Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mwanza 

Mgombea kiti cha Urais kupitia chama cha Sauti ya Umma(SAU),Majalio Kyara,amesema endapo  chama hicho kitashika dola katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29,mwaka huu,jambo la kwanza atahakikisha  kila mtanzania anafikiwa na  maji na huduma hiyo anaipata bure.

Kyara, amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Igoma jimboni Nyamagana,katika mkutano wake wa kampeni mkoani Mwanza.

Ambapo amesema hakuna kiwanda ambacho kinatengeneza maji hayo bali tumepewa na Mungu,hivyo wakipata madaraka watafanya utafiti na kubaini kila kaya inauwezo wa kutumia kwa mwezi uniti ngapi,kama ni uniti 30,ikitokea amefanya uzembe ametumia zaidi yale yaliozidi atayalipia.

Pia amesema ili taasisi za maji ziweze kujiendesha,wale watoa huduma ambao wanafanya biashara na wanatumia maji kama hoteli na migahawa,watalipia ankra(bili) za maji.

Aidha,amesema,watahakikisha wanadhibiti upotevu wa maji ambapo kwa sasa zaidi ya asilimia 50  ya maji yanayozalishwa yanapotea kabla  kufika kwa watumiaji.

“Kwaio tukidhibiti upotevu wa maji, tunauhakika wa kutoa huduma hiyo bure kwa watanzania wenzetu wote, uwezo huo  tunao na nia hiyo Sauti ya Umma tunayo,” amesema Kyara na kuongeza:

“Tunalo jukumu la kuwaandalia watoto wetu,wajukuu zetu kesho ilio bora zaidi,hakuna mwingine zaidi yetu na tusipofanya hivyo watoto wetu watakuja kutulaumu,lazima muelewe na mtambue umuhimu wa kufanya maamuzi sahihi Oktoba 29,2025, mkikosea hapo tuna kwenda kuendelea kuyumba kwani kila kukicha ni shida huduma ya maji safi na salama changamoto,”.

“Hatukupaswa mpaka leo Watanzania,wanamwanza  kama Igoma tuwe tunazungumzia suala la hupatikanaji wa maji safi na salama.Dunia kwa sasa inakuwa kwa kasi sana,hupatikanaji wa maji safi na salama ni kati ya mambo ambayo wenzetu wengi wameisha yasahau kabisa,ni lazima tuchukue hatua tutafute uongozi sahihi ili tuhakikishe huduma za msingi zinawafikia kila mtanzania,haiwezekani  Ziwa Victoria lipo hapa alafu  Igoma wana shida ya maji,”.

Pia Kyara amesema,kupitia ilani yao wanataka kuweka usafiri wa umma jijini Mwanza.

“Tutaweka mtandao wa treni za umma, tunataka tutengeneze usafiri wa umma katika Jiji la Mwanza, ili watanzania na wanamwanza watumie usafiri huo,hivyo kuokoa muda,gharama,kupunguza msongamano na kuwa na uwezo wa kufanya shughuli nyingi za uchumi  wa taifa,kwani kesho ilio bora inajengwa na sisi,”.

Hata hivyo amesema,endapo watashinda na kuongoza nchi, Serikali chini ya chama hicho kitakaweka mfumo ambao utatambua vipaji mbalimbali vya vijana na kisha kuvikuza na kuvilea kwa sababu wanajua wanatengeneza ajira,vipato binafsi na mapato ya taifa.

Sanjari na hayo amesema,kila mmoja ana thamani kwa mwingine,hivyo wanataka kutengeneza Serikali shirikishi ya watanzania wote na kila mmoja atakula matunda ya nchi.

Huku akisisitiza kurejesha heshima ya walimu na lazima kama Serikali watatengeneza mazingira shawishi yatakayo mvutia Mwalimu kutamani  kwenda kufundisha kijiji fulani,ambapo watahakikisha k vifaa vya ufundishaji na vitendea kazi  vinapatikana ili kazi ya ualimu ifanyike kwa ufanisi.