Mwalimu Julius Nyerere aliamini katika dhana ya maendeleo ya watu, na si maendeleo ya vitu. Dhana hii imepewa tafsiri nyingi. Wapo wanaoamini kuwa Mwalimu hakutaka kuona barabara, majengo makubwa makubwa na miradi mingine yenye thamani ya mabilioni ya fedha.

Lakini ukirejea kwenye matendo ya Mwalimu unakutana na vielelezo vinavyokinzana na hao wanaojaribu kuupindisha ukweli wa dhana hiyo. Mathalani, kama Mwalimu hakuamini katika maendeleo ya vitu, basi leo hii tusingeona mabwawa kama yale ya Mwanzugi, Tabora; tusingeona vituo vya umeme kama vile Kidatu mkoani Morogoro; tusingeshuhudia mambo makubwa makubwa yaliyofanywa na serikali chini ya uongozi wake.

Lakini wapo wanaodhani kuwa Mwalimu aliposema vile alimaanisha kuwa maendeleo ya vitu ni vitu vyote vilivyohusu anasa au ambavyo havikuwa na mchango wowote wa maana kwa maendeleo ya watu.

Mathalani, Mwalimu hakuona umuhimu wa kujenga nyumba za starehe badala ya kujenga zahanati, shule au miradi mingine yenye manufaa kwa wananchi wengi.

Mwalimu hakuamini katika ununuzi wa magari ya kifahari, badala yake alijielekeza zaidi kwenye ununuzi wa malori, matrekta, magari ya usafiri na kadhalika. Kwake yeye, magari ya kifahari yalikuwa ni ‘maendeleo ya vitu’.

Mtazamo wa Mwalimu ulikuwa kupambana na maadui wakuu watatu – ujinga, maradhi na umaskini. Huwezi kupambana na maadui hao bila kuwa na miundombinu ya maana. Yawezekana kama si umaskini, Mwalimu angeondoka madarakani akiwa ameshajenga barabara kuu zote za kuunganisha mikoa na wilaya kwa kiwango cha lami, au angejenga flyover na interchange kila palipoonekana kuhitajika huduma hiyo.

Lakini tusisahau ukweli kuwa baadhi ya mambo yanakwenda na mahitaji ya muda. Mathalani, Mwalimu asingejenga interchange Ubungo wakati ule kwa sababu haukuwapo msongamano wa magari. Angejenga Ubungo na kupuuza Reli ya Uhuru, Watanzania na walimwengu wangemshangaa.

Mwalimu asingejenga chuo kikuu kikubwa kama UDOM kwa sababu wanafunzi wenyewe wa kujaza chuo hicho hawakuwapo! Lakini alihakikisha Mlimani kunakuwa na nafasi ya kutosha kwa maendeleo ya baadaye. Leo tunaona chuo hicho kinachopanuliwa.

Kadiri muda unavyokwenda ndivyo mahitaji yanavyoongezeka – na hapo ndipo dhana yake nyingine ya ‘kupanga ni kuchagua’ inapodhihirika.

Kinachofanywa sasa na Awamu ya Tano ni mwendelezo mpana wa yale yaliyofanywa na watangulizi. Kama ni mabwawa ya umeme, Mwalimu na mzee Benjamin Mkapa walishajenga, lakini mahitaji ya leo yanamlazimu Rais John Magufuli kujenga bwawa kubwa zaidi.

Kama ni chuo kikuu, Mwalimu alishajenga, lakini mzee Jakaya Kikwete akaona kile cha Mlimani na vingine havitoshi. Akaamua kuleta chuo kikuu – kikuu kweli kweli kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Kama ni hospitali, tayari tulishakuwa na Muhimbili, lakini waliomfuata Mwalimu wakaona wapanue Muhimbili, na kana kwamba haitoshi mzee Kikwete akaongeza Mloganzila.

Reli ilishakuwapo – ile ya Wajerumani – na nyingine zilizojengwa baada yao. Lakini Rais Magufuli ameona alete reli inayokidhi mahitaji ya leo ya nchi na dunia; na sasa inajengwa reli ya kisasa.

Kama Mwalimu Nyerere aliondoka madarakani Shirika la Ndege Tanzania (ATC) likiwa na ndege, si haba! Hata alipofariki dunia, ni ndege ya ATC iliyopelekwa Uingereza kurejesha mwili wake. Wanaobeza umuhimu wa ndege, basi waanze wakati wa Mwalimu aliyeona umuhimu wa aina hiyo ya usafiri kwa uchumi na maendeleo ya wananchi. Iweje leo kufufua ATC kuwe nongwa? Kwanini ujenzi wa reli uwe suala la mjadala? Kwanini kuongeza wigo wa umeme unaozalishwa liwe ni suala la kumwandama anayetekeleza mradi huo?

Kama kweli tunataka kuwa wanafunzi wazuri wa historia, ni wazi kuwa Rais wa Awamu ya Sita atalazimika kuja na mambo mengine makubwa zaidi yenye kulenga kukidhi mahitaji ya wakati huo. Kwa mtazamo tu wa kawaida, miaka 10 huenda Dar es Salaam ikawa imeshaungana na Chalinze! Kama hivyo ndivyo, atakayekuwa madarakani wakati huo atalazimika kuongeza au kupanua miundombinu kulingana na mahitaji.

Nchi zilizoendelea ziliweka mkazo kwenye miradi mama – yenye kusaidia kuchochea mapinduzi ya uchumi na viwanda; kwa hiyo kuwa chachu ya maendeleo ya watu.

Tanzania leo inatajwa kuwa nchi kinara katika usambazaji wa umeme vijijini (ingawa Butiama ni kama hakuna umeme). Umeme si nguzo na nyaya pekee, bali ni uzalishaji na usambazaji wa nishati hiyo. Haya ni mafanikio makubwa.

Pengine mahali tunapopaswa kupatazama zaidi ili kuleta uwiano wa hii miradi mikubwa na maendeleo ya watu ni katika uboreshaji wa kilimo na ufugaji nchini mwetu. Ajira kuu iko kwenye kilimo. Tuelekeze nguvu huko.

Kabla ya kumwandama Rais Magufuli kwa uamuzi wake wa kujenga miradi mikubwa mikubwa, tuyatazame kwanza mahitaji ya leo. Miradi mikubwa ina faida pana sana katika mapinduzi ya uchumi na maendeleo ya nchi. Ukiwasikiliza wanaopinga miradi hii wakati mwingine unabaki kujiuliza, Watanzania wanataka nini? Miradi haikuwapo tulilalamika, inajengwa tunalalamika! Tufanye nini? Tugawane pesa za hii miradi ili kila mmoja ajue cha kufanya? Kazi kweli kweli.

535 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!