwenda kukaba kama kitasa kweli kweli na mara akinasa mpira yeye ndiye hupiga ‘counter attack’ na watu kama Cristiano Ronaldo, Robin Van Persie, Chicharito na wengine wengi walifunga kwa mipira hiyo.

Katika mazingira ambayo mshambuliaji hushindwa kuleta matokeo ndipo Rooney huibuka shujaa kwa kulazimisha kufunga mabao yanayonyanyua mashabiki jukwaani.

Katika mazingira ambayo timu imepoteza matumaini, utamuona Rooney amekaba beki ya kulia kisha amepokea mpira katikati na amepiga mpira kona ya kushoto kwa Ashley Young, kisha utamuona ndani ya boksi akipiga shuti linalokwenda kutua nyavuni na morali ya timu inapanda.

Kitendo cha Van Gaal kutii kiu ya Rooney na Waingereza ni kama kuwasuta Waingereza na kuwaonesha kuwa kocha ndiye anayeijua timu na wachezaji, hivyo aachiwe timu.

Van Gaal amemuuza Robin Van Persie kisha akamuachia Radamel Falcao aondoke zake, ni wazi kwamba aliamua kuitikia kilio cha Waingereza na Rooney mwenyewe.

Alipoulizwa na waandishi mpango wake kwa ajili ya kusajili straika wa kuziba pengo la Van Persie, Van Gaal alijibu, “Wayne Rooney atacheza kama mshambuliaji na hata ninyi waandishi mlitaka sana nimchezeshe kama namba tisa, nimewasikiliza na kuzingatia mapendekezo yenu.”

Kama alifanya kwa kuridhia au kutaka kuwasuta Waingereza kabla hajasajili straika ni suala la kusubiri pia. Pamoja na majibu hayo ya Van Gaal, ni wazi kuwa kumweka Rooney kama mshambuliaji wa mwisho ni sawa na kumuajiri daktari wa moyo kuwa muuguzi.

Katika hali ya kawaida ni kuipoteza thamani na uwezo wa mtu. Waingereza ni lazima wajue ukweli kuwa Rooney anakuwa bora akiwa na majukumu mengi uwanjani, hivyo kumpunguzia majukumu kunamdhoofisha kwa kiwango kikubwa sana. 

Wengi wanaweza kushangaa kwanini nasema haya ilhali mchezaji huyo amecheza mechi tatu tu za kimashindano na kesho ndiyo anakwenda kwenye mechi ya nne? Ninayaeleza haya kwa kuzingatia rekodi zake katika mechi nyingi alizocheza katika nafasi tofauti na ya sasa na alifanya makubwa sana katika idadi ya mechi tatu kama hizi alizocheza. 

Rooney bado anahitajika kucheza nyuma ya mshambuliaji ili kuongeza nguvu ya timu katika kutafuta ushindi. Rooney ana nafasi ya kuthibitisha kwamba alistahili kuwa mshambuliaji na kwamba ilikuwa makosa yeye kuwa nyuma ya mshambuliaji, lakini ni nani atakuwa nyuma yake kufanya yale majukumu aliyoyaacha baada ya kuwa mshambuliaji? 

Man Utd inamuhitaji sana Rooney nje ya ufungaji. Nauona ugumu wa Rooney kukidhi matakwa ya nafsi hiyo kipindi ambacho yeye anahitajika zaidi katika kutengeneza mabao hayo kwa zile varangati zake.

Ili kuthibitisha hilo anatakiwa kufunga mabao yasiyopungua 20 kwa msimu na suala linalosubiriwa ni yeye kuanza kufunga kuanzia mechi ya kesho ya marudiano katika UEFA. 

Ninachoamini kama hatapata bao katika mechi ya kesho dhidi ya Club Brugge ni dhahiri atakuwa ameisuta nafsi yake na Waingereza wenzake ambao watampigia kelele Van Gaal kudai straika mpya na hapo watamaanisha kwamba Rooney anatakiwa asimame nyuma ya mshambuliaji, jambo ambalo ni kula matapishi yao. 

UEFA ni michuano mikubwa zaidi barani Ulaya na kufunga bao katika mechi za UEFA kutathibitisha madai ya Waingereza na au kuwaumbua Waingereza akiwapo kocha wa timu ya Taifa ya England, Roy Hodgson.

 

Baruapepe: amrope@yahoo.com Simu: 0715 36 60 10

1391 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!