Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, limedai serikali ya Sudan imekuwa ikitumia silaha za kemikali dhidi ya raia wake katika eneo la Darfur na kusababisha vifo vya watoto 200 na kuacha watu wengine kadhaa katika hali mbaya tangu Januari mwaka huu.

Shirika hilo linasema utafiti uliofanyika katika kipindi cha miezi minane umegundua kuwa  serikali ilitumia mbinu za kuteketeza kila kitu, kubaka, kuua na kurusha mabomu eneo la Jebel Marra, Darfur.

Mkurugenzi wa utafiti wa shirika hilo, Tirana Hassan, anasema mashambulio ambayo yamekuwa yakitekelezwa na serikali ya Sudan dhidi ya raia wake, yanaonesha hakuna chochote kilichobadilika licha ya juhudi za kimataifa za kurejesha amani katika eneo hilo.

Anasema katika utafiti huo, watafiti walipata watu 56 wanaosema walishuhudia silaha za kemikali zikitumiwa zaidi ya mara 30 na wanajeshi wa Sudan, ambao walianza operesheni ya kijeshi dhidi ya waasi wa Sudan Liberation Army, wanaoongozwa na Abdul Wahid (SLA/AW) katikati ya mwezi Januari.

Anasema walionusurika wameliambia Shirika la Amnesty International kwamba moshi na harufu isiyo ya kawaida, vilitanda angani baada ya mabomu kurushwa na kuacha mamia ya watu wakipoteza maisha huku wengine wakiwa katika hali mbaya.

Mkurugenzi wa utafiti wa migogoro wa shirika hilo, Tirana Hassan, anasema matumizi ya silaha za sumu ni uhalifu wa kivita  na kuongeza kuwa wakati wa mashambulizi haya, mamia ya raia walipigwa risasi, maelfu walipoteza makazi.

Anasema serikali ya Sudan imefanya mashambulizi 30 yanayoshukiwa kuwa ya silaha za sumu katika eneo la Jebel Marra, jimboni Darfur tangu Januari mwaka huu ikitumia kile wataalamu wanachosema ni kemikali za kusababisha malengelenge.

Hassan anasema inakadiriwa kuwa karibu watu 250 huenda walifariki kutokana na silaha za kemikali na kuongeza kuwa shambulizi la karibuni kabisa lilifanyika Septemba 9 na Amnesty imesema uchunguzi wake ulizingatia picha za satelaiti, mahojiano na zaidi ya watu 200 na wataalamu kuchunguza picha zilizoonesha majeraha.

Omer Dahab Fadi, Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa,  anasema katika taarifa yake  kuwa ripoti hiyo ya Amnesty haina msingi na  kuwa Sudan haimiliki aina yoyote ya silaha za sumu na kuongeza kuwa shirika hilo limesema uongo.

Jeshi la kulinda amani la Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa, linalofahamika kama UNAMID, limekuwa Darfur tangu mwaka wa 2007 pamoja na uwepo wake lakini usalama bado ni tete jimboni humo, ambapo makabila yasiyo ya Waarabu yanapigana na serikali ya Khartoum inayoongozwa na Waarabu.

Kutokana na hali hiyo, kati ya mwaka 2009 na 2010 Mahakama ya kimataifa ya jinai ilitoa waranti wa kukamatwa Rais wa Sudan, Omar Hassan al Bashir,  kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na mauaji ya halaiki kutokana na operesheni yake ya kuangamiza uasi wa Darfur.

By Jamhuri