Tanzania imeanza kuchukua hatua madhubuti kuweka mikakati itakayoiwezesha kukabiliana na mlipuko wa virusi vya corona iwapo utatokea nchini.





Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, akizungumza wakati alipofanya ziara ya kukagua utayari wa kukabiliana na virusi vya corona katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere hivi karibuni.

Mikakati hiyo imebainishwa wiki iliyopita na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Pamoja na kueleza yaliyofanywa na yatakayofanywa na serikali iwapo virusi hivyo vitaingia nchini, Waziri Ummy pia anabainisha ni nini mtu binafsi anapaswa kufanywa ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo vinavyosambaa kwa kasi duniani.

Virusi hivyo viliibuka nchini China mwishoni mwa mwaka jana lakini hadi hivi sasa vimesambaa katika nchi takriban 54 duniani, zikiwemo Algeria, Misri na Nigeria za Bara la Afrika.

Ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) inasema hadi kufikia Februari 27, mwaka huu jumla ya watu 83,652 wamethibitika kuambukizwa corona huku idadi ya vifo vitokanavyo na kirusi hicho ikiongezeka kila siku.

Ripoti ya WHO inaeleza kuwa asilimia 94 ya wagonjwa walioathirika kote duniani wamo nchini China, na Waziri Ummy amewatoa wasiwasi Watanzania kuwa mpaka sasa hakuna mshukiwa wa kirusi cha corona wala mgonjwa aliyepatikana nchini.

Waziri Ummy anasema tahadhari inahitajika ya kujikinga na ugonjwa huo kutokana na Tanzania kuwa na mwingilinao wa wasafiri kutoka mataifa mengine yaliyoathirika.

“Wapo Watanzania wanakwenda kwenye nchi zilizoathirika na wapo wageni wanaingia wakitoka kwenye nchi hizo, serikali imejiandaa kukabiliana na ugonjwa huu kupitia maandalizi ya muda mrefu ambayo serikali imekuwa ikifanya kudhibiti magonjwa ya kuambukizwa,” anasema Ummy.

Serikali inaendelea na uchunguzi na kufuatilia wasafiri wote wanaoingia nchini kupitia mipaka yake pamoja na viwanja vya ndege, bandari na nchi kavu.

Anaeleza kuwa Tangu Januari 30 hadi Februari 27, jumla ya wasafiri takriban 11,048, wamechunguzwa katika mipaka ya Tanzania na wote wametokea katika nchi zilizo na mlipuko wa ugonjwa huo ikiwamo China.

Anasema serikali inavyo vipima joto 140, vipimo vya mikono 125 na vya kupimia watu wengi kwa mpigo 15, ambavyo vimefungwa na vinatumika katika maeneo ya mipakani, vikiwemo viwanja vya ndege na bandarini.

“Tuna walkthrough thermo scanners, wapo wanaosema kwamba tumepita na hatujapimwa, si kweli, bali ukipita pale kipimo kinakusoma, unakuwa scanned na tayari unakuwa umepimwa. Na pale ambapo tunakuwa na shaka ndipo tunapokuchunguza zaidi,” anasema Ummy.

Hata hivyo, anaongeza kuwa serikali imeongeza idadi ya wataalamu wa afya katika maeneo ya mipakani ikiwa ni pamoja na kuajiri watumishi 100 wa kuimarisha zoezi la upimaji wa wasafiri wanaoingia nchini kupitia mipakani.

“Tumeandaa dawa, vifaa kinga na vitakasa mikono ambavyo tayari vimefikishwa kwenye bohari za dawa za kanda kwa ajili ya kutumika endapo ugonjwa huu utathibitika kutokea nchini,” anasema.

Kwa mikoa yenye uwezekano mkubwa wa kupata wagonjwa, anasema kumeandaliwa vituo vya kuwaweka washukiwa na kuwapatia matibabu.

Aidha, anasema serikali imeimarisha uwezo wa kupima sampuli kupitia maabara yake ya taifa ya afya ya jamii iliyopo kwenye kituo cha kufanya tafiti za magonjwa (NIMR), ambapo watu wote wanaohisiwa kuwa na ugonjwa huo au kuonyesha dalili ndani ya saa nne hadi sita  inaweza kutoa majibu ya vipimo.

Anasema serikali itaendelea kutoa elimu ya afya na mafunzo kwa umma kupitia njia mbali mbali ili wananchi waendelee kuchukua tahadhari.

Mafunzo hayo kwa sasa yametolewa kwa Mkoa ya Dar es Salaam, Pwani, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Mwanza na Kigoma na tayari wameunda timu za mkoa zinaitwa ‘rapid response team’ kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Wizara ya Afya imewaelekeza waganga wakuu wa mikoa na wilaya kubainisha vituo vya kutolea matibabu kwa washukiwa wa virusi hivi watakapotokea, kwa sababu haijulikani ugonjwa huu utaanza kuripotiwa wapi endapo ukifika nchini.

Ugonjwa unavyoenea

Virusi vya corona huenea kwa njia ya majimaji yanayosambaa kwa njia ya hewa wakati mtu aliyeambukizwa virusi hivyo anapokohoa au kupiga chafya, kugusa maji maji yanayotoka puani (makamasi), kugusa vitambaa au nguo za mtu aliyepata maabukizi ya ugonjwa huo au kugusa sehemu aliyoshika mtu aliyeambukizwa virusi hivyo.

Ili kujikinga, wananchi wanatakiwa kuzingatia kanuni za afya kwa kufunika mdomo na pua wakati wa kukohoa kwa kutumia kitambaa safi, pia kuvaa glavu mikononi.

Aidha, wananchi wameaswa kuzingatia usafi binafsi, ikiwemo kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono.

Pia wananchi wanatakiwa kujizuia kupeana mikono, kukumbatiana na kubusiana. Aidha, watu wanapaswa kujizuia kusafiri kwenda kwenye nchi ambazo zimeathiriwa na virusi hivyo.

Serikali pia imewataka wananchi kuepuka kugusana na mtu mwenye dalili za maambukizi ya virusi vya corona, hasa mtu mwenye historia ya kusafiri katika nchi zilizoathirika.

Waziri Ummy ameitaka mikoa yote nchini kuwasilisha kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya majina ya vituo vilivyotengwa kwa ajili ya kuhudumia washukiwa, au wagonjwa endapo watatokea katika halmashauri.

Pia kila halmashauri imetakiwa kubainisha kituo mahususi kilichoandaliwa pamoja na vifaa husika kwa ajili ya kupima watu wenye dalili na kuhudumia wale watakaobainika kuambukizwa virusi hivyo.

Hospitali za umma na binafsi zimeshauriwa kuwa na eneo la muda la kumshikilia mshukiwa wakati vipimo vinavyomhusu vikifanyika.

Waziri Ummy pia amewataka wamiliki wa maeneo yenye mikusanyiko ya watu kuhakikisha wanaweka vitakasa mikono, maji yanayotiririka na sabuni ili kuhakikisha watu waliokusanyika wanajiweka safi muda wote.

Watanzania walioko China

Kuhusu Watanzania 504, wakiwamo wanafunzi, waliopo mji wa Wuhan, nchini China ulikoanzia ugonjwa huo, serikali imeendelea kufanya mawasiliano na Serikali ya China kuhakikisha wako salama.

Aidha, Waziri Ummy amewaonya watu wanaosambaza taarifa potofu kuhusu ugonjwa huo na kuwataka kuacha kufanya hivyo mara moja kwani wanaweza kusababisha madhara makubwa kwa jamii.

Nchi ambazo zimeripotiwa kuathirika kwa kiwango kikubwa kwa virusi vya corona ni China,  visiwa vya Hong Kong na Macau, ambako kuna waathirika 78,927 na vifo 2,860.

By Jamhuri