Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tunduru

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limejidhatiti katika kuhakikisha huduma ya umeme inaimarika kwa wilaya za Tunduru, Nanyumbu na Masasi.
 
Amesema hayo Mkurungenzi Mtendaji wa TANESCO Gissima Nyamo-Hanga tarehe 10 Januari 2024 wakati alipotembelea Kituo kipya cha kudhibiti na kuboresha umeme (AVR) kilichojengwa Wilaya ya Tunduru eneo la Pachani.
 
Mha. Gissima amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho kipya ni hatua muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa umeme katika wilaya hizo.


“Kukamlika kwa ujenzi wa mitambo hii kunaenda kuboresha hali ya patikanaji wa umeme kwa baadhi ya wilaya za Mtwara ambazo ni Nanyumbu na Masasi, itasaidia pia kukipunguzia mzigo kituo cha kuzalisha umeme kwa gesi asilia cha Mtwara kwa megawati 5,” amebainisha Mha. Gissima.
 
Ameongeza kuwa kuondoa kwa megawati 5 katika kituo cha Mtwara zilizokuwa zinapelekwa Masasi na maeneo jirani kutasadia kupeleka umeme huo katika wilaya zingine zinazopatikana mikoa ya Mtwara na Lindi na kuimarisha upatikanaji wa umeme katika wilaya hizo.
 
“Hatua hizi tunazozichukua kama Shirika ni utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati waliyotoa kwa nyakati tofauti ya kuhakikisha mikoa ya Lindi na Mtwara inakuwa na umeme wa uhakika,” amesema Mha. Gissima.


Ameongeza kuwa jitihada za sasa zinazofanyika ni za mipango ya haraka, lakini mipango ya muda mrefu ni utekelezaji wa ujenzi wa njia kubwa ya umeme ya kilovoti 220 wa Gridi ya Taifa kutoka Songea, Tunduru hadi Mahumbika.

Mitambo iliyojengwa Wilaya ya Tunduru eneo la Pachani unapokea umeme kilovoti 33 kutoka Songea umbali wa kilomita 197. Hivyo, uwepo wa mitambo hiyo utasadia kuboresha upatikanaji wa umeme unaopelekwa wilaya za Tunduru, Nanyumbu na Masasi.