Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametangaza serikali mpya ya mseto, baada ya chama chake tawala cha African National Congress (ANC) kupoteza wingi wa wabunge katika uchaguzi wa mwezi Mei.

Alisema “serikali ya umoja wa kitaifa… haijawahi kutokea katika historia ya demokrasia yetu”.

Chama cha ANC kitakuwa na nyadhifa 20 kati ya 32 za baraza la mawaziri, huku chama cha Democratic Alliance (DA) – hadi sasa chama kikuu cha upinzani – kitashikilia nyadhifa sita. Nyingine sita zitagawanywa kati ya vyama vidogo.

Kupungua kwa uungwaji mkono wa chama cha ANC katika uchaguzi kulionyesha kufadhaika kwa umma juu ya rekodi yake mbaya ya kutoa huduma za kimsingi na kukabiliana na ukosefu wa ajira, umaskini na ufisadi.

ANC chini ya Nelson Mandela ilifanikisha lengo lake la kukomesha utawala wa wazungu walio wachache nchini Afrika Kusini mwaka 1994, na imekuwa ikitawala nchi hiyo peke yake.

Katika baraza jipya la mawaziri, ANC itashikilia wizara muhimu kama vile ulinzi, fedha na mambo ya nje.

Huku chama cha DA kikishikilia nyadhifa kama wizara ya mambo ya ndani na ujenzi. Kiongozi wa chama hicho John Steenhuisen ataongoza wizara ya kilimo.

Katika hotuba yake kwa njia ya televisheni siku ya Jumapili, Bw Ramaphosa alisema: “Serikali inayokuja itaweka kipaumbele ukuaji wa uchumi wa haraka na endelevu, na upatikanaji wa jamii yenye kuzingatia haki zaidi.”

ANC ilikaribisha hatua hiyo kama “hatua muhimu kusonga mbele, na ushahidi wa uthabiti wa demokrasia yetu”.

Wakati huo huo, DA ilisema “ni fahari kukabiliana na changamoto hiyo na kuchukua nafasi yetu, kwa mara ya kwanza, kuingia katika serikali ya kitaifa”.

Pia iliahidi “utawala bora, kutovumilia kabisa rushwa na utungaji sera kwa vitendo”.

Hata hivyo, licha ya makubaliano ya muungano wa baraza la mawaziri, malumbano makali ya kisiasa yameendelea kushuhudiwa kati ya vyama vya ANC na DA.