Mji wa Morogoro ni miongoni mwa miji iliyokuwa maarufu kwa michezo na burudani katika miaka ya 1950, 1960 na ya 1970.

Watu wengi walitoka jijini Dar es Salaam na kufanya starehe za kumaliza wiki mjini humo. Hali ya hewa na kuwapo kwa bendi mbili maarufu zilizokuwa na uwezo mkubwa, zilifanya wafanyakazi wengi watamani kupangwa kufanya kazi mjini Morogoro.

Bendi hizo mbili zilizokuwa shindani zilikuwa ni Morogoro Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Mbaraka Mwinshehe Mwaruka na Cuban Marimba iliyokuwa ikiongozwa na Salum Abdallah Yazidu aka SAY.

Katika makala hii nitamzungumzia kiongozi huyo wa Bendi ya Cuban Marimba — Salum Abdallah Yazidu — aliyezaliwa Mei 5, 1928 mkoani humo.

Baba yake alikuwa na asili ya Kiarabu na mama yake alikuwa ni mwenyeji wa Mkoa wa Morogoro. Alisoma mpaka darasa la sita pale Msamvu na akachaguliwa kuendelea na shule huko Dar es Salaam. Kwa wakati ule alilazimika kwenda Dar es Salaam ili kuendelea na masomo. Lakini  baba yake aliamua abaki nyumbani ili amsaidie katika shughuli za biashara.

Katika kipindi hicho Salum alianza kuonesha kupenda kwake muziki. Alifurahia sana santuri kutoka Cuba zilizokuwa maarufu kwa kuitwa kwa namba zake GV 1, GV 2, GV 3 zilizokuwa zikipigwa kwa kutumia magitaa  aina ya galaton na kadhalika.

Pamoja na baba yake kutokupenda aina ya muziki aliokuwa anapiga mwanaye, aliona ni heri amnunulie gramafoni ya kupigia hizo santuri. Haukupita muda Salum alitoroka kwao ili kwenda nchini Cuba kujifunza muziki.

Mwaka 1945 alikwenda hadi Mombasa, Kenya ili apande meli kwenda Cuba. Wakati huo kulikuwa bado na vuguvugu la Vita ya Pili ya Dunia hivyo safari yake ikaishia Mombasa, nchini Kenya.

Baba yake alimrudisha Morogoro, akamfungulia mgahawa ili atulie, lakini alikuwa keshapata ‘mzuka’ wa muziki na akawa ameanza kuhudhuria kumbi nyingi zilizokuwa zikipiga muziki wa dansi.

Alipendezwa sana na vifaa vya Dar es Salaam Jazz Band ‘Majini wa Bahari’ waliokuwa na maskani yao mtaa wa Mchikichi, na kutumbuiza kila mwisho wa wiki na siku maalum katika ukumbi maarufu jiji la Bandari Salam — Tanzania Legion and Club — lililokuwa kona ya Mtaa wa Mazengo na Barabara ya Morogoro.

Wakati huo yeye na wenzake walikuwa wameanzisha kikundi ambacho kilikuwa na vyombo vya kuchonga na ngoma za kiasili —  wenyewe wakikiita bendi na kukipa jina La Paloma. Hili lilikuwa jina la wimbo mmoja katika santuri za GV, wimbo huu ni mzuri kiasi kwamba mpaka leo bado unapigwa duniani kote hadi kurekodiwa na wanamuziki mbalimbali akiwamo Elvis Presley aliyeingia katika anga za muziki baadaye sana.

La Paloma ilikuwa na viongozi kama Juma Saidi aliyekuwa rais, Abubakar Hussein akawa mweka hazina, Ramadhan Salum alipewa nafasi ya Katibu Mkuu, Ali Waziri, Naibu Katibu Mkuu, Salum Abdallah akawa mkuu wa bendi.

Baada ya kuviona vyombo vya muziki vya Dar Jazz, hamu ya kuwa na vyombo kama hivyo ilikuwa kubwa hadi kufikia Salum Abdallah kuuza kwa siri nyumba mojawapo ya baba yake na kununua vyombo kama vya Dar es Salaam Jazz band.

Mwaka 1948 La Paloma ikawa bendi rasmi. Viongozi wake walikuwa Salum Abdallah aliyeteuliwa kuwa kiongozi, Abubakar Hussein akawa mweka hazina na Juma Ndehele akapata nafasi ya Katibu. Wanamuziki walikuwa Kibwana Seif, Juma Kilaza, Ligongo, Mgembe, Juma Kondo, Nzige, Daulinge.

Mwaka 1952 kundi hili likajipa jina la Cuban Marimba Jazz Band ambalo lilianza kuwa maarufu kiasi kwamba mwaka huo huo kampuni ya santuri ya Mzuri Records walikwenda Morogoro kurekodi nyimbo za bendi hiyo.

Bendi ya Cuban Marimba ikiwa na nguli huyo, iliwahi kurekodi vibao vingi vikiwamo vya Ngoma iko huku, Naumiya, Ubaya, Nalia Nalia, Wanipendeza, Cuba Chacha na Ndiyo hali ya Dunia. Nyingine ni Kazi Tanzania, Shemeji, Tanzania Twist, Sipati majibu, Salaam kwa jumla na Wanawake Tanzania.

Salum Abdallah hakuishia hapo bali alitoka na vibao vingine vya Kachacha, Tulime Mashamba, Mabeberu, Kimanzi, Si kosa lako Unavunja Utu, Mpenzi Wee na Maisha matamu. Bendi iliendelea kuwa na umaarufu mkubwa mpaka kwenye miaka ya 1970.

Ama kweli ‘kizuri hakidumu’. Usemi huu ulijidhihirisha pale Salum Abdallah alipopata ajali mbaya iliyokatisha maisha yake. Chanzo cha ajali kilielezwa kuwa taa za gari lake zilizimika ghafla akiwa katika mwendo.

Gari hilo lilitoka nje ya barabara na kumtupa nje, akapasuka kibofu na kufariki siku hiyo hiyo Novemba 19, 1965. Juma Kilaza, aliyekuwa msaidizi wake,  aliendelea kupiga muziki katika bendi hiyo akishindana kwa kiasi kikubwa na hasimu wake Mbaraka Mwinshehe.

Mungu azilaze roho zao Pahala Pema Peponi, Amina.

 

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba 0784331200, 0767331200 na 0713331200

By Jamhuri