Mwanambuzi alikwenda mtoni kunywa maji. Akiwa anakunywa maji, alitokea mbwamwitu naye alikwenda kunywa maji. Mbwamwitu alisimama hatua chache kutoka aliposimama mwanambuzi. 

Mbwamwitu alitamani sana kumla mwanambuzi. Alifikiri mbinu za kumkamata asimkimbie. Wakati anafikiri hivyo, mwanambuzi alikwisha kubaini janja ya mbwamwitu. Alijiweka tayari kumkwepa na kumkimbia. 

Mara mbwamwitu akanena: “Wee mtoto mbona hauna adabu? Unatibua maji wakati nakunywa.” Mwanambuzi akajibu: “Mzee wangu, nawezaje kutibua maji ikiwa wewe ndiye wa kwanza kunywa kabla yangu? Kwa maana mto unatokea kwako kuja kwangu. Labda wewe ndiye unayetibua maji.” 

Mbwamwitu alipoona janja yake imeshindwa akasema: “Wewe ulinitusi mwaka jana, nilikuwa nakutafuta.” Mwanambuzi akamjibu: “Mzee wangu, mbona mwaka jana nilikuwa bado kuzaliwa?” Mbwamwitu akaendelea kuhoji: “Kama si wewe ni baba yako au mjomba wako.”

Mwanambuzi akasema: “Vipi suala la baba au mjomba wangu linanihusu mimi? Ni busara uwatafute wao.” Majibu haya yalimghadhabisha sana mbwamwitu. Alipojiandaa kumvamia, mwanambuzi zamani amekimbia.

Ukitafakari hadithi hii utaona zipo hila katika mazungumzo ya wanyama hawa. Mbwamwitu alitoa hila zake kwa nia ya kumtia hofu na kuwa na woga mwanambuzi ashindwe kukimbia na kujisalimisha asiliwe. Mbwamwitu alijizatiti kuondoa uhai wa mwanambuzi ili yeye afaidike na mlo mnono na kumpatia shibe.

Hila kama hizi hazitungwi na wanyama tu, hata wanadamu hutunga hila mbalimbali kupitia ‘hoja ya nguvu’ kuzipachika ndani ya mstari wa demokrasia ya kweli unaobeba utii wa sheria na utawala bora. Ni juu ya wanadamu kuchambua asili ya hoja zinazotolewa ima na wanasiasa au wanaharakati. 

Mwanambuzi asingechambua hila zilizotolewa na mbwamwitu, na asinge tumia subira na angejaza akilini mwake hofu zitokanazo na hila za mbwamwitu, ukweli angeliwa na kupoteza uhai wake. Mwanambuzi alitumia uwezo na ujasiri kutoa majawabu yenye ‘nguvu ya hoja’. Akanusurika. 

Sipingi uwepo wa demokrasia ya sheria na utawala bora. Hasha! Napinga hila zinazotungwa na kupachikwa katika demokrasia na baadhi ya wanasiasa na wanaharakati wachache wanaohalalisha HOJA ZA NGUVU na kuzipa umaarufu na kuzibeza NGUVU ZA HOJA mbele ya wanadamu. 

Leo katika Serikali ya Awamu ya Tano ndani ya miaka mitatu imetoa majibu ya ukweli na uwazi katika kero zilizosakama serikali za awamu zilizopita juu ya nidhamu kazini, utii wa sheria, utawala bora, uwajibikaji, utekelezaji bora wa huduma za jamii na ujenzi wa miundombinu mbalimbali kama vile reli, anga, barabara, nishati na majengo. 

Dhamira ya serikali ni kuleta maendeleo ya wananchi kwa maana ya kuwainua kiuchumi wakulima na wafanyakazi katika ujenzi wa viwanda na kuelekea kwenye uchumi wa kati. Kila siku wataalamu wa uchumi wa ndani na nje ya nchi wanatudhihirishia ukuaji wa uchumi wetu.

Macho yetu yanaona na masikio yetu yanasikia kuhusu maendeleo ya uchumi na jamii yanavyosonga mbele. Ukweli upo hadharani. Cha kusikitisha, kina lila na fila wanachomoka na hila zao za shari za kuzubaisha kukua uchumi na kuua maendeleo, kama yale ya mbwamwitu kutaka kuangamiza uhai wa mwanambuzi. 

Ni kweli, mifuko ya wananchi bado kunona. Lakini subira ina heri. Kuimarishwa miundombinu ya uchumi na huduma bora za jamii, kuchapa kazi kwa ari kila mtu, kutii sheria na utawala bora ni kuipa rutuba mifuko inone. Tibabu la uchumi wetu limo mikononi mwako. Anza tiba sasa. 

Please follow and like us:
Pin Share