Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, uzalishaji wa taka ngumu nchini ni takriban tani milioni 14.4 hadi 20.7 kwa mwaka ikiwa ni sawa na kilogramu 0.66 hadi 0.95 za uzalishaji kwa kila mtu kwa siku.

Aidha, ni takribani asilimia 33 tu ya taka ngumu zinazozalishwa hukusanywa nchini kote. Vilevile, inakadiriwa kuwa asilimia 70 ya taka ngumu zinazozalishwa nchini ni taka zinarejelezeka ambapo kati ya hizo ni asilimia tano hadi kumi pekee zinazorejelezwa na sekta isiyo rasmi.


Kama ilivyo kwa nchi nyingine, Tanzania inakabiliwa na changamoto yausimamizi wa taka kutokana na shughuli zisizozingatia utunzaji wa mazingira, ukuaji wa miji na ongezeko la watu.

Maeneo ya miji yanakadiriwa kuwa na uzalishaji mkubwa wa taka ambapo kiasi kinachokusanywa na kupelekwa dampo ni kidogo na hivyo sehemu kubwa ya taka hizo huchomwa na kutupwa katika maeneo ya wazi hivyo kuathiri mazingira na afya ya jamii.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazungira) Mhe. Dkt. Festo Dugange (wa pili kulia) akipata maelezo kuhusu shughuli za uchakataji wa takaoza na kuzalisha mbolea katika mradi wa kiwanda cha Mabwepande wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam.

Kwa hali hiyo usimamizi wa taka ni mojawapo ya changamoto inayohitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa wakiwamo wazalishaji wa taka, wataalamu wa mazingira, watunga sera na jamii.

Hivyo, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuchukua hatua ili kuimarisha udhibiti wa taka nchini ikiwemo kuhamasisha urejelezaji wa taka, kuandaa na kutekeleza Mwongozo wa Usimamizi wa Taka Ngumu kwa kutumia mbinu ya (Punguza, Tumia Tena na Rejeleza) wa Mwaka 2021.

Pamoja na Mwongozo huo, pia umezinduliwa Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Taka wa miaka mitano (2025 – 2030) wenye lengo la kuimarisha mfumo wa usimamizi wa taka ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira na kulinda afya ya jamii.

Ziara kiwanda cha mbolea Mabwepande

Hivi karibuni, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange alifanya ziara katika mikoa ya Dar es Salaam na Kagera, yenye lengo la kuhamasisha shughuli mbalimbali za hifadhi na usimamizi wa mazingira na kusisitiza uimarishaji wa mifumo ya uchambuzi wa taka ngumu.

Katika ziara hiyo alitembelea kiwanda cha kuchakata taka oza na kuwa mbolea kilichopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni

kilichojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 6 ikiwa ni ufadhili wa Serikali ya Ujerumani na Tanzania kupitia ushirikiano baina ya Jiji la Dar es Salaam na Jiji la Hamburg.

Dkt. Dugange wakati wa ziara hiyo anawahimiza wananchi kuyatumia madampo ya kukusanyia taka ili zitumike kama malighafi katika viwanda vya uchakataji hasa mbolea hatua inayosaidia katika kusafisha mazingira.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Dugange anautaka uongozi wa Wilaya ya Kinondoni kuhamasisha wananchi kutumia kiwanda hicho kwa kukusanya takaoza na kuzipeleka ili zichakatwe kuwa mbolea.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazungira) Mhe. Dkt. Festo Dugange (wa pili kulia) akitembelea na kukagua dampo la Pugu Kinyamwezi wilayani Ilala, Dar es Salaam.
 

Halikadhalika, kutokana na kuwa asilimia 60 ya taka zinazozalishwa na kutupwa katika madampo ni zile zinazooza, anawahimiza wananchi kutumia fursa hiyo kuzikusanya kwa ajili ya viwanda vya mbolea ya asili.

Pia, Naibu Waziri Dkt. Dugange anatoa rai kwa wadau kuwekeza na kuanzisha viwanda vya kuchakata taka za aina mbali ili kupunguza taka kwenda dampo sanjari na utoaji wa elimu ya kuzitenganisha.

Ziara Dampo la Pugu Kinyamwezi

Utenganishaji wa taka ngumu nchini unatekelezwa zaidi na sekta zisizo rasmi zinazojumuisha wakusanyaji wa taka na warejelezaji wadogo wa taka, unaofanywa zaidi katika kaya na maeneo ya biashara kwa lengo la kupata taka zinazoweza kutumika tena au kurejelezwa, ambazo ni pamoja na karatasi, plastiki, vioo na chuma chakavu.

Aidha, kiasi cha taka kinachoweza kurejelezwa hakiwezi kukadiriwa kwa urahisi kwa kuwa ukadiriaji wa kiasi cha taka zinazoweza kurejelezwa unategemea aina na ubora wa taka na masoko yaliyopo kwa wakati huo.

Vilevile, idadi ya wakusanya taka inatofautiana katika maeneo mbalimbali kulingana na upatikanaji wa taka na idadi ya viwanda vya urejelezaji wa taka vilivyopo katika eneo linalohusika.

Akitembelea dampo la Pugu Kinyamwezi lililopo katika Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, Naibu Waziri Dkt. Dugange anasisitiza usimamizi sahihi wa taka, hatua itakayosaidia kuepuka kulundikana na kusambaa ovyo.

Sanjari na hilo, anahimiza jamii kushiriki kikamilifu katika utenganishaji wa taka kuanzia ngazi ya kaya na kwa halmashauri kuongeza uratibu wa usimamizi wa taka katika Serikali za Mitaa.

Changamoto kubwa ni kukithiri kwa taka za mifuko ya plastiki hali inayodhirisha wazi kuwa pamoja na katazo la Serikali la uzalishaji, usambazaji na matumizi ya chupa hizo, bado zinaoNekana katika madampo.

Hivyo, Dkt. Dugange analielekeza Baraza la Taifa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kutumia sheria kudhibiti taka za plastiki ikiwemo mifuko iliyopigwa marufuku na Serikali.

Anabainisha kuwa taka za plastiki katika madampo zimekuwa nyingi, hali inayoonesha pamoja na kupigwa marufuku uzalishaji, usambazaji na uuzaji wa mfuko hiyo bado inaonekana kutumika.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazungira) Mhe. Dkt. Festo Dugange akikagua shughuli za uzalishaji wa vifungashio alipotembelea kiwanda cha L & N Standard PackagingSolutions Ltd kilichopo wilayani Missenyi mkoani Kagera.

Ziara Mkoa wa Kagera

Katika kuhakikisha wakusanya taka wanatambuliwa na kurasimishwa, tayari wakusanya taka zaidi 2,000 wamesajiliwa katika miji mikubwa na pia utenganishaji wa taka usioridhisha unasababishwa na uelewa mdogo miongoni mwa jamii, ukosefu wa motisha na kutokuwapo kwa vituo vya utenganishaji wa taka.

Akiwa mkoani Kagera, Naibu Waziri Dkt. Dugange alitembelea mradi wa vijana wanaojihusisha na uchakataji taka ngumu na uhifadhi wa mazingira wilayani Karagwe na kiwanda cha Plastic Waste Enterprise kinachojihusisha na urejelezaji wa taka za plastiki katika Manispaa ya Bukoba.

Anawahakikishia vijana na wawekezaji kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono katika shughuli zao ambazo si tu zinasaidia kusafisha miji kutokana na ukusanyaji wa taka, bali pia zinatoa fursa ya ajira.

Halikdhalika, anatumia nafasi hiyo kuwaeleza namna taka zinavyoweza kuwa ni mali hivyo anawataka wananchi kuchangamkia fursa ya taka kwa kuzikusanya na kuziuza kwa viwanda vinavyozalisha bidhaa. 

Katika hatua nyingine akiwa wilayani Karagwe alizindua gari maalumu la kukusanya na kusafirisha taka, mradi unaotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kwa kushirikiana na Manispaa ya Fourth nchini Ujerumani.

Anaipongeza halmashauri hiyo kwa kuwa mfano wa kuigwa kwa utunzaji wa mazingira huku akieleza mpango wa Serikali kuhakikisha inajenga mitambo ya kuchakata taka hizi na kuzalisha mbolea asili.

Uwekezaji mifuko mbadala

Ili kuhamasisha matumizi ya mifuko mbadala wa plastiki, Serikali inaendelea kuwaunga mkono na kuwatia moyo wawekezaji wa viwanda vya kuzalisha mifuko mbadala na vifungashio vyenye viwango, hatua inayosaidia jamii kuachana na mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku.

Akiwa wilayani Misenyi mkoani Kagera, Naibu Waziri Dkt. Dugange alitembelea kiwanda cha L & N Standard PackagingSolutions Ltd ambapo alikagua shughuli za uzalishaji wa vifungashio.

Akizungumza mara baada ya kujionea shughuli za uzalishaji anaonesha kuridhishwa na kueleza kuwa wawekezaji wa viwanda vya mifuko mbadala wana nafasi katika utunzaji wa mazingira kwani wanazalisha mifuko ambayo inaoza na haichafui mazingira hivyo waungwe mkono.

Dkt. Dugange ansema kuwa Serikali ilipiga marufuku uzalishaji wa mifuko ya plastiki na vifungashio vya plastiki visivyo na viwango ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira na kulinda afya za wananchi endapo itachomwa au chembechembe zake zitaingia kwenye vyanzo vya maji.

Anafafanua kuwa mifuko ya plastiki inapotupwa na kuzagaa ovyo mitaani huweza kusabaisha maradhi yakiwemo saratani na vifo kwa mifugo endapo wataimeza hivyo viwanda kama hivi Serikali inaviunga mkono.

Aidha, anabainisha kuwa mifuko mbadala ina soko kubwa na kwamba Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na wizara zenye dhamana ya Uwekezaji na Viwanda itahakikisha wawekezaji hawa wanapata ushirikiano ili uzalishaji uwe endelevu.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazungira) Mhe. Dkt. Festo Dugange akitoa maelekezo alipotembelea mradi wa kiwanda cha Mabwepande wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam.