Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Tanzania imefikia hatua muhimu ya kupanga mustakabali wake wa muda mrefu baada ya kukamilika kwa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ambayo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Julai 17, 2025, jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari tarehe 15 Julai 2025, Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Fred Msemwa, amesema mchakato wa uandaaji wa Dira hiyo umechukua takribani miaka miwili, na umezingatia ushirikishwaji mpana wa wananchi kutoka makundi mbalimbali ya kijamii, kitaaluma na sekta binafsi.

“Katika hatua hii ya kihistoria, zaidi ya Watanzania milioni 1.174 walishiriki kwa kutoa maoni yao kupitia njia mbalimbali za mawasiliano, huku takribani wananchi 20,000 wakihudhuria makongamano ya kitaifa yaliyolenga kukusanya maoni ya moja kwa moja kuhusu mustakabali wa maendeleo ya Taifa,” amesema Dkt. Msemwa.

Amefafanua kuwa mchakato huo umeambatana na uchambuzi wa mifumo ya maendeleo ya kimataifa, ambapo Tanzania ilijifunza kutoka kwa mataifa yaliyofanikiwa kufikia uchumi wa kati kwa njia endelevu, ili kuhakikisha dira mpya inatokana na maarifa ya ndani na nje.

Dkt. Msemwa ameeleza kuwa Rasimu ya Dira ya 2050 ilirudishwa kwa wananchi kwa ajili ya uhakiki wa maudhui, ili kuhakikisha kuwa maoni yao yamezingatiwa kikamilifu. Baada ya hatua hiyo, nyaraka hiyo iliwasilishwa pia kwa wadau kutoka sekta binafsi, asasi za kiraia, taasisi za elimu ya juu na makundi ya kijamii, ikiwa ni sehemu ya kujenga umiliki wa kitaifa wa mwelekeo wa maendeleo.

“Dira hii si nyaraka ya kitaalamu pekee, bali ni mwongozo wa matumaini na maamuzi ya pamoja ya Watanzania kuhusu namna tunavyotaka Taifa letu lionekane ifikapo mwaka 2050,” aliongeza.

Kwa mujibu wa Dkt. Msemwa, utekelezaji rasmi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 utaanza Julai 2026, mara baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa Dira ya sasa ya Maendeleo ya 2025. Tume ya Taifa ya Mipango itaendelea kusimamia utekelezaji huo ili kuhakikisha maendeleo yanakuwa shirikishi, jumuishi na endelevu kwa Watanzania wote.

Dira ya 2050 inatarajiwa kuwa nyenzo kuu ya kuongoza sera, mipango ya muda wa kati na mfupi, na programu mbalimbali za maendeleo katika ngazi ya kitaifa na kimataifa, sambamba na kuwa chombo cha kutathmini mafanikio ya Taifa katika kufikia ndoto ya kuwa nchi yenye uchumi imara, jamii yenye ustawi na Taifa lenye mshikamano.