Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) chini ya kikundi kazi cha fedha kina mipango ya kuanzisha Kituo cha Kimataifa cha Huduma za Kifedha (International Financial Services Centre – IFSC) hapa nchini kitakachovutia mitaji na uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.
Akizungumza wakati wa mkutano wa kikao kazi cha pili cha kamati hiyo uliofanyika mwishoni mwa wiki, Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt. Godwill Wanga alisema kuwa kupitia kikundi kazi cha fedha wamekuja na maazimio ya kuanzishwa kwa kituo hicho hapa nchini.

“Uanzishwaji wa kituo hiki utasaidia kuvutia uwekezaji wa mitaji mikubwa katika miradi mbalimbali mikubwa ndani na nje ya nchi na kukuza uchumi ”, alisema Dkt Wanga.
Pamoja na hayo Dkt Wanga aliweka wazi kuwa makundi mbalimbali ya watoa huduma yatafaidika na uanzishwaji wa kituo hicho.
“watakaofaidika ni pamoja na taasisi za fedha kama vile mabenki, masoko ya mitaji, lakini pia watoa huduma za usafirishaji kama vile makampuni ya ndege na mabasi, watoa huduma za chakula na wengineo ambao watakuwepo kwenye mnyororo hu wa thamani katika uwekezaji”.
Naye Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Bi. Sauda Msemo alisema kuwa uwepo wa kituo hicho hapa nchini utasaidia kutimiza azma ya Serikali ya kufikia pato la dola za Kimarekani tirioni moja ifikapo mwaka 2050.
“Kituo hiki kikishakuwa na mtaji wa kutosha kitavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi hivyo kurahisisha ufanyaji kazi wa miradi mingi mikubwa hapa nchini ambayo inahitaji fedha nyingi” alisema Bi Msemo.

Aidha, Bi Msemo alisema kuwa mitaji hiyo ikishawekezwa itasaidia kuweza kuuza bidhaa za Tanzania nje ya nchi ili kuweza kupunguza upungufu wa fedha za kigeni ambazo zitasaidia kama taifa kununua bidhaa za nje kwa fedha hizo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi Tanzania (PPP) Bw David Kafulila alisema kituo hicho ni muhimu sana kwa nchi kwani kitavutia wawekezaji wengi ambao watawekeza mitaji yao na kuamini kuwa mitaji yao iko kwenye mikono salama ya Serikali na kuchangia maendeleo ya nchi kwa kiasi kikubwa.
“Kupitia kikao hiki, wajumbe wameona kuwa ili kuweza kujenga uchumi wa zaidi ya dola za Kimarekani trilioni moja hauwezi kufikiwa kwa kutegemea mikopo na kodi,”
“Ni nchi 19 pekee duniani ambazo zimefikia kiwango hicho, hivyo basi Tanzania ina malengo hayo hivi sasa,” alibainisha Bw Kafulila.
Hata hivyo Kafulila alisema kuwa ili kufikia malengo hayo, mambo mbalimbali yanahitaji maboresho ikiwemo kanuni, sera na sheria.
Lakini pia matumizi ya teknolojia yanahitajika, ikiwa ni pamoja na kujiandaa kifikra na kuamini kuwa inawezekana kutimiza malengo hayo.
Bw Kafulila alisema huo ni wajibu wa kila Wizara na Idara zake kujikita katika kuitumia PPP kwa ajili ya kutekeleza miradi yao, wakifanya hivyo miradi mingi itafanikiwa kwa njia hii ya ubia kati ya sekta binafsi na umma kwani tafiti zinaonesha sekta binafsi zina teknolojia bora na zaidi kuliko sekta za Umma.

Naye Rais wa Chemba ya Wafanyabiashara Tanzania (TCCIA) Bw, Vicent Minja ambaye pia ni miongoni mwa wajumbe kwenye kikao hicho alisema kuwa wasilisho la uanzishwaji wa kituo hicho cha Kimataifa cha Fedha ni zuri na limepokelewa kwa mikono miwili na wadau.
Alisema kuwa ana matumiani kuwa mamlaka za juu za maamuzi zitapitisha mpango huo ili utekelezaji wake uweze kuanza mara moja.