Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetwaa tuzo ya taasisi iliyochangia gawio kubwa zaidi serikalini ikilinganishwa na taaasisi nyingine za Umma ambapo wametoa Tsh bilioni 181 katika mwaka wa fedha wa 2025/2026.
Gawio hilo ni ongezeko la bilioni 25 ndani ya mwaka mmoja, kwani katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 walitoa gawio la bilioni 155.7.
Tuzo hiyo wametwaa jana Ikulu jijini Dar es Salaam, ambapo Msajili wa Hazina Bw Nehemiah Mchechu ameitaja bandari kuwa ni mojawapo ya shirika la umma ambalo limefanikiwa kujiendesha na kupata faida na kila mwaka gawio linaongezeka kutokana na utendaji bora wa mamlaka hiyo.
“Gharama za uendeshaji wa TPA zimepungua kwa nusu trilioni, na hapo hapo wana miradi yao wanaiendesha kwa fedha zao za ndani, hivyo tutawaidia kuwaongezea fedha zaidi ili waweze kuboresha miundombinu yao ya bandarini”, alisema Bw Mchechu.

Bw Mchechu aliongezkuwa tuzo hizo zilizotolewa ni ishara ya kutambua juhudi zao na ni chachu ya kuhamasisha wengine kuendelea kufanya kazi kwa bidi, weledi na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao.
Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan alisema jinsi mashirika ya Umma yanavyoweza kutoa gawio Serikalini, ndivyo ulimwengu utakavyoiheshimu kwa kutatua changamoto zote na kupunguza utegemezi kwa mataifa ya nje.
Wakati wa utoaji wa magawio katika mwaka wa fedha wa 2024/2025, Rais Samia alisema zoezi hilo litakuwa endelevu na kuzitaka taasisi zote za umma ziwe na uwezo wa kujiendesha zenyewe na ziweze kutoa gawio Serikalini.
“TPA imewezeshwa nayo imeweza kuboresha bandari zake, hivyo Mamlaka ijikite kwenye uongozi na kuhakikisha huduma zinazohitajika na wawekezaji zinapatikana, kwani jukumu la kununua mitambo lipo chini ya wawekezaji” alisema Rais Samia.

Pamoja na hayo Rais Samia amewataka TPA kuboresha na kuitunza miundombinu ya hapo bandarini ili ivutie wawekezaji, kuongeza mapato kwa kuongeza kiasi cha mizigo kupitia bandari ya Dar es Salaam, kwani gharama zao nyingi zimepunguzwa na zinafanywa na wawekezaji.
“Kwa ujumla tumepokea jumala ya trilioni 1.28 kutoka kwenye taasisi mbalimbali za umma, hizi zitatusaidia kupunguza mzigo wa Serikali katika kusaidia kujenga bajeti yake ya mwaka”, alisema Rais Samia.
Taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo kuhusiana na muendelezo wake wa kutoa gawio serikalini kwa miaka mitatu mfululizo ni pamoja na kuongezeka kwa shehena ndani ya kipindi cha miezi kumi na moja kwa mwaka 2024/2025 mizigo imeongezeka kwa asilimia 11, ambapo imehudumia tani mil 23.9 kulinganishwa na tani mil 21.5 za miezi 11 ya mwaka 2023/2024.
Pia taarifa hiyo ilisema uwekezaji uliofanywa na DP World pamoja na TEAGTL umepelekea ongezeko la shehena mchanganyiko kutoka tani milioni 15.29 sawa na ongezeko la asilimia 11 ukilinganisha na kipindi ambacho TPA ilikuwa ikiendesha magati hayo kwa mwaka 2023/24 (tani milioni 13.75).
