CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kinampongeza Mobhare Matinyi kwa kuaminiwa na kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali.

Uteuzi wa Matinyi aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa TASWA, umefanywa jana Oktoba Mosi, 2023 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kabla ya uteuzi huo ulioanza mara moja, Matinyi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam.

Matinyi ambaye kitaaluma ni mwandishi wa Habari na Mwanadiplomasia mbobevu aliyewahi kufundisha Chuo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim, Kurasini jijini Dar es Salaam aliwahi kuwa Mwenyekiti wa TASWA kwa mafanikio makubwa.

TASWA tunamtakia kila la kheri katika nafasi hiyo aliyoaminiwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye pia anastahili pongezi kwa uteuzi huu.

Pia uongozi wa TASWA unazipongeza klabu za Simba na Yanga kwa kufuzu hatua ya makundi mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika yanayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

By Jamhuri