Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Rais Samia Suluhu Hassan, amesema Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 imeshiba, ni ya ushindi, imepangiliwa bila kuacha kitu na yaliyopo ndani yanatekelezeka kuendana na mpango na uwezo uliopo.
Rais Samia alieleza hayo Dodoma alipohitimisha Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM Taifa na kueleza kwamba CCM inajiamini kwamba itatekeleza yaliyopo katika ilani hiyo kama walivyofanya katika kipindi cha utekelezaji kilichoisha.

Alisema jambo la msingi ni kuweka utulivu ndani ya nchi na kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha fedha zinapatikana kwa wingi ili kuwezesha utekelezaji huo.
“Ilani imeshiba, haijaacha kitu, kuna mengi lakini imepangwa vizuri, yaliyopo kwenye ilani hii tunaweza kuyatekeleza kuendana na mpango na uwezo tulionao tunajiamini tunaweza kutekeleza, tumeweza kipindi hiki tutaweza kipindi kijacho,” alisema Rais Samia.
Alieleza kuwa ilani hiyo iliyozinduliwa inasisitiza umuhimu wa kushirikiana na sekta binafsi ndani na nje ya nchi kutekeleza mambo makubwa yanayotarajiwa kufanyika.
Pia, alisema wajibu wa wanachama wa CCM ni kila mmoja kuibeba ilani hiyo na kuitangaza ili watu wawaunge mkono kuitekeleza, kwani ilani hiyo ni mali ya CCM kwa maana ya wanachama wote na si ya sekretarieti, kamati kuu wala halmashauri kuu ya chama pekee.
“Kikubwa kwa Watanzania ni kuweka utulivu ndani ya nchi yetu, kufanya kazi kwa bidii, wafanyabiashara wafanye biashara kwa bidii, wakulima walime kwa bidii, wachimbaji wachimbe kwa bidii, wafanyakazi wa umma wafanye kazi kwa bidii ili tupate fedha kwa wingi, yote haya yanaweza kutekelezeka,” alifafanua.

Aliongeza kuwa kwa urahisi wa utekelezaji wa ilani, amemuagiza Katibu Mkuu na Mwenyekiti wa utekelezaji wa Ilani, kutengeneza vitabu vidogovidogo vya ilani ya mikoa ili kila mkoa uwe na ilani yake.
“Kila mkoa uwe na ilani yake, iseme katika ilani inayoisha muda tulipanga nini katika huo mkoa, tumetekeleza nini na kiko wapi na kwenye ilani mpya huo mkoa tumeufikiria nini.
Vitabu hivyo vikimaliza kutengenezwa vitapelekwa kwa kila mkoa kujua wajibu wenu ni upi katika utekelezaji wa ilani hiyo,” alifafanua Rais Samia.