Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imethibitisha dhamira ya kuendeleza miundombinu endelevu na mifumo bora ya usafirishaji kwa Nchi Zisizo na Mlango wa Bahari (LLDCs).
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli nchini (TASAC) Bw. Mohammed Salum alipochangia mada katika majadiliano ya Kujenga Miundombinu Endelevu, Kuimarisha Muunganisho na Kukuza Mifumo ya Usafirishaji Isiyokuwa na Vikwazo kwa Nchi Zinazokosa Ufikiaji wa Bahari kwenye Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa wa Nchi zinazoendelea zisizo na Mlango wa Bahari (LLDC3) unaofanyika Awaza nchini Turkmenstan.
“Kwa sasa, Tanzania inatumika kama njia kuu ya usafirishaji wa bidhaa kwa nchi jirani kama Zambia, Malawi, Rwanda, Burundi, Uganda, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kupitia Bandari ya Dar es Salaam, ambayo inahudumia zaidi ya asilimia 36 ya mizigo yote ya nchi hizo.
Amesema katika kuboresha huduma za usafirishaji, Tanzania imechukua hatua mbalimbali kama vile kupunguza vizuizi vya mizani barabarani, kuondoa vizuizi vya ukaguzi, na kurahisisha taratibu za forodha pamoja na kuendelea kuboresha Bandari ya Dar es Salaam kwa kuongeza uwezo wa kupokea na kushughulikia mizigo, kupunguza muda wa meli bandarini, na kuongeza ufanisi wa kupakia na kupakua mizigo.
“Sambamba na uboreshaji wa bandari, Tanzania inatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kupitia Morogoro na Dodoma. Reli hii itakapokamilika itaunganishwa na nchi za Rwanda, Burundi, na DRC na hivyo kuwa njia ya haraka, salama, na rafiki kwa mazingira ya usafirishaji wa mizigo,” alisisitiza.

Amesema kuwa Tanzania pia imeanzisha bandari kavu na vituo vya usafirishaji katika maeneo ya Kwala (Pwani), Isaka (Shinyanga), na Ihumwa (Dodoma), ili kupeleka huduma za bandari karibu na nchi zisizo na bandari na kwamba Bandari ya Mwanza hutumika kusafirisha bidhaa kwa njia ya Ziwa Victoria hadi Uganda, huku jitihada zikiendelea kufufua Reli ya TAZARA inayounganisha Tanzania na Zambia.
Ameongeza kuwa upatikanaji wa nishati ni sehemu muhimu ya maendeleo ya biashara na kwamba Tanzania inaendelea kuimarisha miunganisho ya umeme na nchi jirani kupitia Mfumo wa Umeme wa Afrika Mashariki, na pia inawekeza katika miradi mikubwa ya nishati jadidifu kama Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere wa megawati 2,115 kwa ajili ya kuendesha reli, vituo vya mizigo, na vituo vya mpaka kwa njia endelevu.