Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

TANZANIA kwa nafasi yake ya Uenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (AGN) itaongoza na kubeba sauti ya pamoja ya vipaumbele vya Bara la Afrika wakati wa Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30).

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja, alisema hayo Jijini Dodoma juzi wakati akifungua Kikao cha Makatibu Wakuu cha maandalizi ya COP 30 utakaofanyika Brazil kuanzia Novemba 10 hadi 21, 2025.

Alisema Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alizindua Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 (Dira 2050) Julai 17, 2025, akiithibitisha nia ya Serikali ya kuwa na maendeleo yenye ustahimilivu wa mabadiliko ya tabiahchi na kuwa taifa lenye ustawi, jumuishi na endelevu, ambapo kila sekta ya maendeleo Nchini inatakiwa kuzingatia dhana ya maendeleo endelevu.

“Mwaka huu COP30 ni ya kihistoria kwa kuwa mkutano huu utafanyika katika nchi yenye historia ya kuanzishwa kwa Mkataba husika na hivyo ajenda zitakazojadiliwa zinatarajiwa kufafanua njia na hatua za haraka hususan katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi baada ya miaka 33 ya uwepo wa Mkataba.

“Kwa Tanzania, Mkutano huu sio wa majadiliano tu bali utahusika pia katika kuongeza mashirikiano na wadau mbalimbali duniani kwa lengo la kuongeza fedha za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zitachangia katika kukuza uchumi na kuimarisha maendeleo ya Kijani Nchini.” alisema Luhemeja.

Aliongeza katika kuhakikisha hili, Serikali imeanza kuandaa nyezo za utekelezaji vipaumbele vya Dira, na kwa sasa, Serikali ipo katika mchakato wa kukamilisha mipango miwili muhimu ambayo ni Mchango wa tatu wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchia.

Kwa upande wake, Mshauri wa Rais katika masuala ya mazingira na Mwenyekiti wa AGN Dkt. Richard Muyungi amesema katika mkutano wa kwanza uliofanyika mapema mwaka huu Zanzibar walikubaliana Ajenda ya nishati safi iwe agenda kubwa ya Afrika kuelekea COP30.

“Tunapopambana kuhusu mabadiliko ya tabianchi tunapaswa kuakisi hali halisi ya Afrika katika kumkomboa Mwanamke, Kijana na Mwafrika hasa kutokana na changamoto tunazozipata zinazotokana na kutokuwa na nishati safi ya kupikia pia kutokuwa na umeme.

“Umeme ni ajenda ya pili ambapo hadi kufikia 2030 asilimia kubwa wawe wanatumia umeme na mwisho ni fursa kwa vijana katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa vijana wengi walikuwa hawashirikishwi lakini kwa sasa tumewapa kipaumbele,” amesema Dkt. Muyungi.

Naye, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, Mhandisi Ussi Khamis Debe akimwakilisha Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema asilimia kubwa ya uchumi wa Zanzibar umejikita zaidi kutokana na Uchumi wa Buluu.

Alisema Uchumi wa Buluu una maeneo mengi kwa upande wa Zanzibar kama vile Uvuvi, Kilimo, Utalii na maeneo hayo yamekuwa yakikumbwa na changamoto kutokana na mabadiliko ya tabianchi.