Wiki hii nianze kwa kukuomba radhi msomaji wangu kwa kutokuwapo kwenye Safu hii wiki iliyopita. Nilipata dharura, ila namshukuru Mungu kuwa imekwisha salama na maisha yanaendelea. 

Leo nimejaribu kuandika somo pana kidogo linalohusu demokrasia katika nchi yetu. Naandika somo hili, si kwa sababu nyingine yoyote bali kutokana na matukio ya Uchaguzi Mkuu, wa wenyevita wa halmashauri na umeya.

Nimeangalia mchakato wa Uchaguzi Mkuu ulifanyika Oktoba, mwaka jana. Nimeangalia mchakato wa uteuzi ndani ya vyama, kutangaza matokeo na hatimaye washindi. Baada ya kutangaza washindi, nimefuatilia uchaguzi katika halmashauri kama nilivyoeleza hapo juu.

Si hayo tu, nimeuangalia mfumo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Tume ambayo mwenyekiti anateuliwa na kulishwa kiapo na Rais wa nchi, Rais ambaye ni mwenyekiti wa chama tawala, ambaye wakati mwingine anakuwa mgombea urais (katika muhula wa pili) na uchaguzi unasimamiwa na mwenyekiti aliyemteua.

Sitanii, suala si tu mwenyekiti aliyemteua, bali hata wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, ambao nao ni wateule wa Rais, Rais ambaye ni mwenyekiti wa chama tawala, na anayeomba kugombea urais akiwa na mamlaka ya kuwafukuza kazi au kuwafikiria vyema baada ya uchaguzi (akishinda). Hapa, simsemi yeyote, lakini najaribu kuwaza kwa sauti na tushirikiane kuwaza kwa pamoja, kuona demokrasia hii ina sura ipi.

Kuna dhana ya Tume Huru ya Uchaguzi. Wapo wanaojiuliza, iwapo Tume huru inakuwa huru kwa kiwango gani. Hoja zinazojengwa ni kuwa Tume iwe na wawakilishi kutoka vyama vyote vya siasa, kwa kanuni waliyokubaliana. Wapo wanaouliza iwapo Tume huru ya uchaguzi inaweza kusaidia chochote kwa kuangalia Tume Huru ya Uchaguzi ya Zanzibar chini ya Jecha Salim Jecha!

Wanaiangalia ZEC ilivyofanya uamuzi kwa wanachokiita shinikizo la dola. Pia wanaangalia iwapo dola au chama tawala kwa nchi zetu za Afrika zimeishafikia ukomavu wa kuachia madaraka pale wanaposhindwa kihalali. Nimejaribu kuuliza kwa marafiki zangu, kwamba hofu ya kuachia madaraka inatokana na nini, jibu nimelipata.

Jibu nililopewa ni kuwa viongozi wengi hawaongozi nchi kwa mujibu wa sheria. Nchi nyingi za Afrika zinaongozwa kwa matamko, ilani za vyama hazifuatwi, na hapa naweza kutoa mfano wa Rais Jakaya Kikwete kwamba alipoingia madarakani kinyume kabisa na ahadi za CCM akajiingiza kwenye mtego wa kuandika Katiba mpya. Sina sababu ya kurejea hasara tuliyopata kama nchi, na dude hili alivyoliacha njia panda.

Sitanii, serikali nyingi za Afrika ni za visasi. Serikali nyingi ni za kukomoana. Ndiyo maana inafika mahala akiingia madarakani mtu wanayefahamiana, watu hawachelewi kufanya sherehe. Wanaambizana kuwa wameula. Wanafikia mahala pa kutumia hata maneno ya uswahilini kuwa ‘kutesa kwa zamu’. Serikali nyingi za Afrika zimekuwa za kuchuma utajiri.

Haishangazi kuona Rais anayeingia madarakani akiwa hohehahe, lakini baada ya muda mfupi anakuwa na ukwasi wa kutupwa. Serikali nyingi zinageuka ‘kijiwe’ cha baba, mama na watoto (BMW). Kimsingi, kinachosemwa hapa; ni hakuna mifumo. Iwe ni wapinzani au chama tawala, wanawaza kuingia madarakani kunyooshana au kutumbua (si majipu), na si kutumikia wananchi.

Wakati vyama vya ukombozi vilikuwa na dira na dhima ya kumuondoa mkoloni, vyama vya sasa vina miluzi mingi. Wapo viongozi wanaolenga kujipatia utajiri, na wapo wanaodhani wanaweza kuitumikia nchi, huku wengine wakiwa katikati hawajui sera ipi nchi inaitumikia kama ni ujima, ukabaila, ubepari, ujamaa au ubwenyenye.

Sitanii, nimeyasema haya kwa nia ya kujenga hoja. Vyama vilivyo vingi haviheshimu taratibu, kanuni, Katiba, miongozo na sheria za nchi. Tuliyasikia ya CCM kwamba Mwenyekiti Kikwete alifika kikaoni na majina kwenye kikaratasi alichotoa mfukoni na kusoma majina ya anaotaka wasonge mbele katika mchakato. Ukiwauliza wenyewe ndani ya chama, utata huu wanautetea.

Tatizo halipo CCM pekee. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakati kinateua mgombea wake, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema “wameamua kubadili gia angani.” Kwa maana hiyo, utaratibu wa kawaida wa kisheria, kikanuni na kikatiba ndani ya chama haukufuatwa, bali walibadili gia angani. Mfumo wa aina hii ni hatari.

Ukiacha hilo, vituko vinavyotokea baada ya matokeo vinatisha. Uchaguzi wa mameya na wenyeviti wa halmashauri umefumbua wengi macho. Kilichotokea Tanga kimeacha maswali mengi kuliko majibu. Halmashauri za wilaya kama Kyerwa, Kyela na nyingine tumeshuhudia vituko vya ajabu. Madiwani wamekamatwa wamewekwa ndani, baada ya uchaguzi wakaachiwa huru.

Dar es Salaam ndiko kwenye vituko. Kwa mara ya kwanza tumeshuhudia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikifanya juhudi za makusudi kutaka kuazima wabunge wa Viti Maalum kutoka Zanzibar waweze kushiriki uchaguzi wa meya wa Kinondoni na Ilala. Nafahamu chama tawala kinavyojisikia vibaya pale Ikulu inapokuwa chini ya meya anayetokana na Kambi ya Upinzani, lakini huko ndiko kukua kwa demokrasia.

Sitanii, nchi hii ina majiji matano ya Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Mwanza na Tanga. Leo upinzani unaongoza majiji ya Arusha, Mbeya na Dar es Salaam. Matokeo ya Mwanza na Tanga, naamini majibu unayo mazuri zaidi kuliko mimi. Kizungumkuti cha Dar es Salaam katika uchaguzi wa mameya si vyema nikakitaja juu juu bila kukidadavua ipasavyo.

Wilaya ya Kindononi Chadema inao madiwani 29, CCM 15 na CUF tisa. Idadi hii inajumuisha wabunge wa kuchaguliwa na wa Viti Maalum. CCM ilipoamua kuingiza wabunge wa kutoka Zanzibar, idadi yao ikapanda hadi 29, hivyo ikawa ngoma droo. Chadema kuona hivyo, nao wakaingiza madaiwani wao kutoka Zanzibar, wakaongezeka na kufikia 36. Pande zote zilifungua kesi kupinga mchezo huu.

Kwa upande wa Manispaa ya Ilala, nako mambo hayakuwa shwari. Chadema wana madiwani 28, CCM madiwani 31 na CUF madiwani 14. Kwa hesabu hizo chini ya mwavuli wa Ukawa, ukijumlisha madiwani wa Chadema na CUF wanafikia 45. Juhudi za hapa na pale zimefanyika ama kuongeza idadi au kuhakikisha si wote wanaofika kwenye kikao.

Sitanii, pongezi za pekee zimwendee Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene. Ametoa mwongozo sawia kuwa mbunge wa Viti Maalum anapata sifa ya kupiga kura katika jimbo husika iwapo tu mchakato wa kupatikana kwake ulianza na kuhitimishwa katika wilaya anakopenda kuingia kwenye Baraza la Madiwani.

Kwa kauli hii, ni wazi Simbachawene aliwaambia CCM kuwa wabunge wa Viti Maalum kutoka Zanzibar hawana sifa za kushiriki uchaguzi wa meya – Ilala na Kinondoni. Kimsingi, hapo Serikali ya Rais John Pombe Magufuli imejijengea heshima. Mchezo wa kitoto waliokuwa wanataka kuufanya wanasiasa ndani ya CCM haukuwa na manufaa kwa nchi. Ungezusha vurugu zisizo na msingi.

Kilichotokea ni historia. Kwa Ilala madiwani wa CCM walifahamu matokeo kabla ya kura kupigwa. Wakaamua kususia uchaguzi. Nasema hii ni historia, kwani kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii chama tawala kimesusia uchaguzi kwa hofu ya kushindwa. Pamoja na madiwani kuondoka, bado Ukawa wamefanya uchaguzi.

Katika uchaguzi huo, Charless Kuyeko (Ukawa) akapata kura kura 31 na Heri Kessy (CCM) kura 0. Kwa upande wa Kinondoni, Diwani wa Kata ya Ubungo, Boniface Jacob, ndiye aliyechaguliwa kuwa Meya wa Kinondoni kwa kupata kura 38 dhidi ya mpinzani wake, Benjamin Sitta, aliyepata kura 20. Hii nayo ni historia ya pili. Dar es Salaam haijapata kuwa na meya wa upinzani tangu enzi.

Sitanii, najaribu kuangalia misingi ya demokrasia kama tayari tumekomaa au demokrasia yetu ni sawa na urembo wa mkorogo. Kwamba CCM wanatafuta wabunge kutoka Zanzibar kupiga kura Ilala, hii naamini ni moja kati ya bahati mbaya zinazoweza kuwapo hapa duniani.

Katika uchaguzi hakuna sare. Kuna kushinda na kushindwa. CCM inaona taabu kushindwa umeya, ila hawaoni kuwa upinzani chini ya Ukawa umepata uvumilivu wa ajabu chini ya Edward Lowassa. Lowassa amethibitisha kuwa mwanademokrasia wa kweli. Iwapo Lowassa angewaambia wafuasi waliompa kura takribani milioni saba wapinge ushindi wa Dk. Magufuli, nchi hii ingekuwa haikaliki.

Hapa ndipo unapoweza kutofautisha wanasiasa na watafuta fursa. Mfano, Dk. Wilbrod Slaa alipata kura milioni 2 na ushei hivi, ila akahamasisha vijana kuingia mtaani. Najiuliza, iwapo Dk. Slaa ndiye aliyekuwa amepata kura alizopata Lowassa, kama leo angekuwa anazungumza lugha ya kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi na kufikiria mwaka 2020 kama anavyofanya Lowassa sasa, kwa nia ya kumpa fursa Rais aliyeko madarakani kufanya kazi kwa utulivu!

Sitanii, lipo jingine. Leo kazi nzuri anayofanya Rais Magufuli kama Lowassa ndiye angeingia madarakani akafanya kazi sawa na anavyofanya Rais Magufuli, ni wazi yangeanza maneno. Maneno wala yasingekuwa mengine, ingeelezwa kuwa Lowassa analipiza visasi. 

Mada yangu ya leo, nalenga tuwaze pamoja wewe msomaji. Najiuliza iwapo kweli nchi yetu tumepiga hatua katika demokrasia au kwa matukio ya Ilala na Kinondoni tunapaswa kujiuliza kama tunafanya siasa au ‘si hasa.’

Kubwa katika yote, tunapaswa kufahamu kuwa kuna umuhimu wa upinzani kuwapo. Nchi yetu kupiga hatua kimaendeleo inahitaji kuwa na upinzani sawa na ilivyo Marekani au Uingereza. Inahitaji kuwa na idadi ya wabunge nusu kwa nusu, baada ya hapo usijali Rais atatokea chama kipi. Hawa watasukuma maendeleo halisi ya Taifa. Kwa nia ya kufikia lengo hilo, kazi iliyopo mbele ya Watanzania ni kudai TUME HURU YA UCHAGUZI. Mungu ibariki Tanzania.

1711 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!