Na Mwandishi Maalum, Arusha
 
Kwa wiki yote iliyopita habari iliyogusa wengi katika sekta ya elimu ni ile iliyohusu kuzuiwa kwa vyuo 19 vinavyotoa elimu ya juu (vyuo vikuu) na baadhi ya vyuo kuzuiliwa kudahili wanafunzi katika baadhi ya kozi wanazotoa.
Jambo hili limegusa watu wengi, wazazi na walezi, wanafunzi na walimu wa vyuo husika. Uamuzi huu kutoka Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) umetokana na ukaguzi uliofanywa na TCU Oktoba, mwaka jana kwa vyuo husika na kubainika kuwapo kwa upungufu na kasoro kadhaa zilizochangia uamuzi wa sasa.
Uamuzi huu umeleta maswali kadhaa miongoni mwa jamii, kwa nini TCU wanatoa uamuzi wa ukaguzi waliofanya mwaka jana wakati huu ambao vyuo vinaelekea kudahili wanafunzi? Je, wajibu wao ni kutoa zuio tu na si kuelekeza upungufu uliojitokeza urekebishwe kabla ya udahili kuanza?
Ni upi mfumo wa ufuatiliaji wa TCU kwa vyuo? Ni huo ukaguzi wa kushtukiza na kufungia vyuo? Je, hawana utaratibu wa ukaguzi unaoeleweka wenye ratiba inayofahamika na vyuo pia? Vyuo hivi, je, vitaweza kulipa walimu na gharama nyingine za kuendesha chuo kwa kutegemea wanafunzi waliobaki?
Vipi kama vilikopa kwenye benki kuweka miundombinu na bado havijamaliza mikopo? Vitatoa wapi pesa kurudisha mikopo kama vimezuiliwa kudahili wanafunzi ambao ndio chanzo cha mapato ya chuo? Ukiachilia mbali tuhuma za rushwa ambazo TCU wametuhumiwa nazo kabla ya Rais kubadilisha mfumo wa udahili, je, ni kosa kuhusisha uamuzi huu wa sasa na rushwa kwamba kuna baadhi ya vyuo vimetoa rushwa kwa TCU ili wafungie baadhi ya vyuo na kozi kadhaa ili vyuo hivyo vipate wanafunzi wengi?
Maswali ni mengi, lakini jambo moja ni dhahiri kwamba TCU wamepoteza imani kwa jamii. Si rahisi kuamini uamuzi wowote wanaofanya katika kuinua elimu ya nchi yetu. Uamuzi mwingi wanaoufanya TCU hauzingatii uhalisia na kile ambacho kinatokea kwenye sekta ya elimu nchini.
Nilitegemea hata tu katika muundo wa timu ya TCU ilipaswa uzingatie uwakilishi wa makundi tofauti katika sekta ya elimu na si watu wa aina moja. Kwa mwenendo huu wa TCU kutojali nini hasa kinatokea kwenye sekta ya elimu kuanzia ngazi ya chini hadi kwenye hatua hiyo ya kuelekea elimu ya juu, nchi yetu bado itaendelea kukwama kielimu hadi pale serikali itakapotambua kuhuisha elimu katika ngazi zote.
Hao wanafunzi ambao TCU inaelekeza vyuo wadahili wanatoka katika shule za sekondari ambazo kuna tofauti kubwa sana miongoni mwao. Mfano kuna usawa gani wa kufanyisha mtihani mmoja wa kidato cha nne au cha sita watoto wa shule moja ya sekondari yenye walimu 5 haina maktaba wala maabara na nyingine yenye walimu 20, maktaba nzuri na maabara iliyokamilika?
Unatarajia watoto wenye shule yenye upungufu wafaulu kwa kiwango sawa na shule yenye miundombinu iliyokamilika? Je, ni sawa kuwahukumu watoto wa shule hiyo kwa ufaulu wao hafifu?
Nilitarajia TCU ielekeze nguvu nyingi kwenye kile ambacho vyuo vinapaswa kufundisha watoto waliotoka kwenye mfumo usio sawa ili angalau taifa letu lipate watu wazuri waliofundishwa  utaalam na ujuzi kwenye mazingira yanayofanana vyuoni, na si kutumia muda mwingi na rasilimali kwenye udahili. Udahili si chujio sahihi kama kweli tunataka kuelimika.
Inasikitisha kuona TCU na kwa maana hiyo serikali kushindwa  kutambua na kuheshimu mchango wa taasisi binafsi kwenye sekta ya elimu. Wote tunajua shule nyingi za binafsi ndizo zinafanya vizuri katika ngazi ya elimu ya msingi na sekondari kuliko shule za umma.
Inashangaza kuviwekea vikwazo au kuvizuia vyuo vingi binafsi, badala ya kuvielekeza na kuvisimamia viimarike ili viendelee kutoa elimu kwa viwango vinavyotakiwa. TCU wanaelekeza vyuo viwe na walimu wenye sifa za kufundisha, lakini hawatambui kuwa serikali inaajiri walimu waliofaulu kwa kiwango cha daraja la tatu kufundisha shule za msingi, je, ni sawa kukazia viwango kwenye ngazi ya vyuo na si kule chini?
Nadhani ili huku juu kwenye ngazi ya vyuo pawe imara ni lazima ngazi ya chini iwe imara zaidi. Vyuo vingi vya binafsi vinajitahidi kutoa fursa kwa watoto wale ambao kiwango chao cha ufaulu kinaathiriwa na mfumo usio sawa katika utoaji wa elimu ya msingi na sekondari.
Kuvizuia vyuo hivi kutoa elimu, badala ya kuvisaidia na kuvielekeza vitimize matakwa ya kutoa elimu ya juu ni kuzuia watoto waliosoma kwenye mazingira hafifu ambao ufaulu wao haukidhi kushindana na watoto waliosoma kwenye shule nzuri zenye mazingira bora ya kujifunzia.
Wengi wa vijana hawa wangependa kusoma kwenye vyuo ambavyo viko karibu na maeneo wanapoishi kwa maana hasa ya kupunguza gharama za masomo kwa sababu wengi wao hawapati ufadhili wa serikali kutokana na kiwango cha ufaulu walichopata.
Lakini pia siyo sawa kwa muktadha huu TCU kutumia viwango vya ufaulu vya sekondari (kidato cha sita pekee) kudahili wanafunzi. Ni bora wafikiri njia nyingine inayoweza kuwezesha kupata wanafunzi bora kuendelea na elimu ya juu. Waruhusu mitihani ya vyuo kuchuja wanafunzi wanaopaswa kuendelea na elimu ya juu. Kiwango cha kujiunga na elimu ya juu kwa maana ya udahili kiwe ambacho kinazingatia utofauti uliopo kwenye mfumo wa elimu ya msingi na sekondari tulionao.
Lipo suala jingine lenye kukatisha tamaa. Masomo ya msingi kwa madaktari ni Kemia na Baiolojia. Leo, TCU imetangaza bayana kuwa kwa watu ambao hawakusoma Fizikia, hata kama wamepata daraja la kwanza hawatadahiliwa kwenye udaktari.
Kimsingi napata tabu. Nafikiri mbali kuwa huenda TCU inafanya yote haya kutokana na hasira ya kunyang’anywa tonge na Mhe. Rais John Magufuli. Hadi sasa bado wanasisitiza kuwa vyuo vikidahili wanafunzi ni wao tu watapaswa kuthibitisha iwapo mwanafunzi anazo sifa za kujiunga na chuo hicho au la.
Kwa masikitiko nashuhudia nchi yetu ikiua elimu kwa njia ya posta (karumekenge), elimu ya watu wazima, mkondo wa kupata vyeti na kukukua kitaaluma hadi kufikia kubobea. Mitihani ya kidato cha sita inatolewa kwa wiki moja, lakini unakuta nesi aliyehudumia kwa miaka 20 ana ujuzi kuliko hata daktari, lakini huyu sasa hawezi kusomea udaktari kwa maelezo kuwa hakuhitimu kidato cha sita.
TCU wanaweza kuwa na nia nzuri, lakini sitaki kuamini kuwa wao wana viwango na  uelewa katika elimu kuzidi nchi kama Uingereza ambayo hadi leo inamdahili mtu aliyepata ufaulu wa E mbili kuingia chuo kikuu.
Tunachofanya leo tunajenga matabaka. Watabaki kuingia vyuoni watoto wa matajiri wanaosomea shule za kisasa na zenye vifaa vya kutosha, lakini wale wanaotokea familia maskini ambao wanategemea kibatari, basi hawa tunawahukumu milele.
Mwisho, ninaiomba Serikali ithamini na kutambua mchango wa sekta binafsi kwenye elimu ambao imekuwa ikiupata kwa muda mrefu. Isikimbilie kuadhibu vyuo badala ya kuvielekeza viendelee kusaidia kuelimisha watoto wetu.
Zuio la vyuo na baadhi ya kozi wanazotoa ni zuio kwa watoto wa masikini wasipate elimu ya juu, ambao ufaulu wao umeathiriwa na mfumo usio sawa wa utoaji na upimaji elimu na ufaulu uliopo.

By Jamhuri