Jana ilikuwa ni siku ya kusisimua kwa Bara la Afrika na hususani kwa wananchi wa Morocco baada ya timu hiyo kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia kwa kuifurusha Hispania kwa njia ya penati. 

Morocco iliandikisha rekodi nyingi sana katika michuano hiyo ambapo rekodi za kusisimua zaidi ni timu hiyo kuingia robo fainali ya Michuano ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza. Jambo la kuvutia zaidi kocha wa timu hiyo mzawa, Walid Regragui (47), amekuwa kocha mwafrika wa kwanza kuifikisha timu ya taifa katika hatua hiyo ya robo fainali. 

Baada ya kufuzu katika hatua hiyo, Morocco, watakutana na Ureno katika hatua inayofuata baada ya wareno kuibamiza Switzerland kwa ushindi mnono wa magoli 5-1. Imani ya Afrika bado ipo kwa wamorocco. 

Dunia imenyamaza, Dunia ipo kimya, hakuna stori ya soka baada ya Michuano hiyo Kombe la Dunia kusimama hii leo na kesho. Wapenda soka duniani kwote wamekuwa wanyonge kwa sababu watakosa burudani lakini Tanzania shangwe ndio kwanza zinaendelea. 

Watanzania wamehama Qatar na kurejea zao Ruangwa kule Uwanja wa Majaliwa kushuhudia mtanange kati ya Namungo na Yanga ambapo timu hizo zitakamilisha mechi za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara. 

Wanayanga wataangalia mechi hiyo wakitaka ushindi huku wapinzani wao wakiangalia mechi hiyo wakiombea wapinzani wao wapoteze point. Saa 1:00 Jioni watanzania tutakuwa Lindi tukitokea Qatar.