Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Serikali imesema kuwa uanzishwaji wa Chuo cha Ufundi Dodoma (DTC) ni hatua madhubuti katika kujenga taifa lenye nguvu kazi bunifu, mahiri na yenye ushindani wa kimataifa, sambamba na utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014, Toleo la 2023, pamoja na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Akizungumza Novemba 27, 2025, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amesema DTC limekusudiwa kuwa kitovu cha utoaji wa elimu ya ufundi nchini, likiwa na jukumu la kuwapa vijana ujuzi na stadi za kazi zinazohitajika katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.

Amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuandaa kizazi chenye uwezo wa kushindana, kuvumbua, kujiajiri na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kisasa.
Naibu Katibu wa Wizara hiyo, Dkt. Hussein Mohamed Omar, amesema ujenzi wa awamu ya kwanza ya chuo hicho umekamilisha majengo muhimu ikiwemo madarasa, mabweni, ofisi, karakana pamoja na ununuzi wa samani za kisasa.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia yanakuwa ya kisasa ili kuendeleza dira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kukuza ujuzi na kuongeza tija ya rasilimali watu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Prof. Preksedis M. Ndomba, amesema tayari watumishi saba wameajiriwa kwa ajili ya kuanzisha shughuli za DTC, na maandalizi yanaendelea kuhamisha watumishi wengine kutoka DIT ili kukifanya chuo hicho kiwe na timu bora ya kitaaluma.

Ameeleza kuwa mahitaji ya kada 39 mpya yameainishwa na kuwasilishwa kwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kukamilisha taratibu za ajira.
Prof. Ndomba ameongeza kuwa ujenzi wa miundombinu ya maji safi, maji taka na barabara umefikia asilimia 15, huku ukisimamiwa sambamba na mikataba ya usambazaji wa samani na vifaa vya zimamoto.
Amebainisha kuwa DTC tayari limewasilisha maombi ya kusajiliwa na kutambuliwa na NACTVET, na mara baada ya miundombinu kukamilika, ukaguzi wa mwisho utafanyika ili kukamilisha hatua za usajili na kuruhusu chuo kuanza kutoa mafunzo yake rasmi.





