DAR ES SALAAM

NA REGINA GOYAYI (DSJ)

Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza, amewataka wahitimu wa kozi za uandishi wa habari nchini kuutumia ujuzi walioupata kwa weledi ili waweze kudumu katika ajira.
Akizungumza katika Mahafali ya 24 ya Chuo cha Uandishi wa Habari cha DSJ hivi karibuni, Shonza amesema hivi sasa kuna changamoto kubwa kupata ajira, hivyo ni vema wahitimu hao wakatumia vizuri fursa ambazo watazipata.
“Soko la ajira ni gumu sana lakini bahati nzuri nyie mmepata ujuzi ambao unapaswa muutumie kuhakikisha kuwa mnabaki ndani ya soko la ajira si tu kwa kusubiri kuajiriwa, bali kutafuta fursa za kujiajiri kwa kutumia ujuzi mliopewa,” anasisitiza Shonza.
Anabainisha kuwa kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano na kushamiri kwa mitandao ya jamii kunaweza kutumiwa na watu wenye ujuzi wa msuala ya habari kujipatia ajira.
“Tunatambua umuhimu wa uwepo wa chuo hiki kwani kinafanya kazi kubwa katika ukuaji wa sekta ya habari. Lakini ili hilo lionekane wazi wazi vijana wanaotoka hapa hawapaswi kubweteka. Watumie mafunzo waliyoyapata kukabiliana na changamoto katika sekta. Tunaamini pia kuwa watatanguliza uzalendo katika kazi zao,” anasisitiza.
Anasema wahitimu hao wanapaswa kutumia kalamu na sauti zao vizuri kwa upande wa watangazaji ili kuhakikisha kuwa wanasaidia ujenzi wa nchi.
“Tukumbuke kuwa na sisi ni sehemu ya Watanzania ambao wanapaswa kufanikisha azima ya serikali ya ujenzi wa uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025. Hivyo, kazi zetu zinapaswa kuhakikisha tunasaidia kufanikisha hilo,” anasema.
Amewataka wahitimu hao kuhakikisha wanazingatia weledi wa kazi zao pamoja na kufuata matakwa ya maadili, sheria na kanuni ili kuhakikisha kuwa wanachokifanya kinakuwa na mcahngo chanya kwa jamii na taifa.
Naye Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Selemani Shekonga, anazitaja changamoto zinazokabili chuo hicho kuwa ni pamoja na uwezo mdogo wa wanafunzi kugharamia masomo yao na kuiomba serikali ifikirie njia za kuwawezesha kujumuishwa kwenye orodha ya wanafunzi wanaostahili kupata mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu au kwa utaratibu mwingine utakaoonekana kuwa unafaa.
Aidha, anasema kuna tatizo kubwa kwa wanafunzi kukosa maeneo ya kufanya mafunzo kwa vitendo, jambo ambalo linakwamisha maendeleo yao kimasomo.
Shekonga pia anaiomba serikali ikisaidie chuo chao kupata masafa ya redio ambayo wanaitumia kwa ajili ya mafunzo, kwani Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) imeshindwa kuwasaidia.

1143 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!