DAR ES SALAAM

NA MWANDISHI WETU

Serikali imetoa mapendekezo ya kushirikishwa kwa taasisi za umma katika mashindano ya kumtafuta mwajiri bora
wa mwaka kuanzia mwakani.
Tangu mwaka 2015 Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), kimekuwa kikitoa tuzo kwa mwajiri bora kila mwaka kwa
lengo la kutathmini na kutambua mchango wa waajiri wenye mikakati bora ya usimamizi wa rasilimali watu kwa
ajili ya kuongeza uzalishaji kibiashara.
Tuzo hiyo pia inalenga kuwahamasisha waajiri kufuata taratibu za kitaifa na kimataifa katika uendeshaji wa biashara zao.
Tuzo hiyo imekuwa ikishirikisha waajiri kutoka sekta binafsi lakini taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu imeeleza kuwa serikali imependekeza kuwa kuanzia mwakani taasisi zilizo katika sekta ya umma nazo zihusishwe kwenye tuzo hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana
na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, wakati wa hafla ya Tuzo ya Mwajiri Bora wa mwaka 2019 iliyoandaliwa na ATE jijini Dar es Salaam. Mgahama alikuwa anamwakilisha Rais John Magufuli.
Mhagama anasema ustawi wa wafanyakazi hauhusu sekta binafsi peke yake, hivyo ili sekta binafsi iwe injini ya kuendesha uchumi, ni lazima pia sekta ya umma nayo iwekeze rasilimali watu ili kuweza kuongeza tija katika maeneo ya kazi.
“Niipongeze ATE kwa kuwa na tuzo hizi. Tungependa kuona ni mashirika gani ya umma yanafanya vizuri katika
kuangalia ustawi wa wafanyakazi na kuleta tija nchini. Uamuzi wa kuwa na washindi wa jumla katika makundi
ya kisekta utaongeza chachu mpya ya mashindano ambayo yatakuza sekta mbalimbali na hatimaye yataboresha na kuleta tija katika ukuaji wa uchumi wa taifa letu,” anasisitiza Mhagama.
Waziri Mhagama anaitaka ATE kuendelea kutoa mafunzo katika maeneo ya kazi na juu ya sheria za kazi na
usimamizi wa rasilimali watu, kwani yatasaidia kupunguza migogoro mahala pa kazi, hivyo kujenga mazingira
tulivu ya kibiashara ndani ya maeneo ya kazi.
“Takwimu zinaonyesha mafunzo ambayo yameratibiwa na kuandaliwa na ATE, yameshirikisha vijana 1,437 ambao
waliidhinishwa na kupata nafasi kwa waajiri huku kwenye tovuti ya serikali wapo vijana 6,919, walijiandikisha hadi
Julai mwaka huu. Hivyo nitoe rai kwa waajiri wapeni fursa vijana ili waweze kujifunza kwa vitendo,” anasema.
Naye Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu), Stella Ikupa, amewapongeza ATE kwa juhudi
zao za kuunga mkono juhudi za serikali za kuwawezesha watu wenye ulemavu, hivyo amewasihi waendelee kujenga mazingira rafiki mahala pa kazi ili watu wenye ulemavu na watu wenye mahitaji maalumu waweze kufanya kazi na
kuchangia kwenye maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya ATE, Jayne Nyimbo, anafafanua kuwa ushirikiano wanaoupata
serikalini umesaidia kuboreshwa kwa tuzo hizo ambazo zimekuwa zikiboresha mazingira ya kazi na ajira nchini.
Awali, Ofisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Dk. Aggrey Mlimuka, alisema Tuzo ya Mwajiri Bora wa Mwaka mwaka huu imefanyia kazi ushauri uliotolewa na serikali mwaka jana (Waziri Mhagama) kuwa katika tuzo za mwaka huu ziongeze vipengele vipya vitatu ambavyo vimezifanya tuzo za mwaka huu kuwa na jumla ya vipengele 38.
“Vipengele vilivyoongezeka ni Mwajiri Bora anayeendeleza mafunzo ya ujuzi wa kazi kwa wahitimu, Mwajiri Bora anayetoa mafunzo ya uanagenzi na Mwajiri Bora anayezingatia haki rasilimali ijulikanayo kama Local Content,”
anasema Dk. Mlimuka.

By Jamhuri