Na Mwandishi Wetu, Jamhuri Media-Korogwe
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameielekeza Wizara ya Kilimo na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufanya kazi ya kupitia mikataba ya mashamba yote ya mkonge ambayo hayaendelezwi ili yarudishwe serikalini.
Rais Samia ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Korongwe na Mombo kwa nyakati tofauti wakati wa mikutano yake ya kampeni zake za uchaguzi mkuu leo Septemba 30,2025.

“Nimeagiza ofisi hizi mbili ziangalie vizuri mikataba ya wahusika kama tunaweza kuivunja mashamba na Viwanda virudi chini ya usimamizi wa Serikali,”amesema.
“Katika miaka mitano ijayo tutahakikisha viwanda vilivyobinafsishwa lakini havifanyi kazi vinapatiwa wawekezaji wengine na kukabidhiwa kwa ushirika chini ya usimamizi wa serikali.
“Niwaambie hapa Korogwe pia kuna mashamba yapo, hayaendelezwi, nimeelekeza pia Wizara ya Kilimo na Mwanasheria mkuu wa serikali wayafanyie kazi, waangalie mikataba yetu na wawekezaji, vipi tunaweza kuvunja mikataba ili mashamba yale yarudi serikalini tufanye maamuzi mengine.
“Kuhusu kiwanda cha Chai, tunakuja pia kufunga mitambo mipya mingine ili kuchakata zao la chai, hiki kiwanda kitaendeshwa na ushirika kikisimamiwa na bodi ya chai.

“Kuna mashamba ya mkonge mbayo hakuonekani kama mambo mazuri na uchakataji wa mkonge umepungua, tulichokifanya ni kuitaka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Wizara ya kilimo wafanye tathmini ya mashamba na kiwanda.
Lengo letu ni kuongeza uwezo wa kuchakata na kile kiwanda cha Tangold na chenyewe kitatupiwa macho vizuri kwa kuangalia muwekezaji mwingine au serikali ikichukue kiwanda kile kifunguliwe,”amesema.
Amesema kitaendeshwa chini ya ushirika ambayo katika miaka ya karibuni imeonekana kuimarika zaidi.



