Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Morogoro imebaini utekelezaji hafifu usiokidhi viwango miradi 12 ya maendeleo ikiwemo ujenzi, afya na elimu yenye thamani ya Sh bilioni 1.26.
Mkuu wa TAKUKURU mkoa huo ,Pilly Mwakasege amesema hayo kupitia taarifa yake kwa waandishi wa habari ambayo iliyosomwa kwa niaba yake na mkuu wa kitengo cha elimu kwa umma mkoa, Bigambo Thomas Bigambo.
Mkuu wa Kitendo cha Elimu kwa Umma wa Taasisi hiyo amesema TAKUKURU ilifanya utuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo 26 inayohusu elimu, maji barabara na afya yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 28. 432.
Amesema lengo la ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi hiyo ni kuweza kubaini viashiria vinavyoweza kusababisha upotevu wa rasilimali za umma ikiwa na kujiridhisha na thamani ya fedha hizo.
“ Miradi hii 12 iliyobainika kuwa na utekelezaji hafifu ambapo ushauri ulitolewa ili mirad hiyo iweze kukamilika kwa wakati “ amesema Bigambo.
Katika hatua nyingine amesema Ofisi Takukuru mkoa kwa kushirikiana na wataalamu wa Ofisi ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ilifanya ukaguzi wa maeneo yote ya wazi yaliyovamiwa na kuendelezwa na wawekezaji.
Bigambo amesema katika zoezi hilo ilifanyika tathimini ya kina kuhusu uwekezaji uliofanyika katika maeneo haya ili kubaini kiasi cha upotevu wa fedha za mapato .
Mkuu wa Kitendo cha elimu kwa umma wa Taasisi hiyo mkoa amesema katika kuhakikisha mapato ya Serikali hayapotei, Takukuru kwa kushirikiana na halmashauri ya Manispaa ya Morogoro imefanikisha kuingiwa kwa makubaliano na mwekezaji SM Holding Msamvu.
Makubaliano hayo ni katika kukusanya kodi itokanayo na maduka yaliyojengwa na mwekezaji huyo katika eneo la Msamvu kiwanja namba 11 na 12 bila kufuata Sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya mipango miji.
Bigambo amesema kutokana na jitihada hizo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro imeanza kupata mapato kiasi cha sh milioni 26.3 kwa mwaka ambapo awali yalikuwa hayakusanywi.
Amesema kuwa mapato hayo yatakusanywa kwa kipindi cha miaka kumi kama ilivyoainishwa katika mkataba wao wa upangishahi na kwamba Halmashauri ya Manispaa hiyo itapata jumla ya Sh milioni 263.5 kwa mujibu mkataba ulivyoingiwa.
Bigambo amesema baada ya muda wa miaka kumi wa mkataba kati ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na SM Holding Msamvu utakapokoma ,maduka hayo yatakuwa ni mali ya Halmashauri ya Manispaa hiyo.
Mkuu wa Kitendo cha elimu kwa umma wa Taasisi hiyo mkoa amesema kuwa ufatiliaji huo ni endelevu katika maeneo yote ya wazi yaliyoko ndani ya Manispaa ya Morogoro ili kuwezesha matumizi sahihi ya ardhi na ukusanyaji wa mapato kutokana na maeneo yanayomilikiwa na Halmashauri hiyo.
