Katika zama hizi za utandawazi, dunia yetu imetawaliwa na mifumo ya aina nyingi inayotikisa na kugusa maisha kila siku ya wakazi wa dunia nzima. Moja ya mifumo hiyo ni mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEKNOHAMA) pamoja na mfumo wa biashara.

Pamoja na kuwa mifumo hii kwa sasa ndiyo inayoiunganisha dunia na kuipa dhana ya utandawazi; kuna kuachana kukubwa sana unapolinganisha kati ya nchi zilizoendelea na zinazojikongoja kiuchumi kama Tanzania.

Kwa nchi zilizoendelea, Teknohama imekua sana. Imekuwa ndiyo kiongozi kwa kutengeneza njia kwa mfumo wa biashara. Kwa lugha rahisi ni kwamba ukuaji wa teknolojia umeendelea kuimarisha na kutengeneza fursa mpya za kibiashara.

Kwa bahati mbaya katika Tanzania, mifumo ya biashara inakua (japo kwa mwendo wa kinyonga) kuliko kasi inayoshuhudiwa kwenye Teknohama.

Historia inatuonyesha kuwa Teknohama ilipata mapinduzi makubwa, mara baada ya kugunduliwa kwa kompyuta zilizoruhusu matumizi ya mtu mmoja mmoja (personal computers) miaka ya 1960 nchini Marekani.

Kampuni nyingi za kijasiriamali zilichangamkia ugunduzi huu na kuanza kuvuna faida kubwa sambamba na kuendeleza ugunduzi mwingine katika eneo hili.

Moja ya kampuni hizo ni Dell Corparation iliyoanzishwa na Michael Dell, IBM iliyoanzishwa na Thomas J. Watson, Apple Computers na nyingine nyingi.

Msukumo zaidi ulitokea mara baada ya kuanza kutengenezwa kwa viendesha kompyuta (softwares). Alikuwa ni Mmarekani kwa mara nyingine tena, Bill Gates, aliyeibuka na kampuni yake maarufu, Microsoft, Inc. kuteka fursa hii ya kibiashara kwa kutengeneza mfumo wa kisasa wa kuendesha kompyuta (Windows-running system). Hii ilikuwa ni mwanzoni mwa miaka ya 1980 wakati Tanzania ilipokuwa katika usingizi mzito kuhusu teknolojia ya mawasiliano.

Mwanzoni mwa miaka ya 1990 dunia kwa mara ya kwanza ikashuhudia kuanzishwa kwa mfumo wa mtandao wa mawasiliano ya kompyuta (Internet); uliowezesha kuiunganisha dunia na kuifanya kama kijiji kwa kuimarisha mawasiliano ya kijamii na kibiashara.

Pengine Marekani iliona mbali kwa kuruhusu mfumo huu, uliokuwa unatumika katika jeshi lake utumike katika dunia nzima. Mawasiliano haya ya intaneti yaliibuka na fursa nyingine kubwa na mpya ya biashara za mtandaoni maarufu kama E-commerce.

E-commerce ni mfumo wa biashara unaowezesha wauzaji na wanunuzi kukutana na kufanya biashara sawa sawa, kama vile ambavyo wangekutana katika mazingira ya kawaida. Huu ni mfumo wa biashara ulioshika kasi katika mataifa yaliyoendelea – Marekani ikiwa inaongoza.

Kwa mfano, takwimu zinaonyesha kuwa kwa mwaka 2004 pekee kati ya mauzo yote ya rejareja yaliyofanywa Marekani, asilimia zaidi ya 16 yalifanyika kwa njia ya E-commerce. Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2025 asilimia 80 ya mauzo ya rejareja nchini humo yatakuwa yakifanyika kwa mfumo huo.

Kupitia mtandao, mteja anaweza kununua kutoka kwa kampuni, biashara kwa biashara zinaweza kuuziana (business to business) na hata wateja kwa wateja wanaweza kufanya biashara (consumer to consumer).

Biashara hii kwa njia ya mtandao inahusisha vyombo na hatua mbalimbali ikiwamo mabenki kwa ajili ya malipo, vituo vya kupokelea oda na kuzishughulikia. Wanunuzi (wateja) wa mfumo huu wanahitaji kuwa na kompyuta iliyounganishwa na mtandao wa intaneti, na au kadi ya malipo ya benki (credit card) au mfumo mwingine wa malipo, ikiwamo posta.

Nchini Marekani, kampuni maarufu ya vitabu ya Amazoni.com inashika asilimia kubwa ya soko la biashara ya mtandaoni, na ina huduma nyingi zaidi ya kuuza vitabu pekee. Mwanzilishi wa kampuni hii alichangamkia fursa ya biashara hii mara tu baada ya kuanzishwa kwa intaneti. Wafanyao biashara hii mtandaoni wanatengeneza maduka yao mtandaoni yanayojulikana kama Frontstores.

Katika nchi yetu, biashara hii ipo kwa asilimia ndogo mno na inakua kwa kiwango kidogo mno. Kutokana na serikali yetu kutokuwa na taasisi maalumu ya kushughulikia E-commerce, tofauti na nchi za wenzetu, inakuwa vigumu hata kupata takwimu sahihi za biashara hizi za mitandaoni kwa Tanzania. Ni wazi kuwa wafanyabiashara wengi bado hawajaishitukia fursa hii kubwa na muhimu kwa nchi yetu.

Tukigusia kukua na kupanuka kwa biashara zinazohusisha teknolojia ya mawasiliano, ni lazima kuangalia maeneo mengine yakiwamo ya benki zetu ambazo ni mhimili muhimu wa kufanikisha malipo ya haraka kwa biashara za mtandaoni. Katika eneo hili hatuwezi kukwepa kuangalia changamoto zinazojitokeza na kuwa kikwazo katika kufanikisha biashara, si tu za mtandaoni bali hata biashara za kawaida.

Benki nyingi zina milolongo mingi katika kutoa huduma zake na hata teknolojia ya kutumia mashine za ATM na mifumo ya kubadilisha na kuhamisha fedha haijaimarika. Bado au inafanywa kwa viwango vinavyoweza kutohimili ubora wa biashara za mtandaoni.

Eneo jingine ambalo ni muhimu sana ili kufanikisha biashara kwa njia ya mtandao, ni namna ya mteja kufikishiwa huduma au bidhaa aliyoinunua mtandaoni mahali alipo. Hapa miundombinu iliyopo nchini ni changamoto nyingine kubwa. Gharama za huduma za posta katika kusafirisha vifurushi, barabara mbovu katika maeneo mengi na kutokuwapo kwa mifumo ya mawasiliano ya kompyuta na simu ni mambo kinzani katika kufanikisha biashara za mtandaoni.

Changamoto hizo nilizozitaja sioni kama ni sababu kubwa za kutopiga hatua katika biashara hizi za kisasa. Kizazi cha wasomi na wataalamu katika nyanja ya biashara na teknolojia ya mawasiliano, inabidi kiamke kwa sababu hii ni fursa kubwa sana ambayo haijatumiwa bado.

Moja ya mambo tunayoweza kujuta ni kuchelewa kuzinduka na kufanya biashara za kisasa, halafu wageni kutoka nje waje kuvamia mfumo huu. Tunayo miji mikubwa ambayo angalau ina miundombinu mizuri na inafikika kwa urahisi. Tuanze kuitumia hiyo kwa kiwango cha juu.

Mwanzoni nimetanabaisha kuwa biashara na teknolojia ya mawasiliano vinapaswa kufunga ndoa – tena iwe ni ndoa ya uaminifu. Ndiyo, kwa sababu katika dunia ya sasa vitu hivi viwili ni shirika na haviachani. Kimoja kikitaka kwenda pekee – ama kitachelewa kufika au kitafia njiani.

Hebu tuangalie mfano mmoja. Kwa sasa kumekuwa na mfumko mkubwa wa kampuni zinazouza vifaa vya mawasiliano, na hapa ninagusia zaidi kompyuta na vifaa vinavyoiwezesha kufanya kazi. Je, ni Watanzania wangapi wanafahamu kutumia kompyuta? Bila shaka ni wachache sana. Ni maeneo mangapi ya nchi hii yana mtandao wa mawasiliano ya uhakika na bei nafuu ya intaneti? Pia jibu hapa utaona ni machache.

Kinachotakiwa hapa ni kuenea kwa miundombinu na elimu ya Teknohama halafu biashara ya huduma na vifaa vya teknolojia hii ifuate. Kuwapo kwa huduma na bidhaa za teknolojia hii kutawezesha kupanuliwa wigo wa kufanyika kwa biashara nyingine; na ni pale ambako Mtanzania atakuwa na uwezo wa kununua bidhaa yoyote kutoka mahali popote Tanzania na kupelekewa popote alipo katika eneo la Tanzania.

Msisitizo wa kutumia teknolojia ya mawasiliano katika biashara kwa wajasiriamali wa Tanzania, unakuja baada ya kutambua athari zinazoweza kuwapata wadau hawa kutokana na utandawazi. Tumeshaanza kuona mifano katika biashara kubwa kama za kuuza magari na mitambo. Kampuni kutoka nje zimeshaingia hadi mikoani na kwa kupitia mawakala wao. Sasa zinauza bidhaa zao kwa E-commerce katika maeneo mbalimbali Tanzania.

Wafanyabiashara wa magari na mitambo wa Tanzania ambao hawakushitukia fursa hii mapema ni kwamba sasa wapo katika hatari ya kupoteza wateja wengi na ushawishi katika masoko. Kwa sasa unaweza kununua hata kalamu kutoka London na ukafikishiwa ulipo, kwanini wajasiriamali wa Tanzania wasichangamkie fursa hii?

Haiwezekani kuwa na asilimia kubwa ya biashara hizi za mtandaoni kwa mara moja katika nchi nzima, lakini changamoto hapa ni kwa wataalamu wa masuala ya biashara na Teknohama kuangalia namna wanavyoweza kupanua wigo wa biashara za namna hii.

Tunahitaji ushindi wa kiteknolojia.

[email protected]
0719 127 901

By Jamhuri