Na Stella Aron, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Taarifa sahihi na za wakati za hali ya hewa ni nyenzo muhimu katika kufanya maamuzi ya kimkakati na kufanikisha maendeleo endelevu ya nchi yetu.

Kwa kutambua umuhimu huo mkubwa katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, uvuvi, usafirishaji na afya. Kwa mfano, wakulima hutegemea utabiri wa hali ya hewa kujua wakati sahihi wa kupanda, kuvuna na kuhifadhi mazao yao. Hali hii husaidia kuongeza uzalishaji na kupunguza hasara zinazoweza kusababishwa na mabadiliko yasiyotabirika ya tabianchi.

Aidha, sekta ya uvuvi na usafirishaji wa majini hunufaika na taarifa hizi kwa kuweza kuepuka hatari zinazoweza kujitokeza kama vile dhoruba kali au mawimbi makubwa. Hii husaidia kulinda maisha ya watu pamoja na mali zao.

Vilevile, taarifa za hali ya hewa husaidia katika kujiandaa na majanga kama mafuriko, ukame na vimbunga, hivyo kupunguza athari zake kwa jamii.

Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ni muhimu kuimarisha mifumo ya utoaji wa taarifa sahihi na kwa wakati. Serikali, taasisi na wadau mbalimbali wanapaswa kushirikiana kuhakikisha kuwa wananchi wanapata elimu na uelewa wa kutosha kuhusu matumizi ya taarifa hizi.

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa

Pia, uwekezaji katika teknolojia za kisasa unahitajika ili kuboresha usahihi wa utabiri wa hali ya hewa jambo ambalo Tanzania imelifanyikazi chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa ujumla, matumizi bora ya taarifa za hali ya hewa ni nguzo muhimu katika kujenga jamii imara, inayoweza kukabiliana na changamoto za mazingira na kuhakikisha ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho.

Akizungumza wakati wa kilele cha Maadhiisho ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani ‘World Meteorological Day -WMD’ ambayo huadhimishwa kila ifikapo Machi 23,  Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (MB), anasema anaungana na jamii ya kimataifa katika kuadhimisha miaka 76 ya kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).

Siku hii ni fursa ya kutambua na kupongeza mchango muhimu unaotolewa na Taasisi za Hali ya Hewa Duniani kote katika kuokoa maisha, mali, na kusaidia kuleta maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.

“Kaulimbiu ya Siku ya Hali ya Hewa Dunia mwaka huu 2026 ni “Pima hali ya hewa leo, ili kesho iwe salama ‘Observing Today, Protecting Tomorrow.” Kaulimbiu hii inasisitiza umuhimu wa ufuatiliaji endelevu wa mifumo ya hali ya hewa na maji na upimaji wa taarifa zake.

Waziri Mbarawa anasema kuwa kwa kuimarisha mifumo hii ya ufuatiliaji na uangazi wa hali ya hewa na maji, nchi nyingi ikiwemo Tanzania, zinajizatiti zaidi kutoa taarifa za tahadhari za mapema hivyo kupunguza athari zinazohusiana na ongezeko la mabadiliko ya hali ya hewa hususan matukio ya hali mbaya ya hewa yanayoongezeka kwa ukubwa na idadi.

“Sote tunafahamu umuhimu wa taarifa sahihi na za wakati za hali ya hewa katika kufanya maamuzi sahihi kwa sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi. Sekta hizi ni pamoja na uchukuzi, kilimo, nishati, maji, afya, miundombinu, ujenzi, madini, na nyingine nyingi zinazohusiana na zinazoathiriwa na hali ya hewa.

“Hata hivyo, mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi yanaendelea kusababisha changamoto kubwa katika sekta hizi kutokana na kuongezeka kwa idadi na ukubwa wa matukio ya hali mbaya ya hewa” anasema Waziri Mbarawa.

Kwa mujibu wa WMO, kati ya mwaka 1970 na 2021, matukio ya hali mbaya ya hewa yamesababisha hasara ya dola za Kimarekani takriban trilioni 4.3 na vifo vipatavyo milioni 2, ambapo zaidi ya asilimia 90 ya vifo hivyo vimetokea katika nchi zinazoendelea, hivyo kuonesha udharura wa kuimarisha miundombinu na mifumo ya ufuatiliaji na uangazi wa hali ya hewa ambayo itasaidia kuimarisha mifumo ya utoaji wa tahadhari za mapema kwa jamii leo na wakati ujao, sambamba na kuongeza uwezo wa wataalamu.

JUHUDI ZA SERIKALI KATIKA UWEKEZAJI WA MIUNDOMBINU

Waziri Mbarawa anasema kuwa uwekezaji katika miundombinu ya hali ya hewa ikiwa ni pamoja na mifumo ya utoaji wa tahadhari za mapema ni uamuzi wa kimkakati ambao Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuufanya.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka juhudi za kipekee katika kuwekeza katika miundombinu na mifumo ya hali ya hewa ili kupunguza pengo katika mtandao wetu wa kitaifa wa uangazii wa hali ya hewa, kuendana na teknolojia za kisasa ikiwemo matumizi ya Akili Mnemba (AI) katika sekta utoaji wa huduma za hali ya hewa.

Jitihada zote hizi zinafanywa kwa lengo la kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi leo na siku zijazo kama ilivyoainishwa katika kaulimbiu ya Siku ya Hali ya Hewa ya mwaka huu. Hivyo, uwekezaji huu katika utoaji wa huduma za hali ya hewa sio mzigo kwa walipa kodi, bali ni uwekezaji katika usalama wa kitaifa, uthabiti wa kiuchumi na ustahimilivu wa muda mrefu kwa taifa letu.

DIRA 205O YATAMBUA HATARI MABADILIKO TABIA NCHI

Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 (Dira 2050) iliyozinduliwa Julai mwaka jana, inatambua mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kama hatari kubwa kwa ukuaji wa uchumi wa muda mrefu, maisha ya watu, na usalama wa kitaifa, na inasisitiza haja ya kujenga ustahimilivu dhidi ya  hali ya hewa hususan mabadiliko ya muda mrefu katika sekta zote.

Kaulimbiu ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa mwaka huu inashabihiana vyema na Dira 2050 na inachangia katika utekelezaji wa nguzo tatu za Dira hiyo, hasa nguzo ya tatu inayohusiana na Uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

Mojawapo ya malengo ya nguzo hii ya tatu ni kujenga Taifa linaloweza kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na linaloweza kulinda watu, miundombinu na mali zake kutokana na majanga ya asili na yale yanayotokana na binadamu, huku vijana na wanawake wakiwekwa mstari wa mbele katika hatua za kukabiliana na mabadiliko haya ya hali ya hewa na tabianchi.

Vilevile, nguzo ya tatu ya Dira inatambua kuwa, mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, yanayoambatana na ongezeko la joto la dunia, mabadiliko ya mifumo ya hali ya hewa, na kuongezeka kwa matukio ya hali mbaya ya hewa, yanatishia maendeleo endelevu ya Tanzania. Na kuwa, athari zake ni kubwa kwa sekta zinazotegemea sana hali ya hewa, ambazo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania.

Kwa kuzingatia haya, kuna haja ya hatua za maksudi kuimarisha uangazi na uchambuzi wa taarifa za hali ya hewa ili taarifa hizi zitumike katika utoaji wa maamuzi sahihi katika sekta mbalimbali kwa jamii kujengewa uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na hivyo kuwa na maendeleo endelevu.

RAIS SAMIA AIMARISHA HUDUMA ZA HALI YA HEWA

Chini ya uongozi mahiri wa Dkt. Samia Serikali imeendelea kuweka kipaumbele katika kuimarisha huduma za hali ya hewa na kuboresha utoaji wa huduma hizi kwa nchi nzima.

Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa taarifa bora za hali ya hewa zinawafikia wananchi katika ngazi zote. Kama nilivyoainishwa hapo awali, uwekezaji mkubwa uliofanywa katika kuboresha miundombinu ya hali ya hewa, ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Uhakiki wa vifaa vya hali ya hewa kinacho endelea kujengwa jijini Dar es Salaam, utaboresha uwezo wetu wa ufuatiliaji na uangazi wa hali ya hewa na hivyo kuongeza usahihi wa taarifa za hali ya hewa.

“Huu ni uthibitisho wa dhati wa adhma ya Tanzania kuimarisha mifumo ya uangazi na ufuatiliaji wa hali ya hewa leo ili kesho yetu iwe salama zaidi kama kaulimbiu ya siku ya hali ya hewa Dunia kwa mwaka huu inavyosema” anasema.

YAIMARISHA USHIRIKIANO NA WMO


Kupitia ushirikiano imara na mzuri na wadau wetu wa maendeleo, ikiwa ni pamoja na Shirika la Hali ya Hewa la Dunia (WMO), Serikali inaendelea kuimarisha mtandao wake wa uangazi  na ufuatiliaji wa taarifa za hali ya hewa kupitia utekelezaji wa programu mbalimbali, ikiwemo programu ya WMO ya uwekezaji katika miundombinu ya hali ya hewa wa  “Systematic Observing Financing Facility (SOFF)” na ile ya kuboresha mpango wa utoaji wa tahadhari za mapema kwa wote yaani  “Early Warning for All (EW4ALL)”.

Programu ya SOFF, inatoa mchango mkubwa kwa kuwekeza vituo tisa (9) vipya vya hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe “Automatic Weather Stations (AWS); vituo vinne (4) vya uangazi wa hali ya hewa ya anga za juu “Upper-Air stations”, pamoja na ukarabati na uboreshaji wa vituo 18 vya AWS na ukarabati wa kituo kimoja (1) cha uangazi wa hali ya hewa ya anga za juu.

SERIKALI YAIPA TANO TMA

Katika kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Dunia 2026, Serikali inapongeza kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Tanzania (TMA) kwa kuendelea kutoa huduma za hali ya hewa zilizoboreshwa, kwa wakati na kwa umakini mkubwa.

“Taarifa za TMA ni muhimu sana katika kuokoa maisha, kulinda mali na kusaidia sekta kuu za uchumi wa nchi yetu. Napenda pia kutoa shukrani za dhati kwa Shirika la Hali ya Hewa la Dunia (WMO) na Washirika wa Maendeleo kwa mchango wao muhimu na mkubwa katika kuimarisha huduma za hali ya hewa nchini Tanzania, hasa katika kuboresha miundombinu ya uangazi na ufuatiliaji wa hali ya hewa na kujenga uwezo wa wataalamu. Ushirikiano wenu ni muhimu sana katika kuongeza ustahimilivu wetu kama Taifa dhidi ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

“Tunapoendelea kuadhimisha siku hii muhimu, natoa rai kwa wadau wote wakiwemo Taasisi za Serikali, Washirika wa Maendeleo, Sekta Binafsi, Taasisi za Elimu, Vyombo vya Habari na Umma kwa ujumla, kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwekeza kwenye mifumo na miundombinu ya uangazi na uchakataji wa taarifa za hali ya hewa nchini.

“Aidha, natoa wito kwa wadau wote kuendelea kutumia ipasavyo taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA na kuzingatia Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019” anasema.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Benedict Chang’a


UJUMBE WA MKURUGENZI MKUU TMA

Dkt. Ladislaus Benedict Chang’a, ni mkurugenzi mkuu wa TMA, lakini pia ni Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), na Makamu Mwenyekiti wa jopo la kimatafa la Sayansi ya mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), TMA inaungana na Jumuiya ya Kimataifa Kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani ikiwa na matumaini makubwa kutokanana uwekezaji mkubwa wa miundombinu uliofanywa na Serikali.

Chang’a, anasema kuwa TMA ina mamlaka ya kitaifa yenye jukumu la kutoa huduma za hali ya hewa kwa umma, taasisi mbalimbali na watumiaji binafsi wa huduma maalum kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, pamoja na kusimamia na kuratibu shughuli za hali ya hewa katika mipaka ya Tanzania na kutoa tahadhari na ushauri kuhusu matukio ya hali mbaya ya hewa kwa lengo la kulinda maisha ya watu na mali zao, inaungana na jumuiya ya hali ya hewa duniani kote kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa mwaka 2026.

“Tanzania ni mojawapo ya nchi wanachama 193 wa WMO, ambapo kupitia TMA inaendelea kuthibitisha dhamira yake thabiti ya kuimarisha huduma za hali ya hewa ambazo ni msingi muhimu wa usalama, ustawi wa jamii na maendeleo endelevu ya taifa.

“Kaulimbiu ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani mwaka huu inalenga kusisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya uangazi wa hali ya hewa na matumizi sahihi ya data za hali ya hewa zinazokusanywa ili kuwezesha maamuzi yenye tija katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi, kusaidia kuongeza uzalishaji, usalama na ustahimilivu wa jamii yetu kwa sasa na kwa vizazi vijavyo” anasema.


Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa wa kimkakati katika huduma za hali ya hewa ambao ni muhimu kwa kuimarisha ustahimilivu wa taifa dhidi ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa ikiwa ni pamoja na tahadhari dhidi ya matukio ya hali mbaya ya hewa yanayoendelea kuongezeka kwa ukubwa na idadi kutokana na mabadiliko haya.

SERIKALI YAWEKEZA MIUNDOMBINU YA HALI YA HEWA

Anasema kuwa serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya hali ya hewa katika mnyororo mzima wa utoaji wa huduma hizi nchini. Miongoni mwa uwekezaji huo ni pamoja na ujenzi unaoendelea wa Jengo la Kanda ya Mashariki ambalo litatumika pia kama Kituo cha Tahadhari za Tsunami; pia ujenzi wa Kituo cha Uhakiki wa Vifaa vya Hali ya Hewa (Instrument Calibration Centre) jijini Dar es Salaam.

Aidha, Serikali imeendelea kuboresha na kuongeza vifaa vya kisasa vya uangazi wa hali ya hewa ili kuimarisha usahihi wa data za hali ya hewa, ufuatiliaji mifumo na utabiri wa hali ya hewa.

MIKOA MITANO YAFUNGWA RADA

Rada ya hali ya hewa Mbeya


Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika uwekezaji katika sekta ya hali ya hewa nchini ni pamoja na uwekaji wa Rada tano (5) za hali ya hewa zilizoko Mwanza, Dar es Salaam, Mtwara, Kigoma na Mbeya kati ya Rada saba (7) zilizopangwa katika mtandao wa kitaifa wa Rada za hali ya hewa.

Serikali imenunua na kufunga vifaa mbalimbali vya kisasa vya hali ya hewa ikiwa ni pamoja na vifaa 10 vya hali ya hewa kwa ajili ya usafiri wa anga (Aviation Meteorological Systems (AVIMET), Vituo 50 vya hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe (Automatic Weather Stations – AWS); Vipima mvua 60 vinavyojiendesha vyenyewe (Automatic rain gauges); Vituo 15 vya kisasa vya hali ya hewa kwa ajili ya huduma za hali ya hewa-kilimo (Agrometeorological AWS).

Serikali pia imewezesha ufungaji wa Kompyuta yenye uwezo mkubwa wa kuchakata taarifa (High Performance Computer – HPC) ambayo imeimarisha sana uchakataji na uchambuzi wa data za hali ya hewa na kuboresha shughuli za utabiri na uandaaji wa taarifa mahsusi za hali ya hewa kwa watumiaji na sekta mbalimbali.

Vilevile, mfumo wa kisasa wa utabiri wa hali ya hewa (forecasting system) umefungwa ili kuimarisha uchakataji wa data na taarifa na kuongeza usahihi wa utabiri wa hali ya hewa hivyo kusaidia kulinda maisha ya watu na kuendeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Vilevile anasema TMA pia imeendelea kushikilia cheti cha ubora cha ISO 9001:2015 katika utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa usafiri wa anga, na hivyo kuendelelea kuthibitisha ubora wa huduma mahususi za hali ya hewa kwa ajili usafiri wa anga.

TMA YATAITAMBULISHA TANZANIA KIMATAIFA

Kwa upande wa ushiriki na mchango wetu kimataifa, TMA imeendelea kuiwakilisha Tanzania ipasavyo katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa ambapo wataalamu 15 wa Tanzania wanahudumu katika vikosi kazi na kamati mbalimbali za Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) pamoja na Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa (IPCC).

Kwa mfano Dkt. Ladislaus Chang’a, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, alichaguliwa mwezi Julai 2023 kuwa Makamu Mwenyekiti wa IPCC kwa kipindi cha miaka saba; Dkt. Pascal Waniha, Mkurugenzi wa Miundombinu na Huduma za Ufundi wa TMA, anahudumu kama Makamu Rais wa Kamisheni ya WMO ya uangazi, miundombinu na ubadilishajaji wa data na taarifa za hali ya hewa (WMO Commission on Observation, Infrastructure, and Information Systems-INFCOM) tangu mwaka 2024.



Pia Dkt. Hamza Kabelwa, Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri, anahudumu kama Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya WMO inayoshughulikia mfumo jumuishi wa WMO wa uchakataji wa taarifa za hali ya hewa na utabiri (WMO Standing Committee on WMO Integrated Processing and Prediction System (SC-WIPPS)) tangu mwaka 2024.

“Ushiriki wa wataalamu hawa katika ngazi na vyombo hivi muhimu vya kimataifa ni kudhihirisha mchango mkubwa wa Tanzania katika kuandaa na kutekeleza kanuni na miongozo ya utoaji wa huduma za hali ya hewa duniani” anasema.

MATUMIZI YA TEKNOLOJIA

Katika juhudi za kuimarisha huduma za hali ya hewa nchini, TMA haijabaki nyuma katika matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo matumizi ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence – AI) ili kuboresha utoaji wa huduma na mifumo ya utoaji wa maamuzi katika sekta mbalimbali nyeti hususan zile zinazoathiriwa sana na hali ya hewa na kwa umma kwa ujumla.

Katika kukabiliana na mabadiliko na maendeleo ya kiteknolojia, wataalamu wa TMA wamebuni mifumo ambayo ni pamoja na; Mfumo wa mawasiliano na ubadilishanaji wa taarifa na data za hali ya hewa kutoka vituo vya hali ya hewa kote nchini na kuzikusanya kwenye kituo kikuu cha utabiri kilichopo Dar es Salaam kabla ya kubadilishana nan chi nyingine duniani ujulikanao kwa jina “Digital Meteorological Observatory (DMO)”, pia mfumo wa ukusanyaji na usambazaji wa taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji wa bahari na maziwa “Marine Meteorological Information System (MMIS)” na mfumo wa mawasiliano ya taarifa za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga “Meteorological Aviation Information System (MAIS)” .

Hata hivyo anaongeza kuwa ubunifu huu umeimarisha uangazi, usimamizi wa data za hali ya hewa, usambazaji wa taarifa hizi na utoaji wa huduma. Juhudi hizi ni utekelezaji wa kazi zetu sambamba na dira ya TMA ya kuwa  “Kitovu bora cha huduma za hali ya hewa kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii”

TMA YATOA USAIDIZI WA KIUFUNDI AFRIKA

Katika Nyanja za Kikanda na Kimataifa, Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Tanzania inaendelea kutoa usaidizi wa kiufundi kwa Taasisi nyingine za Hali ya Hewa za nchi nyingine hususan za barani Afrika katika maeneo muhimu ya sekta hii ya hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa Mfumo wa Usimamizi wa Ubora (Quality Management System-QMS) na Tathmini ya Wataalamu (Competence-based Assessment) na mafunzo kuhusu mifumo ya TMA ya DMO, na MAIS.

Kwa siku za karibuni, TMA imetoa usaidizi wa kiufundi kwa baadhi ya Taasisi za Hali ya Hewa za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kwa kushirikiana na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kupitia programu zake za kikanda barani Afrika.Nchi tulizosaidia ni pamoja na; Burundi na Sudani Kusini,Namibia na Zimbabwe. Matarajio yetu ni TMA kuwa kitovu bora barani Afrika cha kukuza ujuzi na uvumbuzi katika sekta ya hali ya hewa.


Kwa kutambua pia umuhimu wa elimu kwa wataalamu wa hali ya hewa katika kuboresha huduma za tahadhari za hali ya hewa, TMA inasimamia na kuendesha Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa “National Meteorological Training Centre (NMTC)” kilichopo Mkoani Kigoma. Chuo cha NMTC kina ithibati ya NACTE na kina jukumu la kutoa mafunzo kwa wataalamu ikiwa ni pamoja na mafunzo ya uangazi na ufuatiliaji wa mifumo ya hali ya hewa, matumizi ya taarifa za Rada za hali ya hewa, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kwa ngazi za cheti na stashahada.

Mafunzo ya ngazi za juu, kuanzia ngazi ya Shahada ya kwanza hadi Shahada ya Uzamivu, yanapatikana kupitia ushirikiano wa TMA na taasisi za elimu ya juu za kitaifa na kimataifa ikiwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela (NM-AIST) kilichopo Jijini Arusha.

Kifaa cha kisasa cha kupima hali ya hewa kwa ajili ya matumizi ya usafiri wa ndege wakati wa kuruka na kutua, kipo kiwanja cha ndege Mtwara.


KIU YA TMA


Anasisitiza kuhusu dhamira thabiti ya TMA ya kuendelea kuimarisha mifumo ya uangazi wa hali ya hewa kwa kipindi walichonacho ili kuweza kulinda maisha ya watu na mali zao kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi kwa kesho yetu.

“Nachukua fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwekezaji mkubwa wa kuendelea kuimarisha huduma za hali ya hewa hapa nchini. Pia tunaendelea kuwashukuru Wadau mbalimbali wa Maendeleo, wa Kitaifa na Kimataifa, Vyombo vya Habari pamoja na Wafanyakazi wote wa TMA kwa juhudi zao kubwa na mchango wao katika kuendeleza huduma za hali ya hewa kitaifa, kikanda na kimataifa” anasema.