Na Benny Kingson, JamhuriMedia, Tabora

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Tabora imekamata mali za wakulima wa zao la tumbaku zenye thamani ya sh bil 1.4 zilizokuwa zimeibiwa na wafanyabiashara katika vyama vya msingi vya wakulima.

Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Taasisi hiyo Mkoani hapa Azza Mtaita alipokuwa akiongea na gazeti hili katika Ofisi za Taasisi hiyo ambapo ameeleza kuwa mali hizo zimekamatwa katika operesheni maalumu waliyofanya.

Alibainisha mali zilizokamatwa kuwa ni mabelo ya magunia ya kufungashia zao hilo yajulikanayo kama majafafa ambayo ni mali halali ya wakulima, jumla ya magunia 2,681 yenye thamani ya sh bil 1.4 yamekamatwa katika maeneo tofauti.

Kamanda Mtaita alifafanua kuwa magunia hayo yamekamatwa kutoka kwa wafanyabiashara baada ya kukutwa wakiyauza kinyume na utaratibu huku wakijua fika kuwa ni mali halali ya wakulima kwa sababu waliyanunua msimu uliopita.

Mbali na kukamatwa mali hizo pia wafanyabiashara 7 waliokuwa wakiziuza walikamatwa na kufikishwa mahakamani ili kujibu tuhuma zinazowakabili, wakati kesi ikiendelea baadhi yao waliomba kufanya makubaliano ya kulipa fidia (fedha).

‘Utaratibu huu wa makubaliano (plea bargaining) ya kulipa fidia ya hasara kwa wakulima umesaidia kuokoa kiasi cha sh mil 2 na kurejeshewa magunia yao ili wayatumie kufungashia tumbaku yao msimu ujao’, alisema.

Alibainisha kuwa baada ya makubalinao hayo na kulipwa fidia ya hasara kwa serikali, walifanikiwa kurejesha jumla ya magunia 1,315 yaliyotumika msimu uliopita kati ya 2,681 yaliyokamatwa.

‘Wakulima wanaponunua magunia ya kufungashia tumbaku yanakuwa mali yao, kampuni yoyote inayoingia mkataba wa kununua tumbaku inapaswa kuyarejesha kwa wakulima ili yatumike msimu mwingine na sio kuwauzia tena’, aliasa.

Kamanda Mtaita alitaja wakulima waliorejeshewa magunia hayo kuwa ni wa kutoka vyama vya msingi (Amcos) za Mulokhu, Mkombozi, Ikobelo na Kasisi, taratibu za ufuatiliaji zinaendelea ili kuhakikisha magunia yaliyosalia yanarejeshwa kwa wakulima kupitia vyama vyao vya msingi.