Hivi sasa watu duniani wanaonekana kupenda mchezo wa soka zaidi kuliko michezo mingine, na mezzo huo umekuwa ukiongeza ajira kwa vijana kila kukicha.

Lakini kwa upande wa Tanzania viongozi wa michezo wameonekana kujali maslahi zaidi kuliko mipangilio ya kuendeleza soka.

 

Miaka ya 1980 Tanzania ilikuwa tishio katika michezo ukiwemo soka, hali ambayo ilitikisa katika ulimwengu wa michezo.

 

Ufanisi huo uliwezeshwa na wachezaji mahiri pamoja na makocha wazawa, ambao wakati mwingine tunawadharau. Ilikuwa tofauti na sasa ambapo tunabadilisha wa kigeni kila kukicha lakini soka letu halionekani.

 

Kinachoonekana ni kwamba makocha hao wageni wanakuja nchini wakidhani Watanzania wako tayari kucheza soka la kulipwa kama nchi zilizopiga hatua. Serikali na vyama vyetu vya michezo vinadhani makocha wetu hawawezi kuendeleza soka letu.

 

Ilitakiwa makocha wageni wanapokuja hapa nchini, tuchote mafunzo yao ili tuyafanyie kazi, lakini badala yake kabla hawajakaa hata muda tunawafukuza.

 

Natolea mfano kocha wa timu ya vijana ya Simba, Selemani Matola, ambaye aliifundisha timu hiyo katika mashindano yaliyoandaliwa na Benki ya ABC na Simba ilinyakua ubingwa huo.

 

Tabia kama hiyo kwa klabu zetu za Ligi Kuu Tanzania Bara zinaonesha kuchangia kuvuruga maendeleo ya soka kwani kama zingejipanga vizuri, tusingekuwa hapa tulipo.

 

Hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa hata timu yetu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kuwa butu, ingawa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kila kukicha linajitahidi kutoa elimu na misaada mbalimbali.

 

Márcio Máximo, aliingia mkataba wa kwanza kuifundisha (Taifa Stars), Juni 29, 2006, baadaye akaongezwa mkataba mwingine Julai, 2010 kabla ya kupewa Mdenimark, Jan Poulsen, ambaye hakudumu, nafasi yake ikachukuliwa na mwenzake, Kim Poulsen.

 

 

Kocha Tom Saintfiet  alijiunga na Klabu ya Yanga Julai 6, mwaka huu kwa mkataba wa miaka miwili, lakini mapema mwezi huu, uongozi wa timu hiyo ulimtimua kwa sababu za kuiyumbisha timu hiyo. Kwa sasa ameingia kocha Erniest Brandts.

 

Kocha Stewart Hal, yeye aliingia mkataba wa kuifundisha timu ya Taifa ya Zanzibar, (Zanzibar Heroes) kwa miaka mitano, Juni 2010 na Agosti 2012 kabla ya kujiunga na Azam FC.

 

Kocha huyo aliondolewa kuifundisha Azam na kwenda Kenya kuifundisha Klabu ya Sofapaka. Siku aliyotangazwa kutimuliwa, wachezaji walimwaga machozi kutokana na uwezo mkubwa wa kufundisha wa kocha huyo waliyopata, lakini viongozi kwa maoni yao wakaona ni suluhisho kumuondoa. Cha kushangaza amerejeshwa na tayari ameiongoza Azam katika michuano ya shirikisho kabla ya kuondolewa katika raundi ya pili na FAR ya Morocco.

 

Patrick Phiri, huyu alianza kufundisha Simba msimu wa 2004/2005, alionesha ufanisi mkubwa kabla ya timu hiyo kumchukua kwa mara nyingine Januari 2009, na kufanikiwa kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu bila kupoteza mchezo hata mmoja.

 

Pamoja na mafanikio ya kocha huyo alitimuliwa Aprili 2011 na uongozi bila kutaja sababu za msingi.

 

Tujikumbushe Angola ambayo ilishiriki mashindano ya kuwania kombe la Matifa ya Afrika mwaka 2010, baada ya kujipanga ndani ya miaka 10 kufanikisha maendeleo hayo, lakini sisi tunafanya mambo ya zimamoto.

 

Misingi mizuri ya soka ikifuatwa tutaondoka hapa tulipo na kuelekea katika soka la ushindani katika medani za kimataifa.

 

Mfano, benki ya ABC ilionesha kutaka kuboresha soka kwa kuandaa ligi fupi ya wiki mbili na mshindi akajizolea milioni 40.

 

Achilia mbali, Azam ina nia ya dhati kufanikisha soka la Tanzania, kwa kujenga uwanja wa kisasa pamoja na kuwekeza katika soka la vijana.

 

Timu zetu tunazoziita kubwa hapa Tanzania, Simba na Yanga, viwanja vyake ni vichekesho na ubabaishaji tu. Tubadilike ili tufikie walipo wenzetu waliopiga hatua.

 

Sababu za awali zilikuwa ni wanaoongoza soka; elimu yao ni ya ‘ngumbaru’ sababu ambayo inaonekana ni ya ‘walafi’ wanaofanya mipango ya kujaza matumbo yao.

Please follow and like us:
Pin Share