Tanzania iwe kwa Watanzania kwanza

Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) kilichodai Uhuru wa nchi hii kilikuwa na ahadi nzuri. Baadaye Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilizirithi.

Raha ya ahadi hizo ni kuwa zililenga kujenga uzalendo na upendo miongoni mwa wananchi. Shabaha yake ilikuwa kuwafanya Watanganyika na baadaye Watanzania, waone fahari ya kuipenda nchi yao na kuwa tayari kuitumikia kwa nguvu na weledi wote.

 

Ahadi hizo zina sifa ya kuwa tunu ya Taifa na dira ya kutuwezesha kukijenga kizazi imara cha sasa na kijacho. Waungwana hawawezi kuzipuuza kwa sababu tu zinatokana na CCM. Tulikubali jema bila kujali linatoka upande gani. Ahadi hizo ni:

(1) Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja.

(2) Nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote.

(3) Nitajitolea nafsi yangu kuondosha umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma.

(4) Rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa.

(5) Cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu.

(6) Nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa faida ya wote.

(7) Nitashirikiana na wenzangu wote kujenga nchi yetu.

(8) Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.

(9) Nitakuwa mwanachama mwaminifu wa CCM na raia mwema wa Tanzania na Afrika.

 

Tukiacha mambo ya kiitikadi yanayotugawa, ukweli ni kwamba hizi zilistahili kabisa kuwa ni ahadi za kila Mtanzania. Kwa mtazamo wangu, marekebisho madogo yalistahili kufanywa kwenye ahadi ya tisa kwa kuondoa maneno ‘mwanachama’ na ‘CCM’ na kuwa: ‘Nitakuwa mwaminifu kwa nchi yangu na raia mwema wa Tanzania na Afrika’.

 

Operesheni Kimbunga imeibua mengi. Mhamiaji haramu mmoja kaamua kujiua kwa sababu tu katakiwa arejee kwenye nchi yake ya asili, yaani Rwanda.

 

Huu ni ushahidi timilifu wa namna raia wa mataifa mengine wanavyoipenda Tanzania kiasi kwamba wapo tayari kujitoa uhai kwa kutakiwa, ama warejee kwao au wahalalishe ukazi wao. Hii ni changamoto kwa Watanzania wazalendo. Tujiulize, kwanini mtu ajitoe uhai kwa sababu tu katakiwa arejee kwao?

 

Inawezekana mhamiaji huyo alitambua kuwa kwa kurejea Rwanda, hatakuwa na maisha mazuri kama aliyokuwa akiyafaidi hapa nchini. Kwake, kujiua kulikuwa jambo la msingi kuliko kuona akirejea huko.

 

Nimejaribu kuzirejea ahadi hizo za wana-TANU na wana-CCM kwa lengo moja kubwa la kujaribu kuamsha hamasa ya Watanzania tuipende nchi yetu na kuwapenda binadamu wenzetu. Amri ya Rais Jakaya Kikwete ya kuwataka wahamiaji haramu warejee kwao au wahalalishe ukazi wao nchini, haikulenga kuwanyanyasa binadamu hawa wenzetu.

 

Kama nilivyowahi kusema kwenye makala zilizopita, wema unapaswa uwe wa kiasi. Si busara, na kwa kweli si akili, kuona familia yako ikitaabika kwa kulala njaa kwa sababu tu wewe mtunza familia hiyo umeamua kugawa chakula chote kwa majirani. Wema wetu Watanzania unapaswa kuwa wa kiwango. Lazima tuhakikishe kuwa Tanzania inabaki kuwa ya Watanzania kwanza, wageni baadaye. Tunapojaribu kuujenga uchumi hatuna budi kuhakikisha unawanufaisha kwanza Watanzania kabla ya wageni au hawa waliopewa jina zuri la wawekezaji.

 

Athari za kuwapo wahamiaji haramu nchini mwetu ni nyingi kuliko faida tunazopata. Idadi ya wahamiaji haramu nchini ni kubwa mno. Wapo wanaoamini kuwa hata hiki tunachokiona kuwa ni ukuaji wa miji yetu, hakipo kwenye uhalisia wa kasi ya Watanzania kuzaa. Wengi wanaamini wahamiaji haramu wamekuwa kundi kubwa sana ndani ya nchi yetu.

 

Tangu kuanza kutekelezwa kwa Operesheni Kimbunga, lawama zimekuwa zikitolewa na watu na mashirika kadhaa. Hawa wanaoeneza propaganda hizi hawapaswi kutunyima usingizi kwa sababu miongoni mwao ndiyo hao hao wahamiaji haramu. Wanapaza sauti za kuilaani Serikali ya Tanzania kana kwamba hao wahamiaji hawakupewa njia nyingine ya kuhalalisha ukazi wao nchini. Hapa ndipo ninaposhawishika kutoa ushauri kwa vyombo vya dola kuwafuatilia kwa karibu wote wanaopinga Operesheni Kimbunga. Inawezekana kabisa wengi wao wakawa si Watanzania.

 

Hatuwakatai wageni wala watu wa mataifa mengine kupata uraia wa Tanzania. Hakuna anayekataa. Tena basi, tunapaswa kuwahimiza wageni hao wajitokeze kuomba uraia ili baadaye tuwabane waweze kuwajibika kulitumikia Taifa hili.

 

Kwa miaka zaidi ya 50 Tanzania imesomesha wahamiaji haramu wengi mno. Miongoni mwao sasa ni viongozi katika mataifa jirani. Wanajulikana. Walisoma bure, lakini tija za elimu wamezihamishia katika nchi zao za asili. Haikushangaza hivi karibuni kusikia ‘Mtanzania’ mmoja akiteuliwa kuwa Waziri katika Serikali ya Rwanda. Wengine wamesoma kwa mikopo ambayo hawawezi kuirejesha maana wamesharudi kwao.

 

Serikali imetumia mamilioni ya shilingi kusambaza huduma za afya katika maeneo mengi nchini. Wahamiaji haramu wamepewa huduma bila kulipia chochote. Hao hao wamepata huduma za maji safi na salama bure. Hakuna aliyekubali kuitumikia nchi hii baada ya kupata huduma hizo. Wote sasa wapo katika mataifa yao wakiyaendeleza.

 

Wahamiaji haramu wameingia nchini mwetu na kujitwalia maeneo ya ardhi wakijitambulisha kuwa ni Watanzania. Kwa kutumia kigezo cha kila Mtanzania ana haki ya kuishi popote hapa nchini, wamemilikishwa ardhi huku Watanzania halisi wakikosa fursa hizo. Hili haliwezi kuendelea kukumbatiwa na Serikali inayowajali raia wake.

 

Operesheni Kimbunga haipaswi kuishia kwa Wanyarwanda, Wakongo, Warundi, Waganda, Wanigeria, Wasomali, Wanyasa au Wakenya pekee.

 

Kuna idadi kubwa sana ya wahamiaji haramu kutoka Asia. Wanafanya kazi ambazo zingepaswa kufanywa na Watanzania. Wapo wanaofanya hadi kazi za kupaka rangi! Wanaishi kwenye mabohari. Kuna Wachina wengi sana wanaoishi nchini kwa mtindo huo. Kuna Wahindi na Wapakistani wengi sana.

 

Juhudi za kuwashughulikia hawa zinakwamishwa na vitendo vya rushwa miongoni mwa watumishi wa Idara ya Uhamiaji. Tangu kutangazwa kwa Operesheni Kimbunga huu umekuwa mradi wa maofisa Uhamiaji na Polisi. Wanawakamata wahamiaji haramu. Wanahongwa.

 

Wanawaacha waendelee kuishi kihuni nchini mwetu. Hawa ni janga. Wanawakosesha Watanzania wengi kazi. Fagio lililoelekezwa kwa wahamiaji kutoka mataifa ya Afrika lazima lielekezwe kwa hawa wanaotoka Asia, Ulaya na kwingineko.

 

Tunapaswa kupambana na hali hii bila kukata tamaa wala kuvunjwa moyo na manabii walioamua kuwa watetezi wa watu wanaoishi nchini mwetu bila kufuata sheria. Tuna kila sababu za kuwakomalia kwa sababu hata huko walikotoka, Serikali zao haziwezi kukubali kuwaona Watanzania wakiishi bila kufuata sheria za mataifa hayo. Huo ndiyo ukweli. Wakati nikiandika makala haya, Serikali ya Afrika Kusini nayo imetangaza operesheni maalum ya kukabiliana na wahamiaji haramu na kukomesha magenge yanayofanya biashara ya kusafirisha binadamu.

 

Pia tunapaswa kulikemea Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi (UNHCR) ambalo limejaribu kupotosha ukweli juu ya Operesheni Kimbunga. UNHCR wanasema Serikali ya Tanzania inawafukuza wakimbizi. Huu ni upotoshaji. Shirika hili linalenga kuijengea Tanzania taswira hasi mbele ya jumuiya ya kimataifa.

 

Lakini wenye kuelewa hawawezi kushangaa. Shirika hili halijawahi kuendesha ‘sala wala maombi’ yenye lengo la kuona wakimbizi wakikoma kuwapo duniani, hasa Afrika. Limeajiri maelfu ya watu kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi. Wanalipwa mabilioni ya dola kutokana na kuwapo wakimbizi. Wameona wakimbizi wengi wamesharejea Burundi, Rwanda na DRC. Wamerejea kwa hiari baada ya amani kuwapo katika mataifa hayo.

 

UNHCR wanaona uwepo wao unaanza kuwa hatarini. Wanaona fedha wanazotafuna kwa ‘kulea’ wakimbizi zinaelekea kuota mbawa. Kwa hiyo wanajitahidi kuwafanya wahamiaji haramu watambuliwe kama wakimbizi halali wanaostahili kuwapo Tanzania. Hii si mara ya kwanza. Wakati Tanzania ilipowarejesha wakimbizi wa Rwanda na Burundi miaka kadhaa iliyopita, UNHCR ilijaribu kuwashawishi wagome! Tabia hiyo bado wanaendelea nayo. Kama wanaona kuwalea wakimbizi ni jambo jepesi, wawahamishie Ulaya na Marekani.

 

Mapambano ya kuwaondoa wahamiaji haramu hayawezi kuwa na manufaa kama tutawachekea wale wote wanaowakaribisha na kuwapa makazi. Kama wapo walionunua ardhi, lazima tuwajue hao waliowauzia au waliowawezesha wakaipata. Tuwajue viongozi wa vitongoji na vijiji waliojitwalia madaraka ya kuwapa vibali vya kuishi au ardhi ya kilimo na malisho.

 

Twende hadi Uhamiaji na Wizara ya Kazi tujue nani anawapa vibali vya kazi ambazo kimsingi zinastahili kufanywa na Watanzania. Tusioneane aibu kwenye hili jambo. Tija za mpango huu ni nyingi na nzuri. Tangu kuanza kwa Operesheni Kimbunga, matukio ya ujambazi yameripotiwa kupungua. Huu ni ushahidi kuwa wageni hawa wasiokuwa na chembe ya utu ni watu hatari. Kamanda Simon Siro anayeendesha Operesheni hii aungwe mkono.

 

Tuendelee kumuunga Rais Kikwete kwa uamuzi huu ambao wengine tulishauri tangu mwaka 2006. Wale wanaomwandama kwa kutaka kuonesha kuwa amekosa utu, waache propaganda hizo. Misuguano yetu ya ndani ya nchi ibaki kuwa ya ndani. Linapokuja suala la kuungana pamoja kutetea maslahi ya Taifa letu, sote tunapaswa kuwa kitu kimoja.

 

Hapo juu nimeandika ahadi kenda za wana-CCM ambazo naona kimsingi ni ahadi zilizostahili kuwa za kila Mtanzania. Jambo jema tunapaswa kulikubali bila kujali linatoka CCM au upande wa Upinzani. Hizo ahadi tisa tukizizingatia, sina shaka yoyote kwamba ari yetu ya uzalendo itakuwa imepata msukumo mpya.

 

Mwisho, nina mapendekezo mengine. Baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa siasa ya vyama vingi nchini, nafasi ya Balozi wa Nyumba Kumi imepuuzwa. Imepuuzwa kwa sababu imeonekana kwamba ipo kwenye mfumo wa ki-CCM.

 

Pamoja na ukweli huo, nafasi hiyo ni muhimu maana ilisaidia mno kuwatambua wageni katika eneo la nyumba kumi. Tunaweza kuifanya ngazi ya Balozi wa Nyumba Kumi kuwa ya kiserikali kabla ya ngazi ya pili ya Kitongoji au Mtaa. Kama kazi za mabalozi kwa miaka hiyo ilionekana kuwa na tija, sioni ni kwanini sasa tuipuuze! Suala la ulinzi na usalama wa nchi yetu halipaswi kuwa la itikadi ya chama cha siasa.

 

Kwa mara nyingine napongeza uwepo wa Operesheni Kimbunga. Muhimu ni kuifanya iwe endelevu. Tuhakikishe Tanzania inakuwa ya Watanzania kwanza.