DAR ES SALAAM

Na Regina Goyayi

Wimbo ‘Nimpende’ wa msanii Ibra unatajwa kuwa sababu ya kutengana kwa wapenzi wawili, Happy Reuter na Beka Flavour.

Akizungumza na JAMHURI jijini Dar es Salaam, msanii wa filamu na michezo ya kuigiza, Happy, anasema mtunzi wa wimbo huo, Ibra, amemshirikisha kama mpambaji (video vixen) kwenye video yake.

“Ni kazi hiyo ndiyo imeniponza na kuachana na mzazi mwenzangu. Beka alinipigia simu nikiwa kwenye kazi hiyo, akaniambia nisirudi nyumbani.

“Kwamba niliaga nyumbani kwa kusema kuwa ninakwenda kwenye kazi nyingine ya kufanya ‘make up’. Lakini nilivyofika huko haikuwa kama nilivyoeleza, nikawa ‘video vixen’. Hiki kitu kilimkwaza sana Beka,” amesema Happy.

Anasema mara tu alipopokea simu hiyo ya kumzuia kurudi nyumbani, hakuona haja ya kurudi, akidai kuwa anamfahamu vizuri Beka anapokuwa amekasirika.

“Wala sikuona sababu ya kuomba radhi baada ya uamuzi wa mzazi mwenzangu! Beka ni mtu anayefanya uamuzi mgumu na akishaamua, huwa harudi nyuma,” anasema.

Happy na Beka walikuwa wakiishi pamoja ila hawakuwa wanandoa.

Hata hivyo, Happy amesema pamoja na kuwa tayari wametengana na mpenzi wake, hawezi kumsema vibaya hasa linapokuja suala la huduma ya malezi kwa mwanaye.

“Ni mimi ndiye nimekosana na Beka wala si mtoto wetu! Katika suala la kumhudumia mwanaye, Beka yupo vizuri sana kuliko kitu chochote. Kwamba anahudumia mtoto kwa asilimia zote bila hata mvutano wowote kati yetu kama wazazi,” amesema Happy.

Baada ya kutengana na mzazi mwenzie, Happy anasema kwa sasa hayupo kwenye uhusiano na mtu yeyote, na ikitokea kukawa na mipango ya kurejea kwa Beka, basi ni lazima iendane na mipango ya ndoa.

“Ndiyo. Nimeshajifunza. Kwa maana kuishi na mtu bila ndoa ni kitu cha hatari sana,” anasema.

314 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!