Na Mohamed Said, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wiki iliyopita imekuwa ya ajabu sana kwangu. Ubongo wangu umekuwa ukishughulishwa na kumbukumbu za watu na mambo mengi ya nyuma nikiwa mtoto mdogo, sijafikia hata umri wa miaka 15 na sijui kwa nini?

Hujiambia mwenyewe kimya kimya ndani ya nafsi yangu kuwa huenda ni utu uzima nilionao na kuzungukwa na mengi ya udogo wangu. Naweza kuyaona maisha yangu na picha za rafiki zangu wengine marehemu na wengine wako hai kwenye kompyuta yangu kwa kubonyeza tu, basi.

Siku kama tatu zilizopita rafiki yangu mmoja alinirushia picha ya Mzee Mustafa Songambele akiwa anasherehekea miaka 100 ya umri wake na akataka kujua kama ninamfahamu na kutaka kujua mchango wake katika kupigania uhuru wa Tanganyika.

Nina mtindo wangu wa kujibu maswali kama haya na nia hasa ni kutaka kumshtua muulizaji. Nilichofanya sikumjibu swali lake ila nilimrushia picha ya Mzee Songambele kutoka maktaba niliyompiga mwenyewe mwaka 2016. Kama nilivyotarajia aliyeniuliza kama namjua Mzee Songambele alishtuka.

Picha hii nilimpiga wakati wa sherehe za uzinduzi wa nyumba aliyokuwa akiishi ya Mwalimu Julius Nyerere wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika, Mtaa wa Ifunda, Magomeni Mikumi baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa. Shughuli hii ilisimamiwa na Makongoro Nyerere.

Nilialikwa katika shughuli ile pamoja na Mzee Songambele, Mzee Joseph Butiku, Profesa Issa Shivji na Dk. Ng’wanza Kamata na watu wengine wengi. Katika hafla ile, Mzee Songambele alizungumza na kutueleza vipi alijuana na Mwalimu na uhusiano wao.

Nakumbuka siku ile alipozungumza pale yalipokuwa makazi ya Mwalimu alisema kwa furaha kuwa yeye alipata kuwa ‘Justice of Peace,’ katika mji wa Dar es Salaam.

Alituchekesha alipotupa kisa kuwa siku moja alipokea salamu kuwa Mwalimu anamtaka aende Msasani. Anasema yeye hakuenda na hakutoa udhuru, akabana kimya nyumbani kwake akiwa anasikiliza nini Mwalimu atafanya.

Mzee Songambele anasema siku zile Mwalimu alikuwa ana kawaida ya kuweka watu kizuizini, yeye hakuwa na njia ya kufahamu kama mwito ule ulikuwa wa heri au wa shari. Sote tuliangua kicheko. Mzee Songamebele siku ile ndipo nilipomjua kuwa ni mtu wa bashasha.

Namkumbuka wakati alipokuwa Regional Commissioner wa Jimbo la Mashariki (Eastern Province), ikiwa utapenda alipokuwa Regional Commissioner (RC) wa Dar es Salaam, Mji Mkuu wa Tanganyika, nafasi aliyoichukua kutoka kwa Abbas Sykes aliyekuwa RC wa kwanza baada ya uhuru.

Nilimfahamu Mzee Songambele kupitia shangazi yangu Habiba binti Abdallah Simba, ambaye yeye Mzee Songambele alikuwa dada yake.

Bi Habiba ni mtoto wa Liwali wa Songea, Sheikh Abdallah Simba, aliyekuwa rafiki mkubwa wa babu yangu, Salum Abdallah na babu yangu alipanga nyumba yake Mtaa wa Kipata katika miaka ya 1930.

Nyumba hii ikielekezana na nyumba ya Kleist Sykes. Baba yangu na nduguze walilelewa katika nyumba hii na hivi ndivyo baba yangu alijuana na Bi. Habiba katika utoto wao.

Hivi ndivyo nikamtakidi Bi. Habiba kama shangazi na haya ndiyo yalikuwa malezi ya nyakati zile. Haikuwa lazima udugu uwe na damu na Bi. Habiba alimtakidi baba yangu kama kaka yake.

Napata fahamu zangu namuona Habiba wakati huo ni ‘nurse’ Princes Margret Hospital, sasa Hospitali ya Muhimbili na mdogo wake Mwajuma akisoma St Joseph’s Convent School pamoja na Happy Mtamila, mtoto wa Clement Mtamila – mmoja wa viongozi wa TAA na TANU. Shule hii ilikuwa moja ya shule bora Dar es Salaam.

Mwajuma akaja kuolewa na Mponji, aliyepata kuwa waziri katika serikali ya Mwalimu Nyerere.

Sheikh Abdallah Simba alikuwa pia na nyumba nyingine Mtaa wa Somali No. 22, jirani na nyumba ya mmoja wa wazee wa TANU, Mzee Omari Londo.

Nyumba ya Liwali Abdallah Simba pale Mtaa wa Somali ilikuwa nzuri na sifa Gerezani. Habiba aliishi katika nyumba na baba yangu akaja kuwa mpangaji wake.

Mzee Songambele alikuwa akija katika nyumba hii Mtaa wa Somali No. 22 kumsalimia dada yake Bi. Habiba na hivi ndivyo nilivyomfahamu Mzee Songambele. Miaka hiyo alikuwa kijana na nakumbuka alikuwa akija na gari lake Peugeot, gari maarufu miaka hiyo.

Nakumbuka ulikuwa mwaka 1964. Kulikuwa na kipindi TBC kikirushwa Jumamosi mchana kikiitwa, ‘Chipukizi Club.’ Kipindi hiki kilichukua jina lake kutoka kwa vijana wadogo wa Dar es Salaam waliokuwa katika kipindi hiki wakiimba na kupiga muziki wa Kizungu, wakishirikiana na vijana wa Kigoa waliokuwa na bendi yao, ‘The Blue Diamonds.’ Hawa Chipukizi walikuwa vijana wa mjini Dar es Salaam, wengi wao kutokea Kariakoo: Henin Seif, Raymond Chihota, Hussein Shebe, Badrin Abdallah, Abdul Nanji, Salim Hirizi (Sammy Davis), Cuthbert Sabuni, Mariam Zialor, Sauda Mohamed kwa kuwataja wachache.

Kundi hili na kipindi hiki cha muziki tulivipenda. Hizi zilikuwa enzi za Elvis Presley, Cliff Richard, Ray Charles, The Beatles, Rolling Stones, Helen Shapiro, Connie Francis.

Muziki wa wasanii hawa tukiusikiliza ukipigwa katika radio na Chipukizi ulitutia wazimu. Kipindi hiki kilikuwa kikifunguliwa na wimbo unaitwa, ‘Here We Go Looby Loo.’ Mdundo wa wimbo huu peke yake ukitutia wazimu kabla hata hatujawasikia Chipukizi wenyewe na ‘The Blue Diamonds.’

Kipindi hiki tulikipenda kupita kiasi na ikifika Jumamosi mchana sote tulikuwa pembeni ya redio tukimsikiliza Raymond Chihota (licha ya kuwa Chipukizi alikuwa pia mtangazaji wa TBC), akifungua kipindi kwa kuwajulisha akina Hussein Shebe na wenzake wakiimba nyimbo hizo za Ulaya na Marekani.

Hii ilikuwa miaka ya mwanzo ya Tanganyika kupata uhuru na nchi ilikuwa katika kujivua mabaki ya ukoloni. Chipukizi Club ikaonekana na baadhi ya wazee wa Dar es Salaam kuwa ilikuwa inajenga utamaduni mgeni, usiopendeza na uliogusa maadili ya kizalendo.

Regional Commissioner Mustafa Songambele na yeye pia hakufurahishwa na mwenendo wa vijana hawa wa Chipukizi Club. Akaamua kukipiga marufuku kipindi hiki.

Hapa nataka kuongeza kitu. Kama nilivyosema mwanzo kuwa juma hili kichwa changu kimekuwa kikihangaishwa na kumbukumbu nyingi za nyuma.

Juzi tu hapa rafiki yangu amenirushia picha iliyonitia simanzi. Picha hii ni ya vijana kutoka Zanzibar imepigwa mwaka wa 1963, miezi michache kabla ya uhuru wa Zanzibar.

Vijana hawa wakijiita, ‘The Swinging Kids.’ Hawa vijana walikuwa mfano wa Chipukizi iliyokuwa Dar es Salaam na wengi wakifahamiana.

Kisa kilekile cha ‘birds of a feather flock together.’ Wao pia walikuwa katika muziki wa Kizungu ndani ya Zanzibar na wakifanya maonyesho. Kama Chipukizi ilivyotia wazimu vijana wa Dar es Salaam, halikadhalika na Zanzibar ilikuwa hivyo pia.

Baadhi ya vijana hawa kama ilivyokuwa vijana wa Chipukizi Club tulikuja kufahamiana kwa karibu sana ukubwani. ‘The Swinging Kids,’ walikuwa: Muhammad Yusuf (Black), Yusuf Himidi, Ahmed Juma, Mohamed Abdalla Thani, Abdillahi Alifoum, Mussa Khamis Mussa (Baucha), Amiin Ali Moumin (Mziwani), Jamaluddin Omar (Dini) (Bob Dean) na Suleiman Kid.

Vijana hawa wadogo walikuja kufanya makubwa ukubwani wakaitumikia Zanzibar ndani na nje ya mipaka yake baada ya mapinduzi ya mwaka 1964. Kama ilivyo kwa Chipukizi wengi wao wameshatangulia mbele ya haki.

Kwa bahati marufuku ya Mzee Songambele kwa Chipukizi Club haikufika Zanzibar kwa ‘The Swinging Kids.’ Miaka ikapita halikadhalika na ujana wetu pia.

Nakumbuka mara ya mwisho kukutana na Bob Dean ilikuwa Ijumaa Masjid Jibril, Zanzibar. Msikiti ndani umejaa ikabidi tuswali nje kwenye jua kali na mara ya mwisho kukutana na Thani ilikuwa Makka nje ya Haram, nimemkuta kakaa chini nje ya Post Office. Sote tulikuwa tumekwenda Umra. Thani alikuwa ametokea Dubai alikohamia miaka mingi. Sote tulikuwa sasa watu wazima.

Turejee kwa Mzee Songambele. Kiasi cha kama miaka miwili iliyopita rafiki yangu Dk. Harith Ghassany alinipigia simu akaniomba nimfanyie miadi ili akutane na Mzee Songambele.

Nikampigia simu Mzee Songambele nikamuomba tuonane na akanikubalia na akanikaribisha nyumbani kwake. Nikamfikishia salamu za Dk. Ghassany.

Baada ya kusikia kifo chake nasikitika kuwa kwa nini sikuchukua nafasi ile nilipokutana na Mzee Songambele nyumbani kwake sikumuuliza historia yake.

Hakika na kwa kweli nasikitika. Sikuwa nafahamu kuwa Mzee Songambele kadi yake ya TANU ni No. 27. Kadi hii ya TANU ya Mzee Songambele inanikumbusha kadi nyingine za TANU katika mlolongo wa kadi hizi za namba ‘20’, mfano kama kadi ya Idd Faiz Mafungo aliyekuwa na kadi ya TANU No. 24 na kadi ya TANU No. 25 ya Idd Tosiri. Hawa walikuwa wanachama wa mwanzo wa TANU.

Dk. Ghassany alipokuja Dar es Salaam nilimsindikiza kwenda kuonana na Mzee Songambele. Nilibakia nje ndani ya gari. Dk. Ghassany alikuwa amekuja Dar es Salaam mahsusi kwa ajili ya mahojiano na Mzee Songambele kwani alikuwa katika utafiti wa historia ya Tanzania na alifahamishwa kuwa kwa taarifa alizokuwa anatafuta mtu sahihi wa kuzungumza naye ni Mzee Mustafa Songamebele.

Niliamua kubakia nje kwa sababu nilitaka kuwapa faragha wawili hawa wafanye mazungumzo yao kwa utulivu, wawe watu wawili peke yao bila mtu wa tatu pembeni kuwasikiliza.

Napenda kuhitimisha kumbukumbu zangu za nyakati za Mzee Songambele kwa kisa alichonihadithia Mzee Kitwana Kondo.

Kisa hiki nilikisadikisha na kisa kingine alichonieleza Abbas Sykes vilevile kuhusu Mzee Songambele. Abbas Sykes aliniambia kuwa wakati wao walipokuwa watumishi wa serikali, Songambele alikuwa karibu sana na Mwalimu Nyerere na Mzee Rashid Kawawa.

Kwa namna fulani ikawa usuhuba ule na wakubwa hawa wawili waliokuwa juu kileleni katika serikali yeye akiutumia kwa kusukuma utekelezaji wake wa majukumu yake kama RC wa Dar es Salaam. Hili likiwakwaruza baadhi ya watendaji wenzake wa serikali. Lakini hawakuwa na la kufanya.

Mzee Kondo siku moja na yeye akanipa kisa kingine, anasema Mwalimu Nyerere baada ya Azimio la Arusha alitaifisha nyumba nyingi za Wahindi na baadhi za Waafrika kama sehemu ya sera ya siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Songambele nyumba yake ikataifishwa pamoja na nyumba nyingi za viongozi wa serikali. Miaka ikapita na viongozi hawa waliotaifishiwa nyumba zao baada ya kustaafu hali zao zikawa ngumu na wakatamani kama wangerejeshewa nyumba zao zilizotaifishwa ziwasaidie katika maisha yao ya kustaafu.

Rais Mwinyi aliposikia shida walizokuwanazo hawa wastaafu wa serikali aliwaonea huruma na akaamua kuwarejeshea nyumba zao.

Rais Mwinyi akiwa sasa rais wa Tanzania akawa anarejesha nyumba moja moja kwa wenyewe ziwasaidie katika siku zao za mwisho.

Kama Songambele alivyokuwa karibu na Nyerere, Kitwana Kondo na yeye alikuwa karibu sana na Rais Mwinyi. Akiwa kwao Songea, Mzee Songambele akapata taarifa kuwa Rais Mwinyi anarejesha nyumba zilizotaifishwa na mtangulizi wake, Mwalimu Julius Nyerere.

Mzee Songambele akaja Dar es Salaam kwa haraka kufuatilia nyumba yake lakini hajui vipi atafikisha suala lake kwa Rais Mwinyi.

Jamaa wakamwambia aende kwa Kitwana Kondo atamsaidia kumfikisha kwa Rais Mwinyi. Songambele akakumbuka enzi yake alipokuwa RC wa Dar es Salaam na uhusiano wake na Kitwana Kondo.

Mzee Songambele akapiga moyo konde akaenda nyumbani kwa Kitwana Kondo kumweleza shida yake akitaka nyumba yake arejeshewe.

Lakini kwa bahati mbaya hakumkuta nyumbani akamkuta mkewe. Songambele akamwachia Mzee Kondo ujumbe huu kupitia kwa mkewe akasema: “Mwambie mumeo, Mustafa Songambele kaja hapa ana shida anataka umsaidie. Mwambie Mustafa anakuambia, ‘Mungu kibidu, yeye ataelewa.’”

Ujumbe ulimfikia Kitwana Kondo na anasema alicheka. ‘Kibidu’ ni neno la Kizaramo, maana yake kugeuka. Mzee Kondo alikuwa na kawaida ukizungumza naye hakosi kukupa msemo wa katika lugha ya Kizaramo au kukupa shairi la mshairi maarufu, Muyaka bin Haji.

Kifo cha Mzee Mustafa Songambele kimenikumbusha mengi na watu wengi waliotangulia mbele ya haki. Namuomba Allah amsamehe mzee wetu dhambi zake na amtie peponi.