Julai 10, mwaka huu, Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya Kikwete, aliwaoongoza Watanzania katika maadhimisho ya miaka 50 ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), yaliyofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

 

Amiri Jeshi Mkuu huyo aliwakumbusha Watanzania historia ya JKT, umuhimu, madhumuni ya kuundwa, malengo na majukumu yake kwa Taifa. Itakumbukwa kwamba, Machi 31 mwaka 1964, Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere, katika Kambi ya JKT Mgulani aliwaeleza vijana umuhimu wa kuanzishwa kwa jeshi hilo.

“Vijana nadhani mnaelewa kwa nini mpo hapa, mpo hapa kwa ajili ya kujifunza kulitumikia Taifa letu, sisi hasa watu ambao tumezaliwa na kukulia katika ukoloni, tunalo zoea moja kubwa, ambalo tuliambukizwa na wakoloni; tunajua sana kunung’unika, sasa vijana nasema mumo katika jitihada za kubadili upuuzi huu utoke katika nchi yetu.

 

“Hii ni nia ya serikali kwamba, hapa watapita watu wa aina yote, kesho na kesho kutwa hapa ndiyo mlango mkuu, kama hukupita hapa huingii mahali pengine ni sharti upite kwanza mlango huu hapa, ” ni maneno ya Mwalimu Jerere.

 

Kutokana

na kufanyika kwa maasi ya Jeshi la Tanganyika Rifles (TR), serikali iliona umuhimu wa kuanzishwa kwa JKT, ambapo ilikuwa hatua maalum ya kuwaandaa vijana kulinda usalama wa Taifa lao usiku na mchana.

 

Malengo mengine yalikuwa ni kujenga  mshikamano, udugu, kujitegemea, kuongeza ufanisi wa kazi, nidhamu, kujituma na kuwaandaa kulitumikia Taifa kupitia vyombo vya ulinzi na usalama, sanjari na sekta binafsi kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.

 

JKT lilifanikiwa kutimiza malengo yake kitaifa na kimataifa kuwakomboa wananchi kiitikadi, kielimu, kisaikolojia, kiutamaduni, kiutendaji na kwamba hakukuwa na ubaguzi ulioruhusiwa kuota mizizi miongoni mwa jamii.

 

Kufanikiwa kwake kulitokana na uadilifu wa viongozi waliopewa dhamana kuongoza JKT, ambao walishirikiana na watendaji wake kutimiza wajibu wao kulingana na dhamana walizokabidhiwa. Wananchi walijenga imani kubwa kwa JKT kulingana na jinsi ilivyokuwa imejipanga katika nyanja mbalimbali kutekeleza majukumu ya Serikali katika suala zima la malezi ya vijana na uzalishaji mali.

 

Historia ya JKT

Miongoni mwa taasisi zilizoanzishwa na Serikali ya Tanganyika baada ya Uhuru, Desemba 9, 1961  ni JKT ili kuepusha athari zilizoachwa na wakoloni zisilete madhara miongoni mwa jamii.

 

Rais Kikwete anasema JKT ilianzishwa ili kuponya athari zilizoachwa na wakoloni katika suala la ubaguzi, udini, ukabila, rangi na tofauti ya kipato, hatua ambayo ilifanikiwa kutokana na Taifa kutoa elimu kwa wananchi na kuandaa vijana kutumikia nchi yao katika vikosi na kambi mbalimbali za malezi na mafunzo.

 

Taasisi hiyo ina wajibu wa kuhakikisha maendeleo ya nchi yanafikiwa katika sekta ya uzalishaji mali kupitia kilimo, ili kuwakomboa wananchi kiuchumi kwa kutoa mafunzo zaidi ya ujasiriamali vikosini.

 

Kuanzishwa kwake kulitokana na mawazo ya Mwalimu Nyerere na Rashidi Kawawa (Simba wa Vita), ambao kwa pamoja waliona ipo haja ya kuanzisha taasisi itakayokuwa na jukumu la kuwapatia vijana malezi na kuwaandaa kiutendaji.

 

Walipoafikiana mawazo yao yalipelekwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU Youth League), Joseph Nyerere, ambaye naye aliyafikisha katika Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika mkoani Tabora Agosti 25, 1962.

 

Mkutano huo uliafiki mawazo ya viongozi hao na Aprili 19, 1963, Baraza la Mawaziri la Tanganyika chini ya Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, Mwalimu Nyerere, lilipitisha azimio la Umoja huo.

 

Julai 10, 1963, JKT ilianza kutekeleza majukumu yake kwa kuwachukua vijana kutoka mikoa mbalimbali ya nchi kujiunga na jeshi hilo, na kundi la awali la vijana 11 kutoka wilaya 11 walipata mafunzo Kambi ya JKT Mgulani, Dar es Salaam.

 

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, vijana hao walikuwa ni makatibu wa Umoja wa Vijana wa TANU, waliopelekwa nchini Yugoslavia mwaka 1962 kwa mafunzo ya uongozi wa vijana – Z. Kiango, S. Chale, P. Lwegarulira, R. Kamba, H. Ngalason na J. Ndimugango (wote sasa hawapo jeshini).

 

Wengine ni M. Mhando (Senior Guide), D. S. Msilu (Master), E. S. Mwakyambiki (Senior Master), A. I. Msonge (Master) na L. M. Mitande (hawa wangali katika Jeshi la Kujenga Taifa.)

 

Agosti 1963, kikundi kingine cha watu watano kilijiunga JKT na kupatiwa mafunzo ya uongozi wa vijana jeshini, ambacho ni  S. Desai, E. Simkone, J. Mwanimlele (Asst Master) na A. A. Moyo (Asst Master).

 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa JKT, Mwalimu Nyerere aliwaambia wananchi kuwa umuhimu wa jeshi hilo unatokana na Taifa kuhitaji huduma ya vijana kulitumikia Taifa lao katika majukumu mbalimbali ya kujitokeza kijamii, kiuchumi, kielimu na kiitikadi.

 

Pamoja na hayo, mwaka 1964 ilitungwa Sheria ya JKT (National Service Act), ambayo ilianzisha mafunzo kwa mujibu wa sheria na mwaka 1966 na 1967 sheria ilifanyiwa marekebisho kuwezesha vijana waliokuwa wanahitimu kidato cha nne na sita kujiunga katika mafunzo yake.

 

Operesheni Azimio la Arusha

Kundi la viongozi mbalimbali wa kitaifa lilijiunga mwaka 1968 kwa mafunzo maalum ya uongozi wa JKT, wakiwamo Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Makamu wa Kwanza wa Rais, Mzee Aboud Jumbe Mwinyi, Makamu wa Pili wa Rais na Waziri Mkuu, Rashidi Kawawa, na Spika wa Bunge la Jamhuri, Chifu Adamu Sapi Mkwawa, ambalo lilikuwa Opresheni Kazi ‘A’.

 

Mwaka 1975, JKT iliunganishwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ingawa majukumu ya msingi yalibaki ndani ya jeshi hilo, ikiwa ni Brigedi ya uzalishaji ya Jeshi.

 

Athari za mtikisiko wa uchumi duniani

Kutokana na kuyumba kwa uchumi wa nchi zilizoendelea kwa viwanda barani Ulaya na Marekani katika miaka ya 1980-1995, nchi nyingi changa zilizokuwa zinaendelea ikiwamo Tanzania ziliathirika kiuchumi. Amiri Jeshi Mkuu, Rais Kikwete, anasema, Serikali ililazimika kusitisha shughuli za JKT mwaka 1994 hadi 2001 kwa vijana kwa mujibu wa sheria.

 

Kusitishwa kwa mafunzo ya JKT, athari nyingi zilijitokeza miongoni mwa jamii ikiwa ni pamoja na mmomonyoko wa maadili kwa viongozi, watendaji, nidhamu, kuongezeka kwa vitendo viovu mitaani, wizi, uvutaji bangi, ubwiaji wa dawa za kulevya, ubakaji, ujambazi na ubaguzi uliongozeka na kuleta fedheha nchini.

 

Kutokana na hali hiyo, viongozi wa JKT walikabiliana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza sanjari na kufutwa kwa jeshi hilo. Hali hiyo ilitokana na ushawishi wa mataifa yaliyokuwa yanatoa misaada katika nyanja mbalimbali za jamii kwa viongozi wa kitaifa waliokuwa na dhamana ya madaraka, ambao walitaka JKT ifutwe ama ishushwe hadhi.

 

Serikali ilikataa mawazo hayo kwani yalilenga kuparaganisha Taifa ili kutoa mwanya wa kuotesha upya mimea ya ubaguzi, udini, ukabila na vitengo vingine visivyofaa katika jamii.

 

Tume maalum ya wataalamu iliyoteuliwa na Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Makame Rashid wakati huo, ilifanya kazi yake vema na kuishauri Serikali kutofanya ajizi kufuta jeshi hilo kwani athari zake zingekuwa kubwa zaidi.

 

Kufungwa kwa kambi

Mtikisiko wa uchumi duniani uliathiri shughuli mbalimbali, hivyo ulichangia kambi za JKT za kilimo na ufugaji kufungwa, ikiwa ni pamoja na Luwa mkoani Rukwa, Msange- Tabora, Mpwapwa-Dodoma na Makuyuni-Arusha.

 

Kambi hizo zilitumika kutoa mafunzo ya kilimo na ufugaji kwa nadharia na vitendo. Vijana walikuwa wanajiunga na JKT kila mwaka kwa mkataba maalum, hivyo ziliathiri majukumu yake na miundombinu yake.

 

Kuzinduliwa kwa mafunzo ya JKT

Machi 26, mwaka huu, Amiri Jeshi Mkuu, Rais Kikwete alizindua mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria, yalizinduliwa upya, baada ya kusimamishwa kwa zaidi ya miaka 19.

 

Mafunzo hayo yalikuwa ya wiki tatu kwa wabunge 22 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na miaka miwili ya kujitolea Operesheni Miaka 50 ya JKT Kambi ya JKT Ruvu mkoani Pwani.

 

Rais Kikwete ni miongoni mwa viongozi wa kitaifa waliopitia mafunzo ya jeshi hilo katika kambi hiyo kwa mujibu wa sheria, Operesheni Tumaini mwaka 1972 ambaye alikuwa Kombania ‘A’ akipatiwa namba ya JKT 9983.

 

Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Raphael Muhuga alimwambia Amiri Jeshi Mkuu kwamba mafunzo ya miezi mitatu yalianza Machi 4, mwaka huu, Kambi ya JKT Bulombora-Kigoma, Msange-Tabora, Ruvu-Pwani na Mgamboa-Tanga, ambayo yaliwashirikisha vijana 5,000 kati ya 41,000 waliohitimu kidato cha sita mwaka huu na yaligharimu Sh bilioni 7.5.

 

Rais Kikwete alisema wabunge walioomba kujiunga JKT ni 47 kati ya hao, 24 walihudhuria mafunzo kwenye kambi walizopangiwa, 22 walihitimu na wawili hawakufaulu kutokana na sababu mbalimbali za kiafya.

 

Dira ya JKT

Dira ya JKT inataka Tanzania iwe nchi ya watu waliolelewa vema kitaifa na kujengwa katika misingi ya nidhamu, kujiamini, moyo wa uzalendo, umoja na udugu, kupenda kazi na kutekeleza wajibu, tayari kuitumikia nchi yao katika suala zima la uchumi, elimu, ulinzi na usalama.

 

JKT inaendeshwa kwa kufuata misingi, maadili ya kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa ambayo ni uadilifu, kujitolea, mshikamano, umoja, uzalendo, nidhamu na kufanya kazi.

 

Mafanikio yake kwa Taifa

JKT ilifanikiwa kuimarisha umoja wa kitaifa, ambapo vijana mbalimbali waliohitimu mafunzo hayo walijituma kufanya kazi za mikono kwa kujiheshimu, walikuwa viongozi mahiri, wavumilivu, wabunifu na walithamini kuhifadhi utamaduni wa taifa.

 

Jeshi hilo limechangia kuimarisha michezo mbalimbali na kuiletea Tanzania sifa kitaifa na kimataifa, pia vijana walikuwa mstari wa mbele kuokoa jamii katika majanga ya asili yaliyotokea kwa vipindi tofauti hapa nchi.

 

Taasisi hiyo ni mfano mzuri wa kuigwa kutokana na mataifa mbalimbali duniani kufika nchini kujifunza shughuli zake na wao kuanzisha JKT katika nchi zao, ikiwamo JKU Zanzibar, Zambia na Guyana.

 

Hifadhi ya mazingira imepewa kipaumbele kwa kutambua umuhimu wake kwa maisha ya jamii na wanyama, hivyo JKT hugawa miche bure kwa wananchi waishio jirani na kambi, sanjari na kubadilishana uzoefu na utaalamu wa suala zima la utunzaji na uhifadhi wa mazingira.

 

Serikali iliahidi kuendelea kuisaidia JKT kutimiza malengo yake kwa Taifa kwa uharaka na wakati unaotakiwa na kwamba aliwataka watendaji kusimamia mafunzo na malezi ya vijana kwa karibu zaidi ili kuepusha ubabaishaji.

 

Operesheni za vijana JKT

JKT hadi sasa imekwishaendesha zaidi ya Operesheni 102 na baadhi yake ni pamoja na Ujenzi  1980, Tija 1980, Juhudi 1981, Imarisha 1981, Tekeleza ‘B’ 1982, Kujihami 1982, Safisha1983, Nguvu Kazi 1983 na Mshikamano 1984.

 

Nyingine ni Wajibu 1984, Vijana 1985, Okoa 1985, Awamu ya Pili 1986, Nidhamu 1986, CCM Miaka 10 – 1987, Miaka 20 ya Azimio la Arusha 1987, Kizota 1988, Miaka 25 ya JKT 25 ya JKT 1988, Mpito 1989, Programu ya Chama 1989 na Kambarage 1990.

 

Watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa kitaifa, vyama vya siasa, Mkuu wa JKT nchini Msumbiji, Zambia, Balozi wa Israeli nchini Tanzania, Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenereli Samwel Ndomba na wageni mbalimbali walihudhuria maadhimisho hayo.

 

 

 

Please follow and like us:
Pin Share