Kwa mara nyingine tena naomba nichukue fursa hii kwa niaba ya wasomaji wa makala hii, nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye kwa rehema zake nyingi anatujaalia afya njema na uhai usioweza kulinganishwa na kitu kingine katika dunia tunamoishi. 

Kwa vyovyote vile, uhai na afya njema ni vitu vya msingi. Haya masuala mawili yakichanganyika na kuwapo kwa amani ndani ya nchi yetu; matokeo yake ni kuwapo upendo na furaha tele ndani ya mioyo yetu. Kutokana na kuwapo na hali kama hiyo katika Tanzania, sina budi kumshukuru na kumpa heshima, utukufu na kumwabudu pasipo hofu – Mwenyezi Mungu ambaye kwa mapenzi yake anatujaalia haya yote. 

Kuna usemi wa ‘mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe’. Suala hili ni sawa, lakini bila ya rehema za Mwenyezi Mungu hata hizo nguvu zitakuwa nadharia tu. Kwa maneno mengine, hata kama unao mtaji wa nguvu, bora ukamtanguliza Mwenyezi Mungu kwanza na mengine yakafuata.

Kati ya mambo mazuri na muhimu ambayo Tanzania imebahatika kuwa nayo tangu kuumbwa kwa ulimwengu, ni za rasilimali wanyamapori tulizonazo. Kimsingi, Mwenyezi Mungu ametujaalia tuwe na urithi asilia wa wanyamapori katika hifadhi 16 za Taifa (16 national parks) na mapori 28 ya akiba (28 game reserves). Rasilimali hizo zipo katika maeneo mbalimbali nchini. 

Mathalani, pori kubwa la akiba kuliko yote nchini na pengine Afrika na duniani ni Selous Game Reserve lenye eneo la hekta milioni 5. Liko Kusini mwa Tanzania. Pori hili lilianzishwa mwaka 1920 na wakoloni Waingereza waliokuwa wakiitawala Tanganyika kwa wakati huo. Kwa wale wasioifahamu Tanganyika, hii ndiyo tunayoitaja kama Tanzania Bara kwa muundo na utawala wa sasa baada ya nchi Tanganyika kuungana na Zanzibar, Aprili 26, 1964 na hatimaye kuwa Taifa moja la Tanzania. 

Duniani kuna wanyamapori watano (the big five) wanaotambulika kama wanyama muhimu. Wanyama hao ni Tembo (African Elephant) kitaalamu Loxodanta Africana; Simba (Lion) kitaalamu Panthera leo; Faru (Black Rhinoceros) kitaalamu Diceros bicornis; Chui (Leopard) kitaalamu Panthera pardus; na Nyati (Buffalo) kitaalamu Syncerus cafer cafer. 

Hawa kidunia wanatambulika kama The Big Five. Kwanini wanafahamika hivyo, nadhani ni kwa sababu ya umachachari wao wanapokuwa katika maeneo yao porini. Ukikumbana na mmoja wa wanyamapori hao cha moto utakipata hata kama una bunduki. 

Pamoja na wanyama hao, pia kuna wanyamapori wengine kama kiboko (hippopotamus) kitaalamu Hippopotamus amphibious, Twiga (Giraffe) kitaalamu Giraffe comelopadus (mnyamapori huyu ni nembo maalum ya Taifa letu), Pundamilia (Zebra) kitaalamu Equus burchelli na wanyamaori wengine wazuri katika maeneo ya hifadhi za Taifa pomoja na mapori ya akiba. 

Hata hivyo, mbali na Tanzania kuwa na wanyamapori hao, pia imebahatika kuwa na urithi wa wanyamapori wa namna nyingine wengi na wazuri na wenye umuhimu wa kipekee kama Sokwe (Chimpanzee) ambao kitaalamu huitwa Pan troglodytes-Schweinfurthii. 

Katika Tanzania wanyamapori hawa wanapatikana katika maeneo machache kwenye mikoa ya Katavi na Kigoma. Vilevile, wapo sokwe kama hawa tulionao nchini mwetu, wanaopatikana katika misitu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Sokwe hao hujulikana kama Pan pariscus. Vilevile, wapo Chimpanzee wenye umbo kubwa na hupatikana kwenye misitu minene nchini DRC na Rwanda; na wengi wetu huwafahamu kama Sokwemtu kitaalamu Gorilla gorilla (wa upande wa Magharibi mwa Africa na Gorilla bowingei wanaopatikana upande wa Mashariki hasa nchini Uganda maeneo ya Bwindi. Sokwemtu ni wanyamapori wenye nguvu na wakati mwingine huweza kutembea kwa miguu miwili kama binadamu. 

Kwa upande wa Tanzania, taarifa za utafiti zinaonesha kuwa sokwe walioko Katavi na Kigoma wako hatarini kutoweka. Hii ina maana kuwa kuishi kwao kwa sasa kupo shakani, hasa kutokana na shughuli za kibinadamu katika maeneo yenye misitu ya asili ambayo inategemewa na sokwe kama mhimili mkuu kwa maisha yao ya kila siku.

Desemba, 2015 nilibahatika kutembelea Mkoa wa Katavi ambao ni sehemu zenye misitu ya asili inayotumiwa na sokwe kwa mahitaji yao ya chakula, maji na sehemu za kuishi (Chempanzee’s habitable areas). Wakati nikiwa Mpanda nilihudhuria mkutano muhimu wa wadau wa maeneo ambayo sokwe wanaishi hasa mfumo mzima wa ikolojia kwenye ukanda wa Gombe-Mahale-Katavi ecosystem. 

Maeneo ya Gombe na Mahale ni hifadhi za Taifa kwa ajili ya sokwe; wakati Katavi ni hifadhi ya Taifa yenye mchanganyiko wa wanyamapori wakiwamo tembo. Mkutano huo wa wadau ulifanyika Desemba 17 hadi 18, 2015 mjini Mpanda na ulihudhuriwa karibu na wakuu wa idara zote kutoka katika halmashauri za wilaya za Mpanda, Msimbo (Katavi) pamoja na Kigoma na Uvinza (Kigoma). 

Mkuu wa Mkoa wa Katavi na wakuu wa wilaya hizo akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Mlele na Wakurugenzi Watendaji (DED), walihudhuria mkutano huo na kuchangia mijadala kikamilifu. Mkutano huo ulifanyika kwa uhisani wa taasisi za Jane Goodall Institute (JGI) na Nature Conservancy/TUUNGANE, zenye makao makuu mjini Kigoma kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Mpanda.

Taarifa mbalimbali zilitolewa na viongozi wa idara kutoka wilaya zenye maeneo yenye sokwe ya Msimbo, Mpanda, Uvinza na Kigoma. Vilevile, zilitolewa taarifa kutoka kwa wataalamu na watafiti kuhusu masuala ya sokwe na makazi yao. 

Moja ya taarifa za utafiti uliofanyika kati ya mwaka 2012 na 2014 iliyotolewa na Dk. Alex Piel kutoka Uingereza na washirika wake, hasa wataalamu kutoka TAWIRI na wengine TANAPA na pia kutoka taasisi ya JGI Kigoma, imeonesha kuwa idadi ya sokwe katika Ukanda wa Magharibi mwa Tanzania (Katavi na Kigoma) imekuwa ikipungua mno. Chanzo kikuu cha kupungua huko ni kuharibiwa misitu ya asili.

Taarifa iliyowasilishwa na Dk. Piel ilibainisha kuwa misitu ya asili katika sehemu wanazoishi sokwe Afrika Magharibi na Magharibi mwa Tanzania imekuwa ikitoweka kwa kasi kubwa mno.

Kwa mfano, taarifa ilibainisha kuwa kwenye miaka ya 1900 kulikuwa na sokwe waliokadiriwa kufikia milioni moja. Kwa sasa (mwaka 2015) takwimu zinaonesha kuwa kama wapo wengi, basi ni kati ya 150,000 na 300,000. 

Kwa upande wa Tanzania inakadiriwa kuwa wapo sokwe wasiozidi 2,500 katika hifadhi za Taifa za Gombe na Mahale na kwenye sehemu za Hifadhi ya Taifa ya Katavi. Hata hivyo, taarifa ilibainisha kuwa baadhi ya sokwe wanaishi kwenye maeneo ambayo hayajahifadhiwa ambako kimsingi sokwe wamekuwa wakitumia maeneo hayo kama shoroba. Mfano ni eneo la Milima Wansisi katika Wilaya ya Mpanda. Eneo hilo sasa limebainika kugubikwa na shughuli nyingi za kibinadamu. 

Mathalani, kuongezeka kwa shughuli za kilimo, kuchunga mifugo ambayo ni mingi mno; shughuli za kupasua mbao, kuchoma moto mara kwa mara; kuongezeka makazi ya binadamu; kurina asali na hasa kwa kutumia moto ambao huua nyuki na kusababisha moto ndani ya mapori, kumekuwapo ongezeko la njia za wapitaji na kuongezeka mitego ya kukamata/kuua wanyama (snares) kutokana na wawindaji haramu ambao wamekuwa wakiongezeka kila mwaka. 

Taarifa ilibainisha kuwa uharibifu wa misitu katika eneo la Milima Wansisi umeshamiri mno hasa kati ya mwaka 2007 na 2014 na kusababisha idadi ya sokwe ipungue. Vilevile, kwa kubanwa kwenye eneo dogo na kushindwa kutumia ushoroba huo kwenda maeneo ya Gombe, Mahale na Katavi. Taarifa iliainisha kuwa kutoka na shughuli za kibinadamu kuongezeka kwenye Pori la Masito-Ugalla mkoani Kigoma, idadi ya tembo imepungua mno kiasi cha kusema kuwa sasa wanyama hao hawapatikani kwenye pori hilo.

Sokwe ni wanyamapori muhimu katika nchi yetu. Kwanza, hawapatikani nchi nyingi duniani, isipokuwa katika nchi chache barani Afrika. Pili, kwa Tanzania wanapatikana katika mikoa ya Katavi na Kigoma pekee; tena katika eneo dogo. Kwa mikoa hiyo kuwapo wanyamapori hao ni kama kuwapo vito vyenye thamani sana. Inawezekana kwa sasa wengi wetu hatuoni thamani ya kuwa na wanyamapori hao katika maeneo hayo, lakini kadiri miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege; usafiri wa majini na huduma za hoteli na utalii kwa jumla zinapozidi kuboreshwa na kuimarika, ni dhahiri kwa miaka michache ijayo idadi ya watalii na wageni kutoka nchi mbalimbali itaongezeka na kusababisha kiwango cha mapato katika mikoa ya Katavi, Kigoma na Rukwa kuongezeka.

Hata hivyo, tunapoachia shughuli za kibinadamu zikafanyika holela kwenye maeneo yenye misitu ambayo sokwe wanaitegemea kwa maisha yao, utafika wakati Taifa litawapoteza sokwe wengi na hivyo kuwa katika hali ngumu ya utalii endelevu kwenye mikoa ya Katavi, Kigoma na Rukwa.

 

>>ITAENDELEA

2506 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!