Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kigoma
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNCHR) imezindua Mradi wa Kujenga Uwezo wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi katika Mazingira ya Mkoa wa Kigoma.
Mradi huo wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 19 (zaidi ya shilingi bilioni 51), unafadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) kupitia Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (GCF) unaoratibiwa chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC).
Akizindua mradi huo Mei 15, 2025 kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye amesema utatekelezwa katika wilaya tatu ambazo ni Kasulu, Kibondo na Kakonko kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka huu 2025 hadi 2030.

Alisema mradi huo unatarajiwa kunufaisha watu zaidi ya 570,000 na kurejesha takriban hekta 42,000 za misitu na mifumo ya ikolojia ya kilimo ya mkoa huo ambao unapokea zaidi ya wakimbizi 190,000 kutoka nchi jirani zilizoathiriwa na migogoro hasa Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambao wengi wao wanaishi katika kambi za Nduta, Nyarugusu na Mtendeli.
Mhe. Andengenye aliongeza kuwa mradi huo utakuwa ni wa mfano, unaotumia mbinu zinazozingatia hifadhi ya mifumo ikolojia kama mkakati muhimu wa kujenga ustahimilivu wa athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye maeneo yenye changamoto kubwa za kimazingira na migogoro hasa katika kwa jamii za wakimbizi na wakazi wanaozunguka kambi hizo.
Aidha, alisema kati ya mwaka 2011 na 2018, Kigoma ilipoteza takriban asilimia 5.3 ya eneo lake la miti (hekta 108,000 za msitu), kutokana na mahitaji mbalimbali yakiwemo ya kuni hivyo, lengo la mradi ni kujenga uwezo wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi nchini Tanzania mahsusi katika mkoa wa Kigoma.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Kemilembe Mutasa alisema warsha hiyo ya uzinduzi wa mradi imewakutanisha washiriki 90 kutoka maeneo na sekta mbalimbali.
Alisema mradi unakuja na Mkakati wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi (2021-2026) ambazo zinasababisha mvua zilizokuwa na mpangilio, mafuriko, ukame kutokana na shughuli zisizoendelevu.
Bi. Kemilembe pia alisema mradi huo utakuwa chachu katika biashara ya kaboni kwani utahusisha zoezi la upandaji wa miti katika maeneo ya wilaya hizo tatu yatakayotekelezewa mradi.
Naye Bi. Paz Rey kutoka UNEP alisema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na wadau katika kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.
Alisema kuwa uzinduzi wa mradi huo ni hatua mojawapo ya kuungano mkono Mpango Kabambe wa Mazingira uliozinduliwa na kutekeleza na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Bi. Paz alibainisha kuwa katika kuzindua mradi huo kwa wananchi wa Kigoma na mazingira ya mkoa huo kwa ujumla ni mfano mzuri wa kuigwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.
“Naishukuru UNHCR kwa ushirikiano kwetu na hii inaonesha dhahiri namna ushirikiana na Tanzania unavyozaa matunda na kuoata mradi huu na kwa pamoja tutaweza kutatua changamoto hii,” alisema.
Kwa upande wake Bi. Julia Seevinck kutoka UNHCR aliishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kuwapokea na kuwapa hifadhi wakimbizi.

Aidha, alisema kuwa mabadiliko ya tabinchi ni changamoto kubwa inayoikabili dunia na kuathiri kwa kiasi kikubwa wananchi wote kutokana na majanga mbalimbali.
Bi. Julia alisema kuwa pamoja na changamoto mbalimbali, athari za mabadiliko ya tabianchi zinajidhihirisha kupitia mvua za el nino zinanyoesha na kusababisha mafuriko, hivyo zinafanyika jitihada mbalimbali katika kukabiliana nazo.
