TIMU YA USHINDI WA NYALANDU WAPASUA JIPU KUHUSU KUMFATA NYALANDU

 

Nyalandu alijivua uanachama wa CCM na hivyo kujivua ubunge na sasa uchaguzi wa kumpata mrithi wake umepangwa kufanyika Januari 13.

Katika kampeni hizo, Digha ambaye alikuwa mhimili muhimu kwa ushindi wa Nyalandu, anasaidiwa na Narumba Hanje (mwenyekiti wa zamani wa CCM Wilaya ya Singida na Hadija Kisuda (diwani viti maalumu). Wawili hao pia walikuwa wajumbe tegemeo kwenye kampeni za Nyalandu.

Digha alisema kuwa amepokea kwa moyo mmoja na kwa furaha kubwa uteuzi wa CCM wa kumtaka aongoze kampeni hizo.

“Binafsi, uteuzi huu umenifurahisha sana kwa sababu umeondoa au umefuta kabisa maneno ya mitaani kwamba mimi na wenzangu Hanje na Kisuda ambao tulikuwa karibu sana na Nyalandu tutakisaliti chama chetu kwa kumfuata,” alisema.

Kuhusu siri ya uteuzi huo, alisema anaamini amechaguliwa kwa imani kwamba ataitendea haki nafasi hiyo kwa vile anatambulika vizuri kwa wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini na wanamuamini kwa kiwango kikubwa.

‘Kwa muda wote sijawahi kuwakosea wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini na wala sijawahi kuwadanganya,” alisema.

“Hiyo ni sifa mojawapo nzuri ambayo imetumika katika kuniteua. Sifa nyingine ni kwamba mimi ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida kwa hiyo nimekuwa karibu sana na wana CCM na wasio wanachama. Kwa hiyo, CCM Taifa imeona sitakiangusha chama changu kwenye uchaguzi huu mdogo.”

Alisema hadi sasa kampeni za CCM zinakwenda vizuri na kwamba hawajakwama kufanya mikutano yao.

“Pamoja na kwamba huu ni msimu wa kilimo, wana-CCM na wasio wana CCM wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kuja kusikiliza sera na ahadi za ilani za uchaguzi. Mikutano hii ya kampeni inatutia moyo kwamba Januari 13, mapema kabisa CCM itakuwa imejizolea kura za kutosha na kupitiliza,” alisema.

Alisema anamshukru Mungu kwa kuwa ameendelea kumpa mgombea wao Monko afya njema nguvu ya kumudu majukwaa ya kampeni.

Digha alisema mbinu walizokuwa wanazitumia enzi ya Nyalandu, hazitatumika kwenye kampeni za sasa kwa madai kuwa zimepitwa na wakati.

“Unajua dunia ya sasa kila siku inabadilika na mambo yake mengi nayo yanabadilika. Sisi CCM tunakwenda na wakati. Kwa sasa wapigakura wengi ni vijana, kwa hiyo mbinu zetu kwa sasa ni lazima ziwalenge vijana ambao ndio kundi kubwa,” alisema.

“Tunashukru na tunafarijika mno kwa vile mgombea wetu anauzika, analimudu jukwaa na anao uwezo mkubwa wa kuichanganua ilani ya uchaguzi na katiba ya CCM.”

Kabla ya uchukuaji wa fomu za kuomba kugombea, Digha alionekana kama angejitokeza kuwania ubunge kumrithi Nyalandu, ambaye ni rafiki yake wa karibu.

Alisema alipata ushauri kutoka kwa kiongozi wa juu katika Serikali ya Mkoa wa Singida kwamba asiombe nafasi hiyo kwa vile kitendo hicho kingesababisha mkanganyiko.

Katibu mwenezi CCM wa Wilaya ya Singida, Richard Kwimba alisema CCM imeonyesha dalili njema za kuibuka na kushindi mnono Januari 13 kuliko ule wa mwaka 2015.

Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vimetangaza kususia uchaguzi huo vikitaka mazungumzo na Tume ya Taifa Uchaguzi (NEC) kwa madai kuwa uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 43 ulikuwa ni vita baada ya wagombea wake, viongozi na wananchi kukamatwa na kushambuliwa.