* Kila Mtanzania sasa kupata huduma bora za afya bila ubaguzi
*Serikali, TIRA kuhakikisha bima hii inakuwa endelevu kwa wote
*Mkakati ni kuona afya za wananchi zinakuwa bora, uchumi unakua
*TIRA wazindua jengo lao la makao makuu Ndejengwa jijini Dodoma
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Sekta ya bima nchini Tanzania inaendelea kupiga hatua kubwa katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi huku serikali ikiweka msisitizo katika kuhakikisha huduma za bima zinawafikia Watanzania wote.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Saada Salum Mkuya, wakati akizindua Taarifa ya Utendaji wa Soko la Bima kwa mwaka 2024 katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma hivi karibuni.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wakuu wa taasisi, watoa huduma za bima, wakurugenzi wa kampuni, viongozi wa dini, waandishi wa habari na wadau wa sekta ya fedha.
Katika hotuba yake, Dk. Mkuya amesema serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) itaendelea kujenga mazingira rafiki ya utoaji wa huduma za bima na kuhakikisha sekta hiyo inakuwa injini ya maendeleo ya kiuchumi.

Dk. Mkuya ameeleza kuwa ripoti hiyo ya mwaka 2024 ni kielelezo cha uwazi wa sekta ya bima na ni nyenzo muhimu kwa serikali, wawekezaji na wananchi kutathmini mwenendo wa soko.
“Ripoti hii ni chombo cha uwazi. Inatoa taswira halisi ya ukuaji wa sekta, inadhihirisha jinsi wananchi wanavyozidi kujiunga na huduma za bima, na inatupa mwelekeo wa kuboresha zaidi mifumo ya utoaji huduma,” anasema Waziri.
Aidha, amebainisha kuwa sekta ya bima ni nyenzo muhimu katika uchumi wa taifa, kwani inachochea uwekezaji, inalinda mali na rasilimali, na kuchangia katika pato la Taifa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kumekuwa na ongezeko kubwa la wanufaika wa huduma za bima, kampuni zinazotoa huduma hizo, ajira katika sekta hiyo, na thamani ya mali zilizokatiwa bima.

Waziri ameipongeza TIRA kwa kusimamia vema soko hilo kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Fedha (FSDMP 2019/20–2029/30), Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III 2021/22–2025/26) na Ilani ya CCM ya 2020–2025, ambavyo vyote vinatambua mchango wa sekta ya bima katika ustawi wa taifa.
“Mipango hii inazingatia maeneo matatu: kwanza, kujenga ufahamu na masilahi ya umma katika bima. Pili, kusisitiza umuhimu wa bidhaa za bima, kubuni bidhaa na huduma za bima zinazokidhi mahitaji ya soko, na tatu, kuanzisha mifumo ya kushughulikia madai na malalamiko ya wateja.
“Kwa hayo yote niliyonukuu kutoka kwenye mipango hiyo ambayo Wizara ya Fedha imejiwekea, ni wazi kuwa taarifa hii imetuonyesha mageuzi makubwa katika maeneo hayo mahsusi,” anasema Dk. Mkuya.
Ujenzi wa jengo jipya
Akizungumzia hatua ya ujenzi wa jengo jipya la Makao Makuu ya TIRA lililozinduliwa siku hiyo, Dk. Mkuya anasema jengo hilo ni alama ya maendeleo na dira ya kizazi kipya cha utendaji wa taasisi hiyo.
“Jengo hili ni zaidi ya miundombinu; ni chachu ya ufanisi na ubunifu. Litawawezesha watumishi wa TIRA kufanya kazi kwa ufanisi zaidi, kuboresha huduma kwa wananchi, na kuongeza uwazi katika usimamizi wa soko,” anasema.
Ameongeza kuwa serikali inatarajia TIRA kutumia jengo hilo kama kichocheo cha mageuzi ya kidijitali na upanuzi wa huduma za bima hadi vijijini, sambamba na utoaji elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa bima.
Dk. Mkuya ametoa pongezi kwa Kamishna wa Bima Tanzania, Dk. Baghayo Saqware, Naibu Kamishna, Khadija Issa Said, na Bodi ya Taifa ya Bima inayoongozwa na Moremi Marwa, kwa usimamizi thabiti na jitihada zilizofanikisha mafanikio hayo.
Akiwasilisha ujumbe maalumu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuya ametoa maagizo kwa wadau wa sekta ya bima kuhakikisha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote inatekelezwa kikamilifu ndani ya siku 100 baada ya Uchaguzi Mkuu.

“Agizo hili linaonyesha dhamira ya serikali kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya bila vikwazo vya kifedha. Hii ni hatua muhimu kuelekea taifa lenye afya bora na uchumi imara,” anasema.
Amewataka wadau wote wa sekta ya bima kushirikiana na serikali kupitia TIRA, Wizara ya Afya na taasisi nyingine katika kutekeleza majukumu yao ya kisheria, kuelimisha umma, kubuni bidhaa nafuu za bima ya afya na kuhakikisha huduma bora kwa wote bila ubaguzi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Bima atoa mwito
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Bima, Marwa, anasema sekta ya bima imepiga hatua kubwa kutokana na ushirikiano wa serikali, TIRA na wadau wa sekta.
“Taarifa hii ya soko ni muhimu kwani inatupa mwongozo wa tulipotoka, tulipo na tunakoelekea. Ni nyenzo ya kuhamasisha uwekezaji, kukuza ajira na kuongeza pato la taifa,” anasema Marwa.
Anasema uzinduzi wa taarifa ya utendaji wa soko la bima na jengo jipya la TIRA ni sehemu ya mageuzi ya kimfumo yatakayoongeza uwazi, ushindani, na ubunifu wa bidhaa za bima kwa wananchi wote, mijini na vijijini.

Kuhusu jengo, anasema: “Jengo hili jipya la TIRA ni ishara ya dira mpya ya utendaji wa Mamlaka yetu, dira ya ufanisi, uwajibikaji, na ubunifu. Ni jengo litakalorahisisha huduma, kuongeza tija na kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wetu.
“Tunaishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wizara ya Fedha, kwa kuendelea kuunga mkono sekta ya bima na taasisi zake hususan TIRA. Jengo hili ni matokeo ya usimamizi thabiti wa serikali yetu na uongozi imara wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.”
Aidha, anasisitiza umuhimu wa teknolojia katika mageuzi ya sekta ya bima, akisema:
“Tunapaswa kuwekeza katika teknolojia na ubunifu unaolenga kupanua wigo wa bima. Tuwe mabalozi wa bima bora kwa maendeleo ya taifa letu.”
Marwa pia anaishukuru serikali kwa kuendelea kuunga mkono sekta ya bima na kuahidi kwamba Bodi ya Taifa ya Bima itaendelea kutoa ushauri wa kitaalamu kwa TIRA na kuhakikisha sekta hii inakuwa na ufanisi na uaminifu wa hali ya juu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya soko, sekta ya bima nchini imegawanyika katika makundi makuu matatu:
1. Bima ya Maisha – inayoongozwa na kuongezeka kwa uelewa wa wananchi na kupanuka kwa huduma za microinsurance zinazolenga watu wenye kipato cha chini.
2. Bima Isiyo ya Maisha – ikihusisha bima za mali na ajali, ambayo inakua kutokana na kuongezeka kwa tabaka la kati na kasi ya maendeleo ya kiuchumi nchini.
3. Bima ya Afya – inayopata umaarufu mkubwa kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma bora za afya.
Kwa muktadha huo, sekta ya bima imekuwa injini muhimu ya ukuaji wa uchumi, ikichangia si tu katika pato la Taifa, bali pia katika kujenga jamii yenye uelewa, usalama na uthabiti wa kifedha.
Hafla hiyo imeacha ujumbe mzito wa matumaini kwa sekta ya bima nchini. Kupitia ripoti ya mwaka 2024 na jengo jipya la TIRA, Tanzania imeweka msingi thabiti wa kuimarisha usimamizi, uwazi, ubunifu na upanuzi wa huduma za bima nchini.
Dk. Mkuya anahitimisha hotuba yake kwa maneno yenye uzito:
“Tushikamane. Tuwawezeshe Watanzania. Tujenge Taifa lenye afya bora kwa wote.”
Na kwa maneno hayo, waziri amezindua rasmi Taarifa ya Utendaji wa Soko la Bima kwa Mwaka 2024, akisisitiza kuwa sekta ya bima ndiyo nguzo ya ulinzi wa kiuchumi na kijamii wa Watanzania katika safari ya maendeleo endelevu.


