Mamlaka zote za Serikali zimeridhia ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mugumu, Serengeti mkoani Mara.

Kuridhiwa kwa ujenzi huo, kumeelezwa kwamba kumetokana na juhudi za watendaji kadhaa serikalini chini ya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.

Maombi ya ujenzi wa uwanja huo ni yalitokewa miaka minne iliyopita, lakini kumekuwapo danadana na urasimu wa muda mrefu uliokwamisha mradi huo.

Ujenzi huo ulikwama kwa miaka minne licha ya mmoja wa wadau, mfanyabiashara bilionea kutoka Marekani, Tudor Jones, kuwa tayari kusaidia kazi hiyo.

Jones ni mmoja wa matajiri walio karibu mno na kampuni ya Grumeti inayomiliki hoteli kadhaa wilayani Serengeti.

Mbunge wa Serengeti, Dk. Stephen Kabwe, amekiri kukamilika kwa taratibu zote, na kwamba kinachosubiriwa ni ujenzi.

Katika mahojiano yake na JAMHURI, mbunge huyo amesema, “Serikali imeridhia mpango huu wiki moja iliyopita, lakini bado official document (nyaraka rasmi) hazijatolewa. Utaona kuwa hazijatoka kwa sababu ni ndani ya wiki moja tu.

“Tumefanya vikao mimi, Waziri wa Uchukuzi, Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, tumekubaliana ujenzi uanze. Kumeonekana hakuna sababu za kuchelewa,” amesema.

Kebwe ambaye amekataa kutaja mdau wa ujenzi huo, licha ya JAMHURI kumtambua kuwa ni Jones, amesema, ujenzi utafanyika kwa awamu tatu, na unatarajiwa kuanza muda wowote kuanzia sasa.

Awamu ya kwanza itakuwa ni ya kilometa mbili; awamu ya pili itakapokamilika itawezesha ndege kubwa kutua. Hii ina masana ndege kutoka Ulaya, Marekani na Asia zitatua moja kwa moja katika uwanja huo.

“Wabia ni Grumeti Reserve, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na menejimenti-kwa maana ya sera na sheria zote-itakuwa chini ya Wizara ya Uchukuzi,” amesema Dk. Kebwe.

Mbunge huyo amesema uwanja huo utasaidia kukuza uchumi wa Serengeti na Taifa zima, na kwamba utasaidia kulinda mfumo wa ikolojia wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

“Kwa sasa ndege kati ya 40 na 50 hutua kila siku katika uwanja wa Seronera. Kukamilika kwa uwanja wa Serengeti kutasaidia kupunguza kelele za ndege na hivyo kulinda ecosystem ya Serengeti.

“Uwanja wa Mugumu umefanyiwa tathimini zote za kimazingira na kuonekana kuwa hauna madhara yoyote kwa mazingira na kwa wanyamapori,” amesema.

Dk. Kebwe amesema uwanja huo utasaidia kuongeza ajira, wananchi watauza bidhaa kwa watalii na utaweza kukuza soko la utalii nchini.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Mwakyembe, alipoulizwa, alisema, “Ni kweli uwanja huo utaanza kujengwa. Taratibu zinakamilika, hatuna sababu ya kuchelewesha jambo ambalo lina manufaa kwa taifa.

“Kweli nimekutana na wadau mbalimbali wakiwamo mawaziri wenzangu na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na kukubaliana juu ya jambo hili muhimu kwa uchumi wa taifa letu. Muhimu hapa ni kwamba tumeona mambo ya maana hayana sababu ya kucheleweshwa. Hatutaki urasimu maana dunia ya leo ni lazima mambo yaende kasi.”

1250 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!