Na Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limeongeza mapato yake kutoka Sh bilioni 1.3 hadi takribani Sh bilioni 147.8 katika mwaka wa fedha 2025/26, mafanikio yanayoelezwa kuchangiwa na mageuzi ya kiutendaji, uwekezaji katika miradi ya madini na kuimarisha usimamizi wa shughuli zake.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. CPA Venance Mwasse, amesema ongezeko hilo limeimarisha uwezo wa shirika kujiendesha na kupunguza utegemezi wa fedha kutoka serikalini.

Amesema awali shirika lilitegemea Serikali kwa takribani asilimia 89 ya mahitaji yake, lakini mageuzi yaliyofanyika yameongeza uwezo wake wa kugharamia mishahara ya watumishi na kuchangia mapato ya Serikali.

Ameeleza kuwa STAMICO iliyoanzishwa mwaka 1972 na inayomilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali, ina jukumu la kushiriki katika mnyororo mzima wa thamani wa madini kwa niaba ya Watanzania, kuanzia utafiti, uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani hadi biashara ya madini.

Kwa mujibu wa Dkt. Mwasse, kuanzishwa kwa shirika hilo kulilenga kuhakikisha Tanzania hainufaiki na ukusanyaji wa kodi pekee kutoka kwa wawekezaji, bali pia inapata manufaa ya moja kwa moja kupitia uwekezaji na uzalishaji wa rasilimali zake.

Amesema ushiriki huo pia unaimarisha uwezo wa Serikali kuelewa changamoto na fursa zilizopo katika sekta ya madini.

Dkt. Mwasse amesema STAMICO imefanya mageuzi makubwa tangu mwaka 2020, yakilenga kubadili fikra na mifumo ya uendeshaji, kuongeza uwekezaji katika miradi yenye uwezo wa kuingiza mapato na kutengeneza ajira kwa Watanzania.

Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kuongezeka kwa idadi ya watumishi kutoka takribani 111 hadi karibu 800. Sambamba na hilo, shirika limepanua shughuli zake za utafiti, uchimbaji na utoaji wa huduma za kitaalamu kwa kampuni zinazofanya shughuli za madini nchini.

Katika kuimarisha miradi ya kimkakati, amesema STAMICO imeingia mikataba minne ya ubia katika miradi inayohusisha madini muhimu, yakiwamo madini ya kimkakati yanayohitajika katika uchumi wa dunia.

Amesema miradi hiyo inalenga kuhakikisha Tanzania inanufaika na fursa zinazotokana na kuongezeka kwa mahitaji ya madini hayo katika soko la dunia.

Ameutaja mradi wa makaa ya mawe wa Kiwira, mkoani Songwe, kuwa miongoni mwa miradi ambayo shirika limeendelea kuifanyia maboresho baada ya kukumbwa na changamoto za uzalishaji.

Amesema maboresho ya mitambo na miundombinu ni sehemu ya juhudi za kuongeza tija na kufufua shughuli za mradi huo.

AWEKEZA KWA WACHIMBAJI WADOGO

Kuhusu kuwawezesha wachimbaji wadogo, Dkt. Mwasse amesema STAMICO imeongeza uwekezaji katika vifaa na huduma za kitaalamu, ikiwamo kuongeza mitambo ya uchorongaji kutoka mitatu hadi 18 na kuweka mitambo 17 kwa ajili ya kusaidia shughuli za wachimbaji wadogo.

Amesema shirika limeendelea kutoa mafunzo na ushauri wa kitaalamu kwa wachimbaji ili kuwasaidia kuboresha mbinu za uzalishaji.

Ameongeza kuwa STAMICO inaendelea kusaidia makundi mbalimbali ya wachimbaji wadogo, wakiwamo wanawake na vijana, kupitia mafunzo, ushauri wa kitaalamu na vifaa.

Ametoa mfano wa kundi la wanawake wachimbaji lililosaidiwa kwa kupewa pampu 10 kati ya 18 walizoomba ili kukabiliana na changamoto ya maji katika maeneo yao ya uchimbaji.

MASOKO 44, VITUO 120 VYA UNUNUZI WA MADINI

Akijibu maswali ya wahariri kuhusu masoko ya madini, amesema STAMICO ina mtandao wa masoko 44 na vituo vidogo vya ununuzi wa madini takribani 120.

Amesema miundombinu hiyo imesaidia kurahisisha upatikanaji wa maeneo rasmi ya kuuza madini kwa wachimbaji na wafanyabiashara, huku ikisaidia kupunguza mianya ya utoroshaji wa madini na kuongeza mapato yanayokusanywa nchini.

Kuhusu upatikanaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo, amesema shirika linaendelea kushughulikia changamoto za mitaji.

Ameeleza kuwa mchakato wa kuanzisha Benki ya Wachimbaji Tanzania umeanza kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo, ukiwa na lengo la kuongeza upatikanaji wa fedha na kuwezesha Watanzania wengi zaidi kushiriki katika shughuli za uchimbaji.

Aidha, amesema STAMICO inaendelea kushiriki katika miradi ya ubia kwa kuchangia leseni na utafiti wa awali, huku washirika wakitoa mtaji na teknolojia. Faida na manufaa ya miradi hiyo hugawanywa kwa mujibu wa makubaliano ya wahusika.

Amekazia kuwa STAMICO ni mwekezaji katika sekta ya madini, si mdhibiti, jukumu ambalo linatekelezwa na taasisi husika za Serikali.

TEF YATAKA UTAFITI, TAKWIMU ZA KISASA

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema mafanikio ya STAMICO yanaonyesha kuwa taasisi za umma zinaweza kuimarika na kuongeza tija zinapotekeleza mageuzi na kusimamia rasilimali kwa ufanisi.

Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa shirika kuimarisha utafiti na ukusanyaji wa takwimu za kisasa ili mafanikio yake yaweze kupimwa kwa kutumia taarifa sahihi na za wakati.

Balile amewataka wahariri kuendelea kufuatilia miradi ya madini na kuelimisha umma kuhusu mchango wake katika uchumi wa taifa.