Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Mwanza

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kituo cha umahiri katika sekta ndogo ya ngozi.

Kituo hicho kinachojengwa katika Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam (DIT) kampasi ya Mwanza kinalenga kuimarisha mafunzo ya ujuzi juu ya bidhaa za ngozi yanayotolewa katika kampasi hiyo.

Akielezea namna wizara ilivyojipanga katika kukiimarisha kituo hicho mara baada ya ya kukagua utekelezaji wa mradi huo mwishoni mwa wiki Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema shilingi bilioni 19.6 zimetengwa katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/23 kwa ajili ya Chuo hicho.

“Fedha hizo zinatumika katika kufanya ukarabati na kuongeza Miundombinu ya kufundishia na kujifunzia
Kwa lengo la kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanatoa ujuzi ili kuongeza wataalamu katika teknolojia ya ngozi nchini watakaoleta tija katika mnyororo wa kuongeza thamani mazao ya ngozi, ameongeza Prof Mkenda.

Prof. Mkenda amesema serikali itahakikisha DIT inakuwa kitouo cha umahiri cha utoaji mafunzo ya ufundi na ujuzi katika kuchakata mazao ya ngozi na utengenezaji bidhaa mbalimbali za mazao hayo.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa mafunzo hayo yanatolewa katika kanda ya ziwa kwa kuwa kuna malighafi ya kutosha ya ngozi, hivyo anatarajia kuona chuo hicho kinanufaisha vijana wengi ili wakimaliza mafunzo hayo waweze kuwa mahiri na kujiariri ama kutoa ajira.

Nae Mkuu wa wilaya ya Ilemela, Hassan Masala akizungumza katika ziara hiyo ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu katika Mkoa wa Mwanza ikiwemo kampasi ya DIT ambayo itatoa mchango mkubwa na katika maendeleo ya nchi kupita sekta ya ngozi.

Awali akitoa taarifa ya Chuo Mwenyekiti wa baraza la DIT Mhandisi Dkt. Richard Masika amesema DIT imekuwa ikitoa mafunzo ya ufundi wa utengenezaji bidhaa za ngozi kwa nadharia na vitendo ili kuwajengea uwezo vijana wa waweze kushindana katika soko la ajira kitaifa na kimatafa.