Pongezi hizo zimetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, MMonique Nsanzabaganwa alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula pembezoni mwa Mkutano wa Wanawake na Vijana katika Biashara katika Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) uliofanyika kuanzia tarehe 12 hadi 14 Septemba 2022 Jijini Dar es Salaam.

Akifafanua shughuli za utekelezaji zinazofanywa na Kamisheni ya Umoja wa Afrika kwa kushirikiana na Nchi Wanachama Nsanzabaganwa alieleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa wadau muhimu katika Umoja wa Afrika ambapo, licha ya nafasi yake ya kuunga mkono uanzishwaji wa umoja huo pia imekuwa ikikamilisha michango yake ya uanachama kwa wakati.

“Ukamilishaji wa michango kwa wakati kutoka kwa Nchi wanachama unawezesha uendeshaji wa shughuli za Sekretarieti kutekelezeka kwa tija na kusaidia kupatikana kwa maslahi ya watumishi.” alisema Mhe. Nsanzabaganwa.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amemuhakikishia Mhe. Nsanzabaganwa kuwa Tanzania itaendelea kuheshimu makubaliano yaliyokubaliwa katika Umoja wa Afrika sambamba na kuhakikisha inanufaika na fursa mbalimbali zinazopatikana kama vile ajira na biashara.

Pia ameshukuru kwa jitihada zinazofanywa na Umoja wa Afrika kupitia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) kwa kumtambua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama Kinara wa Uhamasishaji wa Masuala ya Wanawake na Vijana katika biashara, sambamba na heshima iliyotolewa kwa Tanzania ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Wanawake na Vijana katika Biashara katika Eneo Huru la Biashara Barani Afrika.

Aidha,Waziri amesema kuwa mkutano huo ni muhimu sana kwakuwa umebeba agenda ya wanawake na vijana yenye lengo la kujenga haki na usawa wa kijinsia katika ajira, kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira, kuwajengea uwezo na kushirikishana uzoefu katika biashara na kuingia katika ushindani wa biashara kitaifa, kikanda na kimataifa.