Kikosi cha Simba Kitakachocheza leo dhidi ya Azam

Kikosi cha Azam

ITAKUWA ni vita kali ndani ya Uwanja wa Taifa leo Jumatano saa 10.00 jioni, pale Vinara wa Ligi Kuu barra, Simba SC, itakapokuwa ikipambana na Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC  kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Utamu na ukali wa mchezo huo unaongezwa kutokana na kuhusisha timu mbili zinazofuatana kwa ukaribu kwenye vita ya kuwania taji la ligi hiyo, Azam FC ikiwa katika nafasi ya pili kwa pointi zake 33 huku Simba ikiwa kileleni ikijikusanyia 38.

Wakati Azam FC ikitoka kuichapa Ndanda mabao 3-1 kwenye mchezo uliopita wa raundi ya 16 ya ligi hiyo, Simba nayo imeipiga Ruvu Shooting 3-0, matokeo yanayofanya timu zote hizo mbili kuingia uwanjani zikiwa na morali kubwa.

Ushindi wowote wa Azam FC utaisaidia na kufanya kuzidi kuisogelea zaidi Simba kwenye mbio hizo na kubakisha pengo la pointi mbili, ushindi kwa samba utazidi kuongeza muachano wa pointi na kufikia nane.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, atakayekuwa jukwaani kushuhudia mchezo huo akiendelea kutumikia adhabu ya kukosa mechi tatu baada ya kufungiwa na Bodi ya Ligi (TPLB), ameshaweka wazi kuwa anakiamini kikosi chake kitafanya vizuri na kubeba pointi zote.

Cioaba ameanza kutumikia adhabu hiyo tokea mchezo uliopita Azam FC, ambapo ataimalizia Jumapili hii Azam FC itakapokipiga na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

Nahodha Msaidizi wa Azam FC beki kitasa, Agrey Moris, naye hakuwa nyuma kuwaambia mashabiki wa timu wajitokeze kwa wingi kuwasapoti huku akidai kuwa hawatawaangusha na wamejipanga vema kuipiga Simba.

Na upande wa Simba kupitia kwa Kocha wao  msaidizi, Mrundi, Masoud Djuma amekiri ugumu wa mechi yao ya leo dhidi ya Azam FC, huku akitaja mbinu za ushindi katika mchezo huo ni kuanza kukabia kwenye lango la wapinzani.

Kauli hiyo, aliitoa hivi karibuni mara baada ya mechi dhidi ya Ruvu Shooting kumalizika iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam iliyomalizika kwa Simba kushinda mabao 3-0.

“Kitu cha kwanza tutakachokifanya katika mechi hiyo na Azam ni kutowaruhusu kufika na kucheza kwenye lango letu kwa hofu ya kufanyika makosa, hivyo hatutaki golini kwetu mpira ukae.” “Kingine, tutaingia uwanjani hapo kwa kuanza kuwakabia Azam kwa kuanzia golini kwao kwa maana ya viungo, mawinga na washambuliaji muda wote wanatakiwa kuwepo kwenye goli la wapinzani wetu. “Kama unavyofahamu, mpira ni mchezo wa makosa hivyo tunataka kutumia makosa yao katika mechi hiyo kuwafunga, “ alisema Djuma.

Rekodi

Rekodi zinaonyesha kuwa timu hizo zimekutana mara 19 kwenye mechi za ligi tokea Azam FC ipande mwaka 2008, matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex wakishinda mara tano, Simba wakiibuka kidedea mara nane na ikishuhudiwa mechi sita wakienda sare.

Aidha kwenye mechi za mashindano yote zimekutana mara 28, Azam FC ikishinda mara 10, Simba mara 12 huku mechi sita zikienda sare, hiyo inajumuisha mechi za ligi, Kombe la Mapinduzi, Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup), Kombe la Kagame, Kombe la Ujirani Mwema, Kombe la Banc ABC Super 8 na Ngao ya Jamii.

Kwa msimu huu, hiyo itakuwa ni mara ya tatu kwa timu hizo kukutana, katika mechi mbili zilizopita Azam FC ikishinda mmoja kwenye Mapinduzi Cup bao 1-0, lililofungwa na winga Idd Kipagwile huku ule wa ligi raundi ya kwanza uliofanyika Uwanja wa Azam Complex ukiisha kwa suluhu.

Nahodha wa zamani wa mafanikio wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, aliyehamia Simba msimu huu ndiye kinara wa kufunga mabao mengi kwenye mchezo baina ya timu hizo, akitupia wavuni mara 19 yote akifunga wakati yupo Azam FC, na anatarajiwa kucheza dhidi ya timu yake ya zamani hiyo kwa mara ya tatu msimu huu.

Hadi sasa ikiwa inaelekea raundi ya 17, wachezaji wanne wa Azam FC wamefunga zaidi ya bao moja kwenye ligi, Yahya Zayd na Mbaraka Yusuph, wawili hao wakiwa kileleni ndani ya timu hiyo kila mmoja akifunga matatu huku Shaaban Idd na Paul Peter, nao kila mmoja akifunga mawili.

Simba hadi sasa wachezaji wao wanne wanaoongoza kwa mabao ni Emmanuel Okwi, aliyefunga mabao 12 akiwazidi wachezaji wote VPL, Bocco anafuatia akiwa nayo tisa, huku Asante Kwasi na Shiza Kichuya kila mmoja akiwa nayo sita.

 

TUTAKULETEA LIVE MECHI HII KUPITIA HAPA HAPA JAMHURI MEDIA  WEBSITE

 

 

 

 

Please follow and like us:
Pin Share