Ligi Kuu imekwisha kufikia tamati na Klabu ya Simba kutwaa ubingwa. Nitoe pongezi kwa Simba na uongozi wao kwa hatua hiyo kubwa.

Lakini mbali na Simba, timu nyingine kadhaa zimeshiriki ligi hiyo kwa mafanikio hata kama si ya kiwango cha kutwaa ubingwa.

Katika miaka isiyopungua 10 lilikuwa jambo gumu Watanzania kushuhudia ligi yao ikirushwa moja kwa moja kupitia kituo chochote cha televisheni. Kilichokuwa kimezoeleka kwa Watanzania katika miaka hiyo au nyuma zaidi ni kufuatilia ligi hiyo kupitia matangazo ya redioni.

Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ilifanya kazi kubwa kuitangaza Ligi Daraja la Kwanza kama ilivyokuwa ikijulikana wakati huo. Taifa liliweza kuwasikia wachezaji wa ligi hiyo, namba walizocheza uwanjani, uhodari wao. Makocha wa timu hizo walisikika, wakati mwingine hadi  madaktari wa timu.

Kwa watu wanaofuatilia historia ya soka nchini hawawezi kupuuza hata kidogo mchango wa RTD  katika miaka ya nyuma hadi pale zilipoibuka redio nyingine binafsi katika tasnia ya utangazaji wa mpira nchini.

Tangu mwaka 2013, kituo binafsi cha televisheni cha Azam ni kama kilitwaa mikoba hiyo ya RTD.  Hatimaye, wakati huo Azam Media Limited ilifanikiwa kukamilisha utaratibu wa ushirikiano na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) uliowawezesha mashabiki wa soka kote nchini kunufaika kwa kuona michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom, kama ilivyokuwa ikijulikana kwa wakati huo. Baadaye ushirikiano huo na TBC1 ulifikia tamati, na Azam TV ikaendelea na jukumu hilo muhimu katika mustakabali wa soka la Tanzania.

Nakumbuka sana maneno ya Rhys Torrington kwa wakati huo akiwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam Media Limited, ambaye alisema: “Ninayo furaha kusema kuwa matayarisho yamekwenda vema kiasi kwamba tumejikuta tuko tayari kurusha matangazo ya kiwango cha juu kabla hata ya kuzinduliwa kwa huduma kamili za AzamTV.”

Ni kweli, kazi imefanyika. Maneno ya Rhys yalitimia na Azam Tv sasa imetoa taswira mpya kwa Ligi Kuu nchini.

Shukrani kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na mmiliki wa Azam Media Limited, Salim Said Bakhresa na familia yake kwa ujumla.

Kwa wapenda soka, familia hii imeweka rekodi ya kipekee nchini. Si tu imeongeza umaarufu kwa ligi hii lakini pia umaarufu wa mchezaji mmoja mmoja na timu zote kwa ujumla. Hata usajili wa mchezaji kutoka timu moja ya ligi kwenda nyingine umekuwa wa wazi zaidi. Wapenda soka wamekuwa na nafasi ya kujua uwezo wa mchezaji anayekusudiwa kusajiliwa na timu yao. Haya ni matokeo ya kuwekeza katika soka.

Natambua kuwa safari bado ni ndefu lakini angalau Azam TV wamefungua njia, na kuanzia hapo tunaweza kujifunza zaidi kutoka maeneo  mengine duniani ikiwamo England, ligi yao ndiyo yenye kutazamwa na watu wengi zaidi duniani.

Kwa mujibu wa kumbukumbu, Februari mwaka 1992 zilizokuwa klabu za ligi daraja la kwanza ziling’atuka kutoka Ligi ya Soka, kwa pamoja, na miezi mitatu baadaye Ligi Kuu ya Soka (Premier League) ikaanzishwa kama kampuni (Limited Company).

Sasa, jambo la kujifunza hapa katika safari yetu ya soka kwa kushirikisha vyombo vya habari kama Azam TV ni kwamba, ligi hiyo (Premier League/Limited Company) ikafanya uamuzi wa kuchukua hatua kubwa kwa kutoa haki za matangazo ya runinga kwa kituo cha televisheni cha Sky TV, kwetu hili tumelianza kiasi, tusonge mbele.

Lakini swali kubwa ni kwamba, tunawezaje kusonga mbele zaidi kama hatutambui juhudi zilizofanywa na sekta binafsi kama Azam TV katika uwekezaji wake huu? Kwa hiyo basi, Shirikisho la Soka Tanzania ni lazima lifanye jambo moja kubwa, litambue juhudi hizi. Kwanza, mchango wa RTD kwa wakati huo, pili, mchango huu wa Azam TV kwa sasa.

Binafsi ni mjumbe wa Kamati ya Habari na Masoko ya TFF, kamati ambayo imekuwa ikikumbwa na misukosuko kadhaa dhidi ya viongozi wake wa juu, mwenyekiti na makamu wake ambao wote wamekwisha kuondolewa katika kamati tendaji ya TFF, kwa hiyo vikao kushindwa kufanyika kwa miezi mingi sasa, na ndiyo maana nimechukua hatua hii ya kuandika gazetini baada ya kutokuwa na uhakika kama ushauri nilioufikisha kwa baadhi ya viongozi wa TFF unaweza kufanyiwa kazi. Ni kweli Azam TV inaingiza pesa kama ilivyokuwa kwa RTD kupitia wadhamini wa matangazo, lakini faida ya matangazo hayo kwa nchi ni kubwa zaidi ya pesa inayoingizwa kwa wamiliki wa vyombo hivyo.

Please follow and like us:
Pin Share