Na Immaculate Makilika – MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema kuwa Serikali imefikia uamuzi wake wa kuingia makubaliano na kampuni zenye uwezo wa kuchimba na kuchakata madini nchini ili nchi iweze kunufaika na kupata faida kutokana na raslimali hizo kwa kuunda kampuni za ubia na hivyo Serikali kunufaika kupitia tozo, kodi, ajira, maendeleo ya miundombinu na ukuaji wa teknolojia.

Amesema hayo leo Aprili 17, 2023 Chamwino Ikulu Dodoma wakati akishuhudia utiaji saini wa mkataba mkubwa na wa kati baina ya Serikali ya Tanzania na Kampuni tatu za uchimbaji madini kutoka nchini Australia.

Rais Dkt. Samia alisema kuwa mikoa ya Lindi na Morogoro ipo katika ukanda wa madini kinywe na Mkoa wa Songwe uko katika ukanda wenye madini adimu ndio maana miradi iliyowekwa saini iko katika Wilaya za Lindi, Ulanga na Songwe.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi pamoja na Wageni mbalimbali mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa Mikataba baina ya Serikali ya Tanzania na Kampuni tatu (3) za Uchimbaji Madini Muhimu na Madini ya Kimkakati kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 17 Aprili, 2023.

“Utafiti wa madini ya kinywe na madini adimu ulianza tangu mwaka 2000 kupitia kampuni mbalimbali ambapo hadi sasa kuna kiasi cha tani milioni 67 zenye wastani wa asilimia 5.4 ya madini ya kinywe yaliyogundulika katika kijiji cha Chilalo ambayo yatachimbwa kwa muda wa zaidi ya miaka 18, tani milioni 63 zenye wastani wa asilimia 7.6 yaliyogundulika katika kijiji cha Epanko nayo yatachimbwa kwa zaidi ya miaka 18.

Pia tani milioni 18.5 zenye asilimia 4.8 zenye madini adimu yamegundulika katika kijiji cha Ngwala ambayo yatachimbwa kwa zaidi ya miaka 20 madini hayo ya kinywe na adimu yapo katika orodha ambayo kwa sasa yanajulikana kama madini muhimu duniani kwa kuwa yanahitajika sana katika teknolojia mpya ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambapo hutumika kutengenezea betri za magari, vifaa vya kieletriniki na mitambo mbalimbali ” amesema Rais Samia.

Ameongeza kuwa kufuatia uwepo wa madini hayo nchini, wawekezaji wakubwa duniani wameonesha kuvutiwa na Tanzania na kuwa hivi karibuni wakati wa ziara ya Makamu wa Rais Marekani nchini, Mhe. Kamala Harris walizungumzia umuhimu wa madini hayo pamoja na mradi wa Nikeli wa Kabanga na kiwanda cha usafishaji madini kitakachojengwa Kahama.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akishuhudia Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Eliezer Mbuki Feleshi wakisaini Mkataba wa Makubaliano ya Msingi (Framework Agreement) baina ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya EcoGraf Limited ya Australia iliyowakilishwa na Mtendaji Mkuu wake Andrew Spinks pamoja na Christer Mhingo kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 17 Aprili, 2023. Mkataba huu unahusu mradi wa Epanko, Ulanga Mkoani Morogoro.

Rais Samia alisisitiza “Katika siku zijazo nchi yetu itakuwa kitovu cha uzalishaji na usafishaji wa madini haya na hivyo kuvutia uwekezaji mahiri, vilevile kwa kutumia nafasi yetu kijiografia ambayo tumezungukwa na nchi nane ambazo baadhi zina madini kama haya fursa hiyo itatufanya Tanzania kuzidi kutunufaisha hasa kwa kuwa tutakuwa na viwanda vya kuchakata madini hayo hapa lakini pia tuna njia za kuaminika za kusafirisha madini hayo”

Waziri wa Madini,Dotto Biteko amesema kuwa miradi hiyo ya madini ni kielelezo tosha kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kwa dhati kuisimamia sekta ya madini na hivyo ukuaji wa sekta ya madini katika mchango wa Pato la Taifa umeongezeka zaidi katika kipindi kifupi ambapo Julai hadi Septemba 2022 sekta ya madini imeshachangia asilimia 9.7 ikiwa ni asilimia 0.3 kufikia lengo lililowekwa katika malengo ya Taifa.

“Sekta hii, Rais umeilea na imendelea kuwa tegemeo kubwa katika mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kutuletea fedha za kigeni hapa nchini. Miradi hii yote ambayo leo imesainiwa italeta mtaji kutoka nje ya nchi jumla ya dola za Kimarekani milioni 667 hii ni miradi mikubwa na jambo la maana sana Mhe. Rais wakati dunia inahangaika kutafuta madini ya mkakati, miradi yote tuliyosaini leo hapa ni madini ya mradi wa kimkakati ambayo dunia inayahitaji” alisema Waziri Biteko.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akishuhudia Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu akisaini Mkataba wa makubaliano ya Wanahisa baina ya Serikali na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Evolution Energy Minerals ya Australia iliyowakilishwa na Mtendaji Mkuu wake Phillip Hoskins, pamoja na viongozi wengine Michael Bourgnoin pamoja na Heavenlight Kavishe kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 17 Aprili, 2023.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Timu Maalum ya Serikali ya Majadiliano, Prof. Palamagamba Kabudi alisema Tanzania imejaliwa kuwa na madini mbalimbali na hivyo kampuni ambazo Serikali inaingia nayo mkataba wa uchimbaji wa madini ni Picklayer Earth Ltd kutoka Australia na kupitia kampuni mbili zilizoundwa kwa ubia za Mamba Minerals Corporations itakayojihusisha na uchimbaji wa madini na Mamba Refinery Corporations itakayojihusisha na uchenjuaji wa madini na kuwa kampuni hizo mbili Serikali ya Tanzania ina hisa ya asilimia 16 isiyofifishwa.

Prof. Palamagamba alisema “Gharama za uwekezaji za awali katika mradi huu ni dola za Marekani milioni 439 na katika maoteo ya mwanzo tuliyofanya mradi huu utakuwa Ruangwa mkoani Lindi kwa miaka 18, tunatarajia thamani ya mauzo ghafi ya madini haya ya Kinywe yatakuwa dola za kimarekani bilioni 1 na milioni 860”

Anaongeza “Kwa mgawanyo tuliouweka katika mizania mgawanyo mwekezaji na mbia wetu yeye atapata dola milioni 389 ambayo ni sawa sawa na asilimia 47 na Serikali itapata dola milioni 437 ambayo ni sawasawa na asilimia 53”.

By Jamhuri