*Wadau wakiri si sahihi polisi kuzua watu kwenda mahakamani
*Wadai ni kinyume na Ibara ya 18 ya Katiba na sheria nyingine kadhaa
*Watoa wito Mahakama kulizuia Jeshi la Polisi kukukuza watu Kisutu
*Wengi wanaamini bado fursa ya mazungumzo ipo
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Kitendo cha Jeshi la Polisi kuwazuia mashabiki na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kufika mahakamani kusikiliza kesi ya Tundu Lissu, kunatajwa sawa na kuitumbukiza serikali kwenye mtego wa Chadema.
Lissu, Mwenyekiti wa Chadema Taifa anayeshikiliwa katika Gereza la Mahabusu la Keko, ameshitakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa makossa ya uhaini na alitakiwa kufikishwa kartini Alhamisi iliyopita.
Hata hivyo, siku hiyo Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam liliendesha kamatakamata ya viongozi na watu wengine wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chadema waliokuwa maeneo ya Mahakama ya Kisutu na hata wengine mbali na mahakama, huku likizuia watu kuingia mahakamani kusikiliza kesi ya Lissu.

Wakizungumza na JAMHURI, wanaharakati na wanasheria kadhaa wamesema kwa kitendo hicho, dola imeingia kwenye mtego wa Chadema hivyo kutia dosari mwenendo mzima wa siasa za Tanzania.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Richard Mbunda, amesema Serikali ilitakiwa kutumia busara badala ya nguvu kwa sababu ni haki ya wananchi kufuatilia kesi mahakamani.
Adhabu kwa mtu aliyekutwa na hatia ya kosa la uhaini ni hukumu ya kunyongwa hadi kufa.
Dk. Mbunda amesema wananchi wana sababu ya kufuatilia wajue sababu za kiongozi wao kuwekwa mahabusu
“Wangetumia njia ya kuchagua, kwa mfano wangewaruhusu wanachama 50 tu, wengine wangeelekezwa na wangeelewa.
“Kutokuwepo uwazi katika kesi hii kama ilivyotokea, ndiko kunakoleta tafsiri tofauti kabisa mioyoni mwa watu, kuwa wananyimwa haki,” amesema.
Mbunda amesema kukamtwa kwa Lissu na matukio ya kupigwa baadhi ya wafuasi haikuwa sahihi.
“Ikiwa kiongozi mkubwa anashutumiwa kwa kesi kama hii, inaonyesha kesi hiyo ina umuhimu mkubwa wenye maslahi ya umma.
“Watu wanataka kujua hoja zitakazowasilishwa hadi kuishawishi Mahakama kuzikubali tuhuma nzito kisi hicho. Mimi ningependa kuona mahakama ikifanya kikao cha wazi kabisa ili wale wanaopenda kusikiliza waweze kushiriki.
“Hii itawapa nafasi watu kujiridhisha kwamba mtu huyo anastahili kuhukumiwa kwa haki, kwa sasa anashutumiwa tu,” amesema.
Anawashangaa polisi kutumia nguvu kubwa kuwanyanyasa wananchi akisema hilo linaonyesha kutokuwepo uwazi katika kesi husika hivyo watu kufikiria kwamba huenda Lissu amebambikiziwa kesi kutokana na harakati zake.
Kama kudhihirisha kuwa serikali imeingia mtegoni, Dk. Mbunda anasema kwa sasa vyombo vya habari vya kimataifa vinayazungumzia kwa kina mambo hasi yanayoendelea kwenye siasa za Tanzania.
“Mamlaka ilipaswa kuangalia jambo hili kwa makini kabla ya kuchukua hatua, linaweza kuathari taswira ta taifa,” amesema akiamini kuwa hali hiyo bado inaweza kurekebishwa.
Mwanasheria kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Deogratias Bwire, amesema hatua ya polisi kuzuia wananchi kwenda Mahakama ya Kisutu haikuwa sahihi.
Anatoa sababu kwamba mahakama ni eneo la umma ambapo kila mtu anakaribishwa kuangalia na kufuatilia kesi zinazomuhusu na zenye maslahi kwake binafsi au kwa umma.
“LHRC tumeshazungumza na kuweka wazi kuwa kilichofanyika hakikuwa sahihi. Kesi hii ina ‘presha’ ya kisiasa na inahusisha maslahi ya umma. Ni kesi inayogusa mioyo ya wengi kwa kuwa anayekabiliana nayo ni kiongozi wa chama kikubwa nchini,” anasema Bwire.
Kwa ujumla, mwaka huu ambao ni wa uuchaguzi, Watanzania wapo katika hali fulani (presha ya kisiasa) tofauti ni miaka mingine, na Bwire anashauri vyombo vya dola kutumia busara zaidi kipindi hiki.
“Majukumu ya polisi yalikuwa ni kuzuia machafuko, lakini bado walipaswa kutumia busara zaidi badala ya nguvu. Ni wazi nguvu imetumika zaidi ya inavyotarajiwa. Hili linahitaji majadiliano ingawa si rahisi Jeshi la Polisi kujihusisha katika suala hili la kisiasa.
“Nafikiri bado kuna uwezekano wa kuanzisha mdahalo kuwapa nafasi polisi kueleza na kuelezwa nini majukumu yao. Kama hali itaendelea hivi, itakuwa changamoto. Ni muhimu kuzingatia njia bora ya kushughulikia hali hii na kuikomesha kwa busara kuliko kutumia nguvu,” amesema.
Anasema kama matukio hayo yanatokea bila mamlaka kuchukua hatua kunaweza kusababisha watu kuwa na hisia za chuki na kuleta madhara zaidi.
Hata hivyo, bado jeshi la polisi halijazungumzia ni nini hasa kilichotokea siku hiyo huku kukiwa na madai ya mtu mmoja kuuawa.
Mwaka jana, Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kilimwalika Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Mulilo, kuzungumzia (au kufafanua) madai ya watu kupotea.
Kutokana na hoja hiyo, Bwire anaamini Muliro au maofisa wengine wa juu wanaweza kushiriki kwenye mijadala mizito kwa maslahi ya umma.
Wakati wa Sikukuu ya Pasaka viongozi wengi wa Kikristo walitumia mahubiri yao kutahadharisha kuwapo kwa tishio la mwelekeo mbaya wa kisiasa nchini.
Nao walitoa wito wa kutafuta namna ya kumaliza hali hiyo kwa mazungumzo badala ya nguvu.
Akizungumzia mahubiri hayo, Wakili wa Kujitegemea na mkazi wa Morogoro, Evaristi Mnyele, anasema viongozi wa dini walijikita katika kauli moja tu; haki ni tunda la amani.
“Tujiulize. Viongozi hao wa dini wanamaanisha nini? Wana maana kuwa Tanzania hakuna haki? La hasha!
“Wao wanapigia kelele ile haki ambayo ikipuuzwa inaweza kuwa na madhara ya moja kwa moja ya uvunjifu wa amani, na hiyo ni haki ya kufanya siasa ili kushika dola,” anasema Mnyele.
Anasema ni eneo hilo ndilo huzua migogoro ya mara kwa mara nchini hasa nyakati za uchaguzi kama kipindi tulichomo sasa.
Anaashauri Tanzania kama taifa kufanya mabadiliko ya dhati kumaliza aina hiyo hata kama ikibidi kubadili sheria kwa kuwa: “Migogoro ya aina hii inalipaka tope taifa letu na kuonekana halitendi haki wakati kimsingi haki nyingi za binadamu zinatekelezwa nchini Tanzania.”
Kauli hizo za wadau, wanaharakati na wanasheria zinaungwa mkono na Aloyce Komba, Wakili kutoka Haki Kwanza Advocates ya jijinii Dar es Salaam, akisema:
“Kipimo cha 4Rs za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ikiwemo uwazi, uvumilivu, na utawala wa bora wa Serikali yake inayomshtaki Lissu ni pamoja na kuifanya kesi husika isikilizwe katika Mahakama huru ikiwemo kuruhusu wasikilizaji, hasa wafuasi wa Chadema.
“Mahakama isinyamaze katika hili. Itoe tamko kwamba ni haki ya kila mtu mwenye nafasi kwenda mahakamani kusikiliza mwenendo wa kesi yoyote ikiwemo hii ya Lissu yenye masilahi au mvuto mkubwa wa kisiasa kwa jamii.
“Waandishi wa habari wote (wa umma na wa binafsi) waruhusiwe ili kuepusha upotoshaji wa taarifa za kesi hiyo. Lengo liwe ni ‘Umma wa Tanzania’ kupewa taarifa sahihi kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya Mwaka 2016 na Sheria nyingine za Haki Jinai.”
